Vyama vya upinzani katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) vinakamilisha
utaratibu kumteua mgombea mmoja
watakayemkabidhi jukumu la kupeperusha
bendera katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika nchini humo Desemba 23, mwaka
huu.
Kiongozi wa Chama cha UDPS, Felix
Tshisekedi, Vital Kamerhe wa UNC na Freddy
Matungulu wa BISCO walikuwa miongoni mwa
viongozi wakuu kutoka vyama vya upinzani
waliokuwepo katika kikao hicho kilichoitishwa
mahususi kuangalia uwezekano wa kuwa na
mgombea mmoja.
Katika mkutano huo, Jean-Pierre Bemba
Gombo, kiongozi wa Chama cha upinzani cha
MLC na Gavana wa zamani wa Mkoa wa
Katanga, Moise Katumbi, nao pia walikuwa
na uwakilishi wao katika hafla hiyo. Hata hivyo
Chama cha ECiDé kinachoongozwa na Martin
Fayulu hakikuwa na mwakilishi.
Viongozi hao walitoa tamko la pamoja
kupongeza uamuzi wa Rais Joseph Kabila
kuheshimu katiba baada ya kutangaza

kutowania muhula wa tatu.
Wakati hayo yakijiri, Tume ya Uchaguzi nchini
humo tayari imetangaza kusajili majina ya
wagombea 25 wanaotarajiwa kugombea nafasi
ya rais, miongoni mwao akiwemo aliyewahi
kuwa msemaji wa rais wa zamani Rais Joseph
Mobutu, Tryphon Kin-Kiey Mulumba, ambaye
pia alikuwa akitetea uamuzi wa Rais Kabila
kugombea mhula wa tatu.
Katika uchaguzi huo, Jean-Pierre Bemba, Félix,
Vital Kamerhe ndio wagombea wenye nguvu
kutoka vyama vya upinzani wanaotarajiwa
kutoa upinzani kwa chama tawala
kilichomchagua Emanuel Shandary.
Wakati hali ikiwa imepamba moto, Moise
Katumbi, gavana wa zamani wa Jimbo la
Katanga anayeishi uhamishoni nchini Afrika
Kusini alikwama kurudi nyumbani kuwasilisha
fomu za kugombea urais, baada ya kuzuiwa
kuingia nchini humo na vyombo vya ulinzi na
usalama.
Katumbi aliondoka nchini humo mwezi Mei
mwaka juzi kuelekea Afrika Kusini kupata
matibabu, huku nyuma akifunguliwa mashtaka
kwa makosa ya kuwaajiri wapiganaji, kuuza
viwanja kinyume cha sheria na kupewa adhabu
ya kifungo cha miaka mitatu gerezani bila ya
kuwepo mahakamani.

DRC ni moja ya nchi maskini barani Afrika,
licha ya utajiri wake wa rasilimali haijawahi
kushuhudia mchakato wa
kubadilishana madaraka kwa njia ya amani
tangu kupata uhuru wake kutoka mikononi kwa
Wabelgiji Juni 30, 1960.
Kutokana na historia hiyo, tayari Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) limetoa
wito kwa mamlaka zinazotarajiwa kusimamia
uchaguzi huo kuhakikisha uchaguzi unakuwa
huru na wa haki kwa pande zote ili kuepusha
vitendo vinavyoweza kuliingiza taifa hilo katika
machafuko.
Hata hivyo Emerie Damien Kalwira, Rais wa
muungano wa asasi zinazopigania serikali
ya mpito nchini humo amesema mazingira ya
sasa hayatoi nafasi kwa uchaguzi huru na wa
haki nchini humo, na kusisitiza haja ya jumuiya
ya kimataifa kishinikiza kuundwa kwa serikali ya
mpito.
Rais Kabila anayemaliza muda wake
ameiongoza nchi hiyo tangu Januari
mwaka 2001, aliingia madaraka siku kumi
baada ya kuuawa kwa baba yake, Rais Laurent
Desire Kabila, alichaguliwa katika chaguzi za
mwaka 2006 na 2011.
Tangu aingie madarakani, amekuwa akikabiliwa
na vita mashariki mwa nchi yake na vikosi vya
waasi wa ndani vinavyoungwa mkono na
mataifa jirani ya Uganda na Rwanda.

Rais Kabila alizaliwa Juni 4, 1971 katika Kijiji
cha Hewabora, eneo la Fizi, Mkoa wa Kivu ya
Kusini, mashariki mwa DRC.

Mwisho