*Washindwa kuzihesabu kutokana na wingi, wapima kwa kutumia mizani
*TRA yakata kodi kiduchu kwa mwezi bila kujali wacheza kamari wameshinda kiasi gani
Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wachina wanaomiliki mashine za kamari (slot machine) maarufu kama ‘dubwi’ au ‘bonanza’ wanakusanya kiasi kikubwa cha fedha lakini wanalipa kiasi kidogo cha kodi cha Sh 100,000 tu kila mwezi.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umegundua kuwa kutokana na kukusanya kiasi kikubwa cha fedha kikiwa katika sarafu za thamani ya Sh 200 kila siku, hasa maeneo ya Dar es Salaam, sasa Wachina hao wanatumia mizani kuzihesabu kisha wanazibeba kwa kutumia ndoo zenye ujazo wa lita 20.
Pia uchunguzi uliofanywa kwa muda mrefu katika maeneo mbalimbali umegundua kwamba kupitia mashine hizo, mchezaji anaweza kushinda zaidi ya Sh 500,000 kwa mchezo mmoja, lakini kiasi hicho hakikatwi kodi, tofauti kama zilivyo kamari nyingine.
Kupitia uchunguzi huo, imebainika wamiliki wa baa zinazochezwa kamari hizo wanalipwa kamisheni kubwa na Wachina hao kila baada ya siku mbili inayoweza kufikia kati ya Sh 800,000 hadi Sh 900,000 kutegemeana na mzunguko wa wachezaji.
Wamiliki hao wa baa wanalipwa kamisheni ya asilimia 15 katika kila mfuko/trei moja linalobeba sarafu za Sh 200 zenye thamani ya jumla ya Sh 60,000.
“Ukijumlisha kwa mwezi mzima unaweza kupata kamisheni ya kati ya Sh 500,000 hadi Sh 900,000 kutokana na watakavyocheza zaidi.
“Watu wakicheza sana ndipo mimi napata kamisheni kubwa. Hapa kwangu nina mashine mbili, watu tofauti wanaweza kushinda hadi Sh 300,000, Sh 400,000 hadi Sh 600,000.
“Wachina wakija kufungua hizi mashine katika kila Sh 60,000 mimi wananipa Sh 9,000.
Kwa sababu kwangu watu wanacheza sana, kwa hiyo wanakuja kila baada ya siku mbili,” anasema mmiliki mmoja wa baa iliyopo Kinondoni (hakutaka jina lake liandikwe gazetini) alipozungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mmiliki mwingine wa baa aliyepo Mikocheni (naye hakutaka jina lake liandikwe gazetini), amesema kutokana na sarafu za Sh 200 kuwa nyingi, Wachina hao wameamua kwenda na kuzihesabu kwa kutumia mizani.
“Hapa kwangu watu wanacheza sana na maeneo mengine pia wanacheza zaidi. Zamani Wachina wakija wanafungua mashine zao wanachukua zile sarafu za Sh 200 kisha wanaanza kuzihesabu hadi itimie Sh 60,000 kisha wanazipanga kwenye trei zao maalumu ambazo ni ndogo au mifuko ya nailoni.
“Lakini wakaona kitendo hicho kinawapotezea muda, kwa hiyo sasa wanakuja na mizani kabisa wanazipima zile sarafu na zikifikia uzito fulani ujue hiyo ni Sh 60,000. Sarafu zinakuwa nyingi, maana siku wakitoa hapa kwangu pamoja na maeneo mengine wanajaza ile ndoo ya lita 20,” amesema alipozungumza na JAMHURI hivi karibuni.
Naye mchezaji mmoja wa kamari hizo, Gerald Sudi, ameiambia JAMHURI wiki iliyopita jinsi anavyoshinda na kushindwa mchezo huo.
“Siku nyota yangu ikiwa nzuri naweza kushinda hata Sh milioni moja, lakini siku nyingine pia madubwi yananikanda (yananila) na ninachokifanya ni kuhama hama kila baa ambako michezo hiyo inachezwa. Kwa siku naweza nikahama hadi sehemu mbili.
