Kambi ya Upinzani bungeni imeanza kuonesha mambo yaliyo kinyume na maana halisi ya upinzani, kuhakikisha inapinga kila kitu kinachokuja mbele yao.
Hilo ni jambo la kusikitisha na kushangaza ikichukuliwa kwamba kambi hiyo imesheheni watu walio waelewa wa mambo mengi mbalimbali.
Kiutaratibu na kikanuni, Bunge, kwa mfumo wa mabunge ya Jumuiya ya Madola, huwa na kamati za kudumu zinazoundwa na wabunge wenyewe. Kuna kamati ambazo ili ziweze kufanya kazi ya kuisimamia vizuri serikali bila kuyumbishwa, zinapaswa ziwe za wabunge wa kambi ya upinzani. Kamati hizo kwa hapa kwetu ni za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Lakini, hata hivyo, jukumu la kuunda kamati hizo linapaswa liwe la Spika wa Bunge. Hiyo maana yake ni kwamba Spika hana upande, anawajua wabunge wote, kwa Upinzani na kwa chama tawala.
Yeye ndiye mwenye kujua ni nani anayeweza na anayefaa kuwa katika kamati fulani kulingana na anavyoliona Bunge lake lilivyo. Spika hawezi kuteua mjumbe wa kamati yoyote nje ya wabunge
Kwa hiyo, katika kuondoa vurumai bungeni, kazi inayofanywa na Spika wa Bunge haipaswi kuingiliwa na yeyote – awe mbunge wa Upinzani au wa chama tawala. Hiyo ndiyo maana ya uspika.
Lakini jambo la kushangaza wapinzani wanaona kumpinga hata Spika ni sehemu ya jukumu lao! Siyo kwamba wanapinga ya Serikali peke yake, hata maelekezo ya Spika wanaona wanayo haki ya kuyapinga, kitu kilicho kinyume kabisa na utaratibu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola.
Kwa mfano, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amesema upande wa Upinzani ulio chini ya Muungano usio rasmi wa Ukawa, hautaongoza kamati mbili za kudumu za Hesabu za Serikali (PAC) na Serikali za Mitaa (LAAC) hadi ofisi ya Spika itakapobadilisha uteuzi wa wajumbe wa kamati hizo.
Kwa maana hiyo ni kwamba wabunge wa Upinzani ndiyo wanaotaka kumwendesha Spika badala ya Spika kuwaendesha wao.
Tangu Spika Job Ndugai afanye uteuzi wa wajumbe wa kamati hizo kama kanuni zinavyoagiza, Ukawa wamesusia kuteua wenyeviti wa kamati hizo kwa madai ya kwamba hawataki kupangiwa wajumbe wa kamati hizo. Lakini Spika kafanya kazi yake kwa mujibu wa kanuni za Bunge, wao wanataka kumwingilia ndipo wafanye mambo yao. Hilo ni jambo lisilowezekana.
Hivi kweli tukiangalia hapo tunapata picha gani? Ina maana wabunge wa Upinzani hapa Tanzania wanaamua kutunga kanuni zao ambazo hazimo kwenye kanuni za mabunge ya Jumuiya ya Madola? Kweli huo ndiyo upinzani unaotakiwa?
Tunaposema upinzani hatumaanishi upinzani wa kuvuruga na kuvunja, upinzani unaofahamika ni upinzani wa kujenga na kuboresha na siyo wa kuvuruga kama huu unaojionesha hapa nchini kwetu.
Lissu anasema ni bora wasiziongoze kamati hizo kwa kuwa katika kila kamati kuna wajumbe sita wa Ukawa wakati kila kamati ina wajumbe 23.
Anashangaa eti Kamati ya Ukimwi ambayo nayo ina wajumbe 23 imetengewa wajumbe 12 wa Ukawa. Kwa mujibu wa Lissu, Kamati ya Ukimwi haina umuhimu sana kwa Ukawa, lakini kinchi kamati hiyo ina umuhimu mkubwa na wa kipekee.
Hivi kweli mbunge huyo anataka kusema kwamba janga la Ukimwi halina umuhimu? Ina maana wananchi wakipangiwa pesa ambazo zinasimamiwa na PAC na LAAC pesa hizo zitakuwa na maana yoyote iwapo wananchi wote watakuwa wamemalizwa na Ukimwi? Kwa hiyo, tunaweza kuona kwamba kwa Lissu pesa ni muhimu sana kuliko afya za wananchi! Hayo ndiyo mawazo ya upinzani kweli?
Jambo jingine la kustaajabisha ni kwamba upande wa Upinzani unadai kwamba wajumbe wote walioteuliwa na Spika Ndugai kuingia kwenye Kamati za Kudumu za Bunge za PAC na LAAC hawana uwezo wala sifa za kuingia kwenye kamati hizo!
Ndiyo maana wanataka wapinzani waachiwe jukumu la kuteua wajumbe wa kamati hizo wao wenyewe. Wanasahau kwamba kwa kufanya hivyo tayari wanakuwa wamegeuza kanuni za Bunge.
Hilo la kugeuza kanuni za Bunge hawaliangalii ilimradi matakwa yao yametimia. Lakini je, Bunge lipo kutimiza matakwa ya kila mbunge mmoja mmoja au kutimiza matakwa ya kibunge kwa ujumla kwa faida ya wananchi? Sababu kanuni za Bunge zipo, si kwa wabunge waliopo peke yao bali hata kwa wabunge wengine baada ya hawa waliopo kumaliza muda wao.
Haiwezekani kila mbunge akawa anataka Bunge liendeshwe kadiri anavyotaka yeye na akija mwingine hivyo hivyo. Ndiyo maana zikawekwa kanuni za Bunge kusudi kila mbunge atakayekuja awe anaelewa ni kipi kinatakiwa kifanyike vipi.
Jambo jingine ni kwamba kwa nini wapinzani waonekane wanadharauliana? Madai ya kwamba kuna baadhi ya wabunge wa upinzani wasioweza lolote yanatoka wapi? Hawa wabunge wa upinzani anaowasema Lissu kwamba hawana uwezo waliwezaje kuwa wabunge? Na kama ni wapinzani wasio na uwezo kwa nini alaumiwe Spika Ndugai badala ya kuwalaumu waliowawezesha kuwa wabunge?
Hiyo inajionesha wazi kuwa kumbe Upinzani hauwezi kitu, isingekuwa upinzani uko makini na unaweza ukawaleta bungeni wabunge wanaotiliwa mashaka na hao hao waliowawezesha kuwa wabunge. Kwa hilo, unapaswa ulaumiwe upande wa upinzani.
Sababu wabunge wote wakishaingia bungeni wanachukuliwa kuwa wana uwezo sawa na haki sawa. Kwa nini Upinzani uwazoe tu watu usiowaamini na kuwaleta bungeni wakawe wawakilishi wa wananchi na watunga sheria wao?
Kwa hiyo, kwa jambo hilo Lissu hana hoja yoyote, anapaswa aone kwamba hapa nchini hakuna upinzani wa maana, sababu, kwa mujibu wa mawazo yake, upinzani unawazoa tu watu mitaani na kuwapigia debe waingie bungeni wakati hawawezi lolote. Hilo siyo jambo la kumlaumu Ndugai ila Upinzani ujilaumu wenyewe.