Serikali inaendelea kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ufanisi katika kuhudumia shehena kubwa zaidi. Katika maboresho hayo magati 1-7 yanafanyiwa ukarabati pamoja na ujenzi wa gati jipya litakalohudumia meli zenye shehena ya magari.
Maboresho hayo ambayo yako chini ya mradi wa Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP), yana umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu na nchi zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe, amesema serikali imeamua kufanya maboresho hayo ili kuongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam, ambayo kwa sasa ina uwezo wa kuhudumia hadi tani milioni 18 za shehena kwa mwaka.
“Watanzania wanataka kazi nzuri, wamechoka kusikiliza maneno mazuri, lengo la serikali kufanya maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam ni kuhakikisha tunaondoa vikwazo na kuwavutia wawekezaji wa ndani na nchi jirani waje kutumia bandari yetu,” amesema Kamwelwe.
Bandari ya Dar es Salaam ina gati 12 za kuhudumia shehena za aina mbalimbali za mizigo, ikiwa ni pamoja na shehena ya mizigo mchanganyiko, makasha na mafuta.
Lengo la maboresho hayo ni kuijengea uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam ili iweze kuhudumia meli kubwa zaidi zenye uwezo wa kubeba makasha kutoka 2,500 hadi 4,000 TEUs za sasa hadi kufikia 6,000 mpaka 8,000 TEUs, yaani meli za ukubwa wa Post Panamax na zile za urefu wa wastani wa mita 320 kutoka wastani wa mita 243 za sasa.
“Upakuaji wa meli unahitaji vyombo, yale makreni ya kushusha mizigo yanatakiwa kuletwa haraka, tunataka kuwepo na ufanisi wa kupakua mizigo katika bandari yetu.
“Ndugu zangu, mimi kazi yangu ni kujitahidi kuondoa vikwazo vyote, ndiyo maana kodi kama delivery fee imetolewa, striping fee na escort fee zote zimeondolewa…kontena moja lilikuwa linatozwa dola za Marekani 70 (sawa na Sh 159,000) hadi dola za Marekani 150 (sawa na Sh 340,000), kodi ambayo haikuwa inaingia serikalini,” amesema Kamwelwe.
Mhandisi Kamwelwe amesema ukarabati wa Bandari ya Dar es Salaam unakwenda sambamba na ukarabati wa bandari nyingine za Tanga, Mtwara na Kigoma. Amesema ujenzi wa miundombinu mingine unajumuisha ukarabati wa viwanja vya ndege pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi huo unalenga kuzihudumia nchi za Rwanda, Uganda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa gati maalumu ya magari (Ro-Ro Berth), upanuzi na uimarishaji wa gati namba 1 hadi namba 7 kwa kuongeza kina kutoka mita 10 za sasa hadi mita 14.5, uchimbaji na upanuzi wa mlango wa kuingilia na kutokea meli (entrance channel) pamoja na eneo la kugeuzia meli (turning basin).
Mradi utahusu pia kuchimba zaidi kina cha mlango wa bahari kutoka wastani wa sasa wa mita 10.2 hadi mita 15.5 na kupanua upana wa lango kutoka mita 140 hadi mita 170.
Mradi huu utakapokamilika utaongeza uwezo wa bandari wa kuhudumia shehena kutoka tani milioni 14 za sasa hadi tani milioni 28 kwa mwaka, badala ya tani milioni 18 ambazo zingekuwa kikomo cha bandari ya sasa kama isipoendelezwa zaidi.
Huduma zinazotolewa na Bandari ya Dar es Salaam ni pamoja na kuongoza meli katika kuingia na kutoka bandarini, kuziegesha, kupakia na kupakua shehena za mizigo na kuitunza mpaka mwenye mzigo anapokuja kuchukua.