“Naangalia wapi wamecheza sana, kwa hiyo najua mashine zinakuwa na fedha, ndipo hapo ninacheza. Kuna siku nilishinda nikawa naidai mashine, kwa sababu nilikula kiasi kikubwa cha fedha lakini mle ndani hakuna, ikabidi nisubiri hadi kesho Wachina waje kuweka fedha ndipo zangu zitoke,” amesema.
Mchezaji mwingine, Kichua Fundi, ameiambia JAMHURI hivi karibuni jinsi anavyocheza na kushinda michezo hiyo.
“Ndiyo, kwa muda mrefu sasa nacheza hiyo michezo. Si mimi tu hata watu wengine wanashinda na kupata fedha. Kwa mfano kuna mwenzangu mmoja juzi tu hapa kalibutua (kashinda) hilo dubwi akapata Sh 400,000 pia tunashinda zaidi ya hizo ila siku nyingine Mchina anakuotea anakubutua,” amesema na kuongeza:
“Katika ule mchezo kuna mzunguko wa picha za wanyama kila ukitumbukiza Sh 200. Kwa mfano kwenye ile picha ya tembo zinaingia sarafu 25 za Sh 200. Kwa hiyo hapo unapata Sh 5,000 na unaweza kum-dabo (kumzidisha) na ukashangaa anajiongeza mwenyewe hadi mara 100 na hapo utashinda Sh 500,000.
“Katika ule mzunguko wa ule mchezo kuna picha za wanyama wanane wakubwa na wadogo na kila moja ina thamani yake. Kuna tembo, ng’ombe, simba, nyani, dubwi na twiga huku tembo kuna mwenye thamani ya kati ya Sh 25, Sh 50 na Sh 100 na twiga ni Sh 5.
“Ushindi unategemea na bahati yako siku hiyo, tembo ndiye mwenye thamani kubwa, kwa mfano ukiweka sarafu yako ya Sh 200 kwa tembo kisha akakubali na ukamdabo, maana yake unapata fedha nyingi zaidi.”
TRA yatoa ufafanuzi
Akizungumza na JAMHURI wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, amesema kila mwezi wanakusanya kodi ya Sh 100,000 kwa kila mashine.
“Zamani zilikuwa zinaitwa mabonanza, kodi yake tunayoikata ni fixed. Mashine hizo zinasajiliwa na kulipiwa kodi hiyo kila mwezi, haijalishi mshindi kashinda kiasi gani cha fedha kwa sababu zina kikomo cha ushindi.
“Sisi tunasimamia tu ukusanyaji wa kodi. Hata mshindi apate kiasi gani cha fedha hakatwi, lakini anayelipa ni yule mwenye hiyo mashine ambayo ni Sh 100,000 kwa mwezi,” amesema.
Pia amesema hilo ni suala la kisera na inawezekana baadaye ikabadilishwa, kwa sababu awali walikusanya kodi ya Sh 30,000 kila mwezi hadi ilipopandishwa mwaka huu.
“Mwanzo kodi ilikatwa kidogo ndipo ikapandishwa hadi Sh 100,000. Kuna kitu kinaitwa winning tax. Anayeshinda hakuna anachokatwa chochote. Wenzetu nje ya nchi hii michezo si sehemu ya kujipatia kipato bali ni sehemu ya michezo tu ya kujifurahisha na ndiyo maana ikaitwa michezo ya kubahatisha.
“Ile michezo mingine wanakatwa wote kwa maana anayechezesha na anayeshinda hasa ile ya online ina kiwango kabisa cha kodi. Kwa mfano ukisikia mtu kashinda milioni 10, maana yake hapati kiasi hicho chote bali kuna kodi atakatwa na kwa mwezi tunakusanya karibu Sh bilioni 15 kupitia michezo hiyo.
Katika hatua nyingine, amesema TRA ina jukumu la kusimamia mapato yote yanayotokana na michezo ya kubahatisha.
