*Yaendeleza ubabe Ukraine mataifa yakishuhudia
*Putin atishia kutumia silaa za nyuklia, aonya vikwazo
*Majeshi yake yadhibiti mtambo muhimu wa nyuklia Ukraine
*Waharibu mitambo kitengo cha ujasusi, maghala ya silaha
Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu
Urusi ni balaa. Ni maneno sahihi kutumika sasa wakati majeshi ya Urusi yakiendeleza kila kilichotajwa na Rais Vladimir Putin kama ‘operesheni ya kijeshi ndani ya Ukraine’.
Leo ni siku ya 11 tangu taifa hilo kubwa duniani lilipoanzisha ‘operesheni’ usiku wa Alhamisi ya Februari 24, mwaka huu; operesheni inayolaaniwa na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensnky, akiita ni ‘uvamizi’.
Tayari kumekuwapo mamilioni ya watu wanaolikimbia taifa lao kutafuta maeneo na makazi salama katika mataifa mengine, wakiacha nyuma yao majeshi ya Urusi yakiisambaratisha Ukraine kwa makombora mazito.
Huenda nguvu za kinyuklia ilizo nazo Urusi ndizo zinaipa jeuri, huku mataifa mengine yakishindwa kuingilia kati kuchukua hatua za kijeshi kuwadhibiti askari wa Putin.
Tayari vikosi vya nyuklia vya Urusi vimewekwa katika hali ya tahadhari na utayari, kitendo ambacho ni sawa na watu wawili wenye ugomvi wakiwa wamesimama kwenye dimbwi la petroli, mmoja akiwa na kijiti cha kiberiti akisubiri kuguswa tu, akiwashe.
Ni katika mazingira hayo ambapo mataifa karibu yote yamekaa pembeni yakishuhudia Ukraine inavyonyanyaswa kijeshi na Urusi na kusababishiwa kila aina ya hasara, unaweza kujiuliza; kwa nini yaliituma Ukraine kuichokoza Urusi?
Urusi imekuwa ikielekeza mabomu na makombora yake katika maeneo nyeti na sasa majeshi yake yanaudhibiti mtambo wa nyuklia wa Zaporizhia, ambao ni muhimu kwa uchumi wa Ukraine.
Mtambo huo unaozalisha Megawati 5,700 sawa na nusu ya mahitaji ya umeme ya Ukraine, umetekwa baada ya mapigano makali katika eneo la karibu.
Taarifa zinasema wakati wa mapigano hayo makombora kadhaa yaliangukia kwenye kinu cha nyuklia na kusababisha mlipuko mkubwa uliodhibitiwa na askari wa Ukraine.
Haijaweza kufahamika mara moja ni majeshi yapi yaliyotupa makombora hayo huku pande zote mbili zikitupiana lawama.
Ulaya na Marekani wamelaani uvamizi katika mtambo wa kuzalisha umeme kwa nyuklia, wakisema unaweza kuleta maafa katika bara zima.
Wakati hayo yakiendelea, Rais Putin ametoa onyo kwa mataifa yanayopinga operesheni zinazofanywa na Urusi akisema yanasababisha tatizo kuwa baya zaidi.
Marekani na mataifa kadhaa wameiwekea vikwazo vya kiuchumi Urusi, hatua ambayo Putin anasema itasababisha uhusiano kuzidi kuwa mbaya, na ni sawa na kutangaza vita dhidi ya Urusi.
Hata hivyo, Putin ameshikilia msimamo kwamba operesheni inayofanywa na Urusi lazima itafanikiwa, kwa kuwa lengo ni kukabiliana na hatua zisizo ‘rafiki’ dhidi ya taifa hilo.
Urusi inavyoendesha operesheni
Vita hii inahusisha wanajeshi 200,000 wa Urusi wakiwa wamegawanyika katika vikosi 60, ambavyo ndani yake wamo jumla ya askari 60,000 kati ya hao 200,000 wenye mafunzo maalumu ya kuendesha vita ya angani, silaha za masafa marefu na jeshi la wanamaji.
Taarifa za kijeshi zinasema vikosi hivyo vinaongozwa na kikosi maalumu chenye majukumu ya kuratibu namna ya kuendesha vita.
Awali, Urusi ilitanguliza vikosi viwili vyenye wanajeshi 40,000 sambamba na wanamgambo kutoka majimbo yaliyojitenga na Ukraine ya Donetsk na Luhansk.
Ndani ya majeshi ya Urusi yaliyoko vitani Ukraine, kipo kikosi maalumu cha kuchunguza mipango ya majeshi ya Ukraine na kuandaa mikakati ya kuhujumu mbinu zao.
