*Watoto wengine wa vigogo wajazwa Idara ya Afya

*Washika nafasi zote za Jiji, Ilala, Temeke, K’ndoni

Siku chache baada ya kuibuka mjadala wa kuwapo watoto wengi wa vigogo ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hali kama hiyo imejitokeza tena kwenye Idara ya Afya katika Jiji la Dar es Salaam na manispaa zake tatu za Temeke, Ilala na Kinondoni, JAMHURI imebaini.

Baadhi ya wafanyakazi wa Idara hiyo, wametoa waraka wakihoji namna watoto hao wa vigogo walivyoweza kushika nyadhifa kubwa katika manispaa hizo, ilhali watumishi wengine wenye sifa, ama wakiachwa au wakipelekwa mbali na Jiji la Dar es Salaam.

 

Katika waraka huo, ambao JAMHURI imepata nakala yake, wanatajwa baadhi ya watoto wa vigogo na nyadhifa zao kuwa ni Janeth George Kahama, ambaye ni Mganga Mkuu wa Jiji. Huyu anatoka katika familia ya Mzee George Kahama, mmoja wa mawaziri wawili walio hai wa kwanza katika Baraza la Kwanza la Mawaziri la Tanganyika huru. Mwingine aliye hai ni Job Lusinde.


Waraka huo pia unasema nafasi ya Mganga Mkuu Msaidizi wa Jiji la Dar es Salaam inashikwa na Dk. Hawa Rashidi Kawawa. Huyu ni mtoto wa Mzee Rashidi Mfaume Kawawa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Tanganyika, Waziri Mkuu wa Tanzania, na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).


“Hivi ni kweli watoto hawa wa wakubwa ndiyo wenye sifa tu za kushika nyadhifa hizi? Kweli, wanaweza kuwa na sifa, lakini iweje wasipelekwe Tandahimba, Kibondo au Karagwe? Kwanini Dar es Salaam tu?” Wamehoji waandishi wa waraka huo.


Wameendelea kusema kuwa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni ni Dk. Gunini Kate Kamba.  Huyu ni mtoto wa Kamba aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza na ndani ya CCM. Wadhifa wa karibuni kabisa aliokuwa nao ni wa ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki.


Kwa upande wa Manispaa ya Ilala, Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo ni Dk. Asha Omar Mahita. Dk. Asha ni mtoto wa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu Omar Mahita.


Mtoto mwingine wa kigogo ni Dk. Amani Kighoma Malima ambaye ni Mganga Mfadhiwi wa Hospitali ya Temeke. Huyu ni ndugu yake na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima.


Dk. Amani ni mtoto wa marehemu Kighoma Malima, ambaye alishika nyadhifa mbalimbali serikalini. Mara ya mwisho kabla ya kufikwa na mauti alikuwa Waziri wa Fedha.

 

Aidha, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Dk. Sylvia Mamkwe, ingawa si mmoja wa watoto wa vigogo, lakini alikuwa na uhusiano wa karibu mno wa kikazi na aliyekuwa Mganga Watoto wengine wa vigogo wajazwa Idara ya Afya

Washika nafasi zote za Jiji, Ilala, Temeke, K’ndoni

Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa; aliyeondolewa kwenye nafasi hiyo mwaka huu kutokana na shinikizo la madaktari waliogoma.


“Haya ni majina ya baadhi tu ya watoto wa vigogo katika Idara ya Afya katika Jiji la Dar es Salaam na Manispaa zake. Tunauliza, iweje watoto wa wakubwa tu ndiyo washike nyadhifa hizi kwa Dar es Salaam na si mikoani?” Umehoji waraka huo.


Wiki iliyopita, JAMHURI iliandika taarifa ya kuwapo watoto wengi wa vigogo ndani ya BoT. Hadi sasa, majina yanayovuma ya watoto hao ni ya Pamela Edward Lowassa, Filbert Tluway Sumaye, Zaria Rashidi Kawawa, Harriet Matern Lumbanga, Salama Ali Hassan Mwinyi, Rachel Muganda, Salma Omar Mahita, Justina Joseph Mungai, Kenneth Nchimbi, Blasia William Mkapa, Violet Philemon Luhanjo, Liku Kate Kamba, Thomas Mongella na Jabir Abdallah Kigoda.


Kuwapo kwa watoto wa wakubwa katika sehemu nyeti na nzuri kumeanza kuzua minong’ono ya upendeleo miongoni mwa wananchi.


Mmoja wa wananchi amehoji hali hiyo kwa kusema, “Ninachojiuliza na sipati majibu mpaka sasa ni hiki, kama imetokea coincidence (bila kutarajia) BoT ikaajiri watoto 14 wa vigogo; je, coincidence hiyo hiyo inaweza kutokea kwenye Wizara ya Elimu watoto wenye majina kama hayo hayo wakapangwa kwenda kufundisha shule za kata vijijini, ambako hakuna maji wala umeme na wakaendelea kuifanya kazi hiyo kwa moyo wa kizalendo bila kujali kuwa mishahara imechelewa na hawajapandishwa vyeo; na wakati huo huo wakiidai serikali sikivu malikimbizo?


“Hivi kweli binadamu wote ni sawa kwa maana ya fursa za ajira bila kuangaliana usoni, hasa BoT?”