“Mshindi wa michezo ya kubahatisha analipa kodi kwa utaratibu wa zuio, hivyo wote wenye leseni na wanaofanya biashara ya bahati nasibu wana jukumu la kuwakata washindi na kuwasilisha ritani na malipo TRA si zaidi ya tarehe 7 ya kila mwezi unaofuata.
“Bodi ya Michezo ya Kubahatisha ina njia mahususi ya mawasiliano na udhibiti inayosimamia mifumo wanayoitumia wafanyabiashara wenye leseni ya michezo hii,” amesema.
Vilevile amesema TRA inatumia mifumo hiyo kupokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wadau na kufanya ukaguzi kubaini endapo kama kuna ukwepaji wa mapato kutoka kwa wafanyabiashara wenyewe au mapato ya washindi ambayo ni jukumu la wafanyabiashara kulipa kwa niaba ya washindi.
Kodi michezo ya kubahatisha
Kwa mujibu wa TRA kila mchezo wa kubahatisha una kiwango chake cha makato ya kodi tofauti na kile wanachokatwa washindi, ikiwa pia ni tofauti na zile za mashine ya dubwi.
Mchezo wa kasino kiwango kinachotumika kukatwa ni asilimia 18 ya mapato yote baada ya gharama huku kasino ya mtandaoni kiwango kinachotumika kukatwa ni asilimia 25 ya mapato yote baada ya gharama.
Kwa washindi wa kasino kiwango kinachotumika kukatwa ni kati ya asilimia 12 hadi 15 ya thamani ya ushindi.
Kwa upande wa kodi kwa kampuni wanalipa asilimia 25 ya mapato ghafi kwa michezo ya kubahatisha, huku michezo ya simu (sms) wanalipa asilimia 25 ya mapato ghafi na bahati nasibu ya taifa wanalipa asilimia 20 ya mapato ghafi.
Pia mashine (forty machines sites) wanalipa asilimia 25 na michezo ya kompyuta wanalipa asilimia 10, huku michezo mingine chini ya kifungu cha 51 wanalipa asilimia 10.
Mashine za dubwi zakamatwa
Wakati huohuo, msako mkali umefanyika katika kata tano za Wilaya ya Kinondoni na kufanikisha kukamatwa kwa mashine 72 za dubwi zinazoendeshwa kinyume cha sheria.
Kupitia msako huo uliofanywa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, mashine zilizokamatwa ni zile zisizo rasmi, hazilipi kodi na hazitambuliwi na Bodi ya Michezo ya Bahati Nasibu (GBT).
Pamoja na ukamataji huo, pia amepiga marufuku na kuahidi kuwakamata wote wanaochezesha kamari hiyo kwa watoto kwa masilahi yao binafsi.
“Wanaochezesha mashine hizi zisizo rasmi, waziondoshe mara moja. Tumeanza katika kata tano na tutaendelea katika wilaya yote ya Kinondoni, kwa sababu tunafahamu michezo hiyo isiposimamiwa vizuri ikaendelea kuenea katika maeneo yetu itahamasisha uhalifu.
“Itahamasisha baadhi ya watu kuamini kwamba wanaweza kupata fedha wakawa na maisha mazuri kwa kupitia michezo hii ya bahati nasibu, hasa isiyo rasmi,” amesema.
Mbali na kutosajiliwa na kutolipa kodi, mashine hizo zimewekwa katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria.
“Tumezikuta hadi kwenye maeneo ya makazi, lakini tuliona hadi watoto wadogo wakicheza kamari ya dubwi hadi saa nne usiku. Miongoni mwa watoto waliobainika kucheza kamari hiyo wamo wenye umri wa kwenda shule, baada ya kuzikamata tumezikabidhi GBT,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa GBT, James Mbalwe, ameyataja maeneo yasiyotakiwa kuwapo michezo hiyo kuwa ni eneo lililo karibu na nyumba za ibada, majengo ya shule, hospitali na makazi ya watu.