Sina hakika kama lipo suala linaloweza kumpotezea binadamu muda wake bila manufaa yoyote kama kupitia taarifa zinazotufikia kwa njia ya mtandao. Watumiaji wa mtandao duniani wanakadiriwa kufikia bilioni 3.2 na wengi wao, kila siku wanasambaza taarifa za kila aina mtandaoni.

Nyingi ya hizo hazina manufaa yoyote kwa mpokea taarifa. Wanaofaidika zaidi kiuchumi ni wamiliki wa kampuni zinazodhibiti na kuuza taarifa zetu za mienendo yetu ya matumizi ya mtandao kwa wauza bidhaa na huduma.

Lakini pamoja na kuwapo kwa taarifa nyingi za kipuuzi hutokea pia kupenya taarifa zenye manufaa makubwa kwa binadamu; taarifa zinazosaidia kujenga uhusiano mzuri miongoni mwetu.

Ili mradi unamiliki simu, si rahisi kuepuka mtandao siku hizi. Huwa naepuka sana kufungua video ninazopokea kwa sababu zinatumia kwa kasi kubwa muda wa data. Lakini siku za hivi karibuni nilifungua video moja ambayo ilinipa somo zuri.

Ilikuwa ya muumini wa dini mojawapo yenye wafuasi wengi. Siitaji dini hiyo na nitafafanua sababu. Mzungumzaji, akihutubia hadhira ya waumini wenzake, aliwasihi juu ya umuhimu wa kujenga uhusiano mzuri na binadamu wengine, hata wale ambao si wa dini yake, kwa kigezo cha kupima jinsi anayemulikwa anaishi maisha yake.

Alisema: “Wapo wengi wa dini nyingine, ambao wanafanana sana kwa tabia zao kama dini yetu inavyofundisha. Kuna wengine ambao hawana dini kabisa, lakini wanaishi tunayofundisha sisi.”

Aliongeza: “Kuna aina mbili ya watu: au ni ndugu zako katika imani, au ni wenzako katika utu.”

Kwa kifupi alisisitiza umuhimu wa kumpima mtu kwa tabia yake na siyo kwa imani anayohusishwa nayo.

Kwenye moja ya hotuba zake mwanaharakati Mmarekani wa asili ya Afrika, Martin Luther King Jr. alisema: “Nina ndoto kuwa siku moja watoto wangu wanne wadogo wataishi kwenye taifa ambapo watapimwa kwa tabia yao na siyo kwa rangi ya ngozi yao.”

Sababu ya msingi ya kutotaja dini ya mzungumzaji ni moja: najikita kwenye ujumbe na siyo kwa anayetoa ujumbe. Kwa hulka ya binadamu, ujumbe unapounganishwa na imani ya mtoa ujumbe mada zinaweza pia kuongezeka: badala ya kuwa mada moja zikawa mbili.

Aidha, upo uwezekano mkubwa kuwa si waumini wote wa mtoa mada watakaokubaliana na ujumbe wake kuwa matendo ya binadamu ni muhimu kuliko utambulisho wa dini yake.

Lakini, suala la msingi zaidi la kutotaja dini ni kuwa mjadala wangu si wa dini, bali wa ujumbe ambao umetolewa katika muktadha wa dini. Ni ujumbe ambao unaweza kutumika katika muktadha mwingine wowote: kama vile siasa, na katika nyanja nyingine zozote za maisha.

Ni ile tabia ya binadamu ya kumuona na kumpima binadamu mwenzake kwa utambulisho wa anayemulikwa, ndiyo suala linalotufunga macho na kutuziba masikio kuona na kusikia sifa nyingine ambayo haiko bayana.

Kama ipo faida ya msingi ya kumpima mtu kwa matendo yake na siyo kwa jinsi anavyojitambulisha au anavyotambulishwa na watu wengine, itakuwa ni kumvua kinga inayomfunika na kuficha ukweli, au kumtoa doa ambalo linaficha ukweli badala ya kubainisha hulka yake halisi.

Kwa lugha nyingine, kama hili linafanyika bila ushabiki wa aina yoyote ila tu kwa madhumuni ya kubaini ukweli juu ya uhusiano baina ya binadamu mmoja na binadamu wenzake, tunaweza kujifunza kuwa wale tunaowadhania ni maadui ni marafiki zetu, na wale tuliyowadhania marafiki tukakuta ni maadui zetu.

Zaidi ya hapo tunaweza kujifungulia fursa ya kuthibitisha tu kuwa hali tuliyodhania ndiyo ukweli ni kweli, kama tulivyoidhania. Naamini kuwa ni kazi itakayomuongezea kila binadamu marafiki na kumpunguzia maadui.

Inakadiriwa kuwa wanazaliwa watoto wanne duniani kila sekunde, watoto wanaoanza maisha ndani ya dunia iliyojaa kila aina ya tabaka na migawanyiko. Baadhi ya migawanyiko ni ya kweli na hatuwezi, kwa ndoto tu, kuifanya iishe au iondoke. Norway ni nchi tajiri kuliko Tanzania na hiyo inatuweka raia wa nchi hizo mbili katika matabaka mawili tofauti.

Hata hivyo, baadhi ya migawanyiko ni ya kubuni na inahitaji kuchunguzwa na kuthibitishwa, iwapo tunakubaliana juu ya faida ya kupunguza mifarakano na kutoaminiana kati ya binadamu mmoja na mwenzake. Akijitokeza mtu na kusema kuwa raia wa Norway ni watu wabaya, pamoja na ukweli kuwa siyo wenzetu kwa maana ya kuwa matajiri kuliko sisi, tunahitaji kuyaweka maelezo kama haya kwenye mizani na kumpima mtu kwa mwenendo wake na siyo kwa uraia wake.

Kikwazo kimoja dhidi ya kupunguza tofauti zilizopo kati ya binadamu ni matumizi ya kawaida ya lugha. Neno moja tu la kugawa watu linaweza kuzima kabisa hotuba ndefu ya maelewano na maridhiano ya mtoa mada wa kwenye video, au ya Dk. Martin Luther King Jr.

Tunaweza kutofautiana juu ya ugumu wa kufikia maridhiano, lakini hatuwezi kupuuza umuhimu wa binadamu kuendeleza jitihada za kupunguza tofauti zetu.