Kikosi hicho ndicho kinachotajwa kuongoza mashambulizi ya makombora na mizinga iliyoharibu viwanja vya ndege na mitambo ya rada katika siku ya kwanza tu ya mashambulizi.
Pia ndicho kilichoongoza mashambulizi kuharibu makao makuu ya Kitengo cha Ujasusi wa Jeshi la Ukraine pamoja na maghala ya risasi.
Maeneo yanayodhitiwa na Urusi
Mpaka sasa jeshi la Urusi limefanikiwa kudhibiti eneo la Zaporizhia ulipo mtambo wa nyuklia; na Hostomel, mji ulio nje kidogo ya Kiev ambalo ni eneo muhimu na la kimkakati kwa Ukraine.
Hostomel ipo kaskazini magharibi mwa Kiev na ndipo ulipo uwanja wa ndege wa kimataifa wenye jukumu la kusafirisha mizigo na bidhaa zinazozalishwa au kuingizwa Ukraine.
Mapambano yanaendelea katika maeneo ya Chernihiv, Sumy, Kharkiv, Mariupol na Kharson ambako Urusi wamekumbana na upinzani mkali, ikiwamo ndege zake kadhaa kudunguliwa.
Katika kukabiliana na tishio la kudunguliwa ndege zake, sasa Urusi inafanya mashambulizi kwa kutumia makombora ya masafa marefu yenye ubora wa hali ya juu.
Mashabulizi hayo hutekelezwa kwa kutumia mifumo ya aina mbalimbali kama yale yanayobebwa na ndege za kisasa, matumizi ya bunduki aina ya 2S7 yenye uwezo wa kufyatua risasi hadi umbali wa kilometa 37.
Matumzi ya ‘Kikosi Z’
Urusi wanatumia makomandoo wa ‘Kikosi Z’ kutoka Chechnya, maarufu kama Kadyrovtsy.
Kikosi hiki kimesheheni askari hodari katika mapigano na kazi yao kubwa ni kutekeleza mashambulizi ya kutisha yakilenga kuvitia hofu vikosi vya Ukraine.
Kikosi hiki kilianzishwa na majeshi yaliyojitenga na kuendesha mapambano na Urusi mwaka 1994, kikiongozwa na Akhmad Kadyrov.
Hata hivyo, mwaka 1999 kiongozi huyo alijiunga na majeshi ya Urusi na kuanza kushirikishwa kwenye utekelezaji wa shughuli za ulinzi wa viongozi wa Urusi na kudhibiti uasi nchini humo.
Kwa upande mwingine, mashambulizi ya Urusi yanaongozwa na majeshi yaliyoboreshwa tangu mwaka 2008 yakihusisha askari maalumu wa miguu, askari wa kuongoza magari, ndege na silaha za kisasa za kivita.
Kwa nini Urusi inajiamini angani?
Kwenye uwanja mapambano, majeshi ya Urusi yanaripotiwa kutumia ndege aina ya Su-57 ambayo ni toleo la kizazi cha tano cha ndege aina ‘The Sukhoi’.
Su-57 inatajwa kuwa ni ndege ya kivita iliyoboreshwa kwa viwango vya juu, ikitumia teknolojia aina ya ‘stealth’ tangu Urusi ilipoanza matumizi ya ndege za kivita aina ya MiG-25 miaka ya 1960.
Toleo hili jipya ni la mwaka 2020, na ndege hii ina uwezo wa kuruka kwa spidi ya ‘supersonic’ ikiwa na uwezo wa kuzishambulia ndege nyingine zilizopo angani, kufanya mashambulizi ardhini na majini.
Ubora mwingine wa ndege hiyo ni uwepo wa mfumo wa kompyuta unaosaidia kujiendesha yenyewe na uwezo wa kubeba makombora aina ya ‘hypersonic missiles’.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu, kuhusu ndege za kijeshi zinazomilikiwa na Marekani, China na Urusi; Urusi inaonyesha kuwa na idadi ya ndege za kisasa za kivita 1,571, miongoni mwa ndege hizo zimo aina ya 273 Su-24, 192 Su-25, 350 Su-27/30/35 na 125 Su- 34.
Urusi inaweza kuwa imepiga hatua kubwa angani kutokana na ndege yake ya MiG-25 (Mikoyan-Gurevich-25) ya miaka 1960 kuwa na uwezo wa kuruka kwa spidi ya kilometa 3,494 kwa saa; ilhali Marekani ambayo ndiyo iliyokuwa imeonyesha kupiga hatua kubwa ndege zake za kivita kama F-108, SR-71, na B-70 zenyewe zikiwa na uwezo wa kuruka kilometa 3,018 kwa saa mwaka 1960. Kwa sasa ndege hizi zinakwenda kwa kasi zaidi.
Nguvu za kinyuklia
Teknolojia ya nyuklia na uwezo ilionao Urusi inatishia dunia nzima, hali inayofanya mataifa mengine kuhofia kuingilia kati vita ya Ukraine.
Kwa mujibu wa ripoti ya wanasayansi wa Marekani, mpaka sasa Urusi inamiliki silaha za nyuklia 5,977, idadi inayolifanya taifa hilo kuwa la kwanza kwenye umiliki wa silaha za nyuklia.
Marekani inamiliki silaha za nyukilia 5,428, ikifuatiwa na Ufaransa (290) na Uingereza (225).
Jarida linaloandika masuala ya ‘atomic’ la Marekani linaeleza kuwa silaha za nyukilia 4,447 ziko tayari kwa matumizi muda wowote na nyingine 1,588 kati ya hizo zimetegeshwa kama makombora aina ya ‘ballistic Missiles’ huku nyingine zikiwa kwenye vituo vya kurusha makombora mazito.
Wanaioipinga Urusi wanasema inatishia amani ya mataifa mengine kama Marekani na washirika wake kutokana na uwezo wa makombora yake ya nyuklia ya masafa marefu (ICBMS).
Makombora hayo yanatajwa kuwa na uwezo wa kurushwa kutoka Urusi na kutua Ulaya na hata Marekani ndani ya dakika 20 tu.
Jarida la Atomic linasema kichwa kimoja cha kombora la nyuklia la Urusi kina uzito wa kati ya tani 300 hadi 800 za TNT (milipuko ya gesi).
Vyanzo mbalimbali vya habari vinaeleza kuwa uzito wa kombora moja la nyuklia likidondoshwa ardhini linaweza kuharibu eneo lenye ukubwa wa Jiji la Washington au London kwa muda mfupi.
Kikosi cha Kaskazini
Urusi mbali na kujivunia uwezo wake wa kumiliki silaha za nyuklia, inajivunia manuari zenye uwezo mkubwa wa kijeshi ikiwamo yenye urefu wa mita 252 iliyopo katika kambi ya Kikosi cha Kaskazini, Arctic.
Manuari hiyo iliyopewa jina la ‘Pedro the Great’ ni meli kuu na muhimu kwa majeshi ya Kaskazini yaliyoundwa na Urusi ikiwa na sifa ya kubeba kila aina ya silaha na kuendeshwa kwa nguvu za nyuklia.
Walinganisha Marekani na Urusi
Wakati mataifa ya Ulaya na Marekani yakichukua hatua za ziada za kuidhibiti Urusi kwa kuiwekea vikwazo kutokana na kitendo cha kuivamia kijeshi Ukraine, Marekani imewahi kuzivamia nchi 35 na kuzishambulia kijeshi kwa hoja kwamba inaendesha operesheni maalumu katika nchi hizo.
Mataifa yaliyovamiwa na Marekani tangu mwaka 1950 hadi 2020 ni:- Korea iliyovamiwa mwaka (1950-53), China (1950-53), Guatemala ilivamiwa mwaka 1954, Indonesia mwaka 1958, Cuba (1959-60), Guatemala mwaka 1960, Belgian Congo mwaka 1964, Guatemala mwaka 1964, Dominican Republic (1965-66), Peru mwaka 1965 na Laos (1964 -73).
Mataifa mengine ni Vietnam (1961-73), Cambodia (1969-70), Guatemala (1967-69), Lebanon (1982-84), Grenada (1983-84), Libya mwaka 1986, El Salvador (1981-92), Nicaragua (1981-90), Iran (1987-88), Libya mwaka 1989, Panama (1989-90), Iraq mwaka 1991 na Kuwait mwaka 1991.
Aidha, iliivamia Somalia (1992-94), Bosnia mwaka 1995, Iran mwaka 1998, Sudan mwaka 1998, Afghanistan mwaka 1998, Yugoslavia – Serbia mwaka 1999, Afghanistan mwaka 2001, Libya mwaka 2011, Iraq na Syria mwaka 2014.
Vilevile Marekani iliivamia Somalia mwaka 2011 na Iran mwaka 2020 na bado inaendesha operesheni za kijeshi katika mataifa hayo mawili.