Habari Mhariri,

 

Mimi ni mkazi wa Pugu, mmoja ya wapenzi wakubwa wa gazeti la Jamhuri linaloanzia wengine wanapoishia, naamini ni kwenye uwezo ndio maana sahihi ya kauli hii (uwezo wenu ni zaidi ya wale).

Napenda kuwasilisha kilio changu, na cha wengi  juu ya mradi wa utanuzi wa uwanja wa ndege Julius Nyerere ulivyotusababishia matatizo, hasara, ugomvi kati ya majirani/wakazi wa huku, huku viongozