Na Joe Beda Rupia Jamhuri Media
Hii ni aibu. Aibu kubwa kweli kweli! Kwa hakika ni ujinga unaoachwa kuendelea bila kukemewa. Matokeo yake tunabaki kujificha kwa kufumba macho.
Hivi, unaweza kujificha kwa kufumba macho? Nao huu ni ujinga mwingine. Lakini ndivyo tunavyofanya mara kwa mara. Tunajificha kwa kufumba macho.
Bahati nzuri macho yanafumbika. Bahati mbaya masikio hayafumbiki. Kwa hiyo unajificha (kwa kufumba macho) lakini (kwa kuwa hujalala usingizi) kila kitu unakisikia!
Ni ujinga kwa wazee wa sasa kufumba macho. Ni kama vile kufunika kombe mwanaharamu apite. Sasa inakuwaje huyo ‘mwanaharamu’ anapogoma kupita?
Ndiyo. Umefunika kombe, halafu naye (mwanaharamu) anasimama tu. Hapiti. Utalifunika hilo kombe hadi lini? Ujinga mwingine huu.
Kwa kawaida sisi binadamu ni wabinafsi na aghalabu, kikitokea kitu cha hovyo au cha aibu, hutafuta ‘mbuzi wa kafara’.
Yaani wa kumtupia lawama. Badala ya kukubali kuwa na wewe mwenyewe ni sehemu ya waliochangia uozo, unamtafuta wa kumtwisha zigo la misumari.
Hapa na mimi ninasimama kama binadamu nikijiuliza, ni nani kati ya LATRA na BASATA (si mimi) anayestahili kubebeshwa zigo la ujinga huu unaoendelea kwenye vyombo vya usafiri hasa mabasi yaendayo mikoani?
Yaani, unapanda basi zuri kabisa Stendi ya Magufuli ukielekea ama Mwanza, Arusha au hata Dodoma. Bei elekezi; viti vya kulala na viburudisho kama peremende, biskuti, soda na maji unapata.
Mbele wameweka ‘video’ kukuburudisha wewe na abiria wengine mnapoendelea na safari ili hata msifuatilie sana mwendokasi wa dereva kwa siku hiyo. Zamani walikuwa wanasema ‘safari na muziki’.
Lakini sasa ni muziki wa aina gani? Unastahili kupigwa au kuonyeshwa kwa watu wote? Je, safarini ni wakati sahihi? Ndani ya basi ni sehemu sahihi kwa muziki huo?
Unalenga kumburudisha nani? Una maudhui gani? Yanajenga taifa? Yanaimarisha utamaduni wa Mtanzania? Maswali ni mengi na magumu, lakini muziki unapigwa.
Majina tofauti tofauti yanapita. Mengine makubwa kweli kama Diamond. Mengine ya kawaida kama Roma na Stamina na mengine hata haujawahi kuyasikia kama Dullah Makabila.
Ukifanya tathmini ya muziki na nyimbo zote (au walau asilimia 98) ni za kijinga kabisa kimaudhui, kiuchezaji na hasa kwa kuwa zinapigwa au kuchezwa sehemu ambayo si sahihi.
Ndani ya basi kuna watoto wadogo kabisa (wanaopakatwa), watoto wa shule, vijana wa rika mbalimbali, wanawake, wanaume, watu wazima na hata wazee; lakini muziki unaopigwa ndio balaa! Haubagui rika wala jinsia.
Wanaoshiriki kucheza na kuimba kwenye nyimbo hizo (hasa wanawake) wote wanaelekeza bila soni, mtanisamehe kwa kukosa maneno mazuri zaidi, namna ya kufanya ngono! Jamani! Tunajenga taifa la namna gani? Nani wa kuukemea ujinga huu?
Mwanamke anacheza muda wote ameelekeza makalio kwenye kamera. Ukitazama kwa jicho la kikubwa unaona kabisa hana nguo ya ndani huyu!
Maneno yanayoimbwa ili yeye acheze hayastahili kuimbwa katika hadhara inayosafari ndani ya basi la abiria mchanganyiko.
Ukitazama abiria wanaoangalia video, unakuta vijana wamekodoa macho; wazee wengine wanaibiaibia kuona huku wengine, hasa akina mama, wakijificha kwa kufumba macho.
Lakini hakuna hata mmoja anayepaza sauti kumwambia kondakta kuwa nyimbo anazopiga si mahala pake! Aibu. Yaani kizazi cha wazee wa sasa kinakubali kuendeshwa na fikra za akina Dullah Makabila?
Hakuna mzee mwenye uwezo wa kuwakemea makondakta? LATRA, kama walifanikiwa kuzuia mihadhara kwenye mabasi, wanashindwaje kuzuia nyimbo hizi zisizo na maadili?
BASATA nao wapo wapi? Kwa nini wanaruhusu nyimbo na uchezaji wa aina hii?
Nyimbo hizi zikipigwa kwenye majumba ya burudani saa tano au saa saba usiku, hakuna atakayelaumu kwa kuwa wakati huo ni sahihi na waliokwenda huko ni watu sahihi.
Lakini kwenye mabasi ya abiria? Hapana! Hapana! Hapana.
Chambilecho Mzee Mkapa, kuruhusu haya kuendelea ni “ulofa na upumbavu!”