Shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ya kuboresha utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika sekta ya afya na Ukimwi, SIKIKA, wiki iliyopita limetoa taarifa yenye kushtua juu ya upatikanaji wa dawa na wagharimiaji.
Utafiti wa shirika hili umebaini kuwa kuna upungufu wa jumla wa asilimia 26 kwa dawa za malaria katika mikoa yote nchini. Upungufu huu hautokani na ukosefu wa fedha, bali mipango dhaifu ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD).
Tunafahamu baadhi ya vyombo vya habari vimeandika kukemea upungufu huu na hatari inayolinyemelea Taifa, kwa wagonjwa wa malaria kufika hospitalini wakaambiwa hakuna dawa, hasa maeneo ya vijijini.
Upungufu huu unamaanisha kuwa juhudi zote za Serikali kupambana na malaria na hasa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, zinaweza kuishia hewani ikiwa dawa hazitapatikana kwa wakati. Kama kikwazo ni Sheria ya Ununuzi ya Mwaka 2004 yenye kuchelewesha ununuzi kwa wastani wa miezi minane, ufanyike utaratibu wa dharura kufanya ununuzi wa haraka.
Hata hivyo, kubwa lililotushtua katika taarifa hiyo, ni suala la nani anagharimia dawa tunazotumia kutibu watu wetu hapa nchini. Taarifa ya SIKIKA imesema kati ya mwaka 2003 na 2010 wafadhili walitenga dola milioni 450 kugharimia dawa za malaria nchini kwa asilimia 100. Mkurugenzi Mtendaji wa SIKIKA, Irenei Kiria, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hadi sasa wafadhili ndiyo wanaogharimia dawa hizo kwa asilimia 100.
Kwa wastani inaonesha nchi yetu inatumia kiasi cha Sh bilioni 102 kwa mwaka kununulia dawa. Tumesikitishwa mno na taarifa kwamba wafadhili ndiyo hugharimia kwa asilimia 100 dawa za malaria na nyingine katika nchi yetu. Mara nyingi tunajitia aibu wenyewe. Si kweli kwamba Serikali yetu haiwezi kupata Sh bilioni 102 kwa mwaka kutibia watu wake.
Ni hatari kuwategemea wafadhili kwa asilimia 100 kwani siku wakiamua kuasi na wasitusaidie tutakufa kama kuku wa mdondo. Ikiwa SIKIKA haikupotosha, Serikali inawajibika kuwapa majibu Watanzania kodi zetu tunazolipa zinakwenda wapi, kama tunashindwa kununua hata dawa za matibabu. Tunasema tubadilike, nchi yetu isiwe ombaomba kupita kiasi.