Kesi ya kughushi kibali cha madini ya U.S.D Mil 8 inayomkabili mfanyabiashara, Ndama Shabani Hussein maarufu ‘Ndama mtoto ya Ng’ombe’ kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo upelelezi wake unasubiriwa kutoka nchini Australia.
Hayo yameelezwa na wakili wa serikali, Elia Athanas mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Athanas ameeleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika kwa sababu kuna taratibu baina ya nchi mbili Tanzania na Australia zinaendelea ili kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo, hivyo anaomba iahirishwe hadi tarehe nyingine ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Hata hivyo, wakili wa utetezi Nashon Nkungu amedai kuwa wanasikitika kwa kuwa upande wa mashtaka hawalipi uzito suala hilo na kwamba upelelezi huo umekuwa haukamiliki tangu 2017 kesi ilipofunguliwa.
Pia Nkungu ameiomba mahakama kuuonya upande wa mashtaka kutekeleza jukumu lake katika kesi hiyo, na ukiona umeshindwa kukamilisha upelelezi huu ambao haufikii kikomo, ufanye kama sheria inavyotaka uiondoe hati ya mashtaka.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Kasonde amesema hakuna ubishi suala la upelelezi linahusisha nchi mbili, hivyo anatoa nafasi kwa upande wa mashtaka ambapo anaahirisha kesi hiyo hadi September 21, 2018.
Katika kesi hiyo, Ndama anakabiliwa na mashtaka 5 ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Miongoni mwa mashtaka yanayoendelea kumkabili Ndama ni pamoja na kudaiwa February 20, 2014 Dar es Salaam kugushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboxi 4 ya dhahabu yenye kilogramu 207 yenye thamani ya U.S.D 8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.
Pia anadaiwa March 6, 2014, Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonesha kilogramu 207 za dhahabu kutoka nchini Congo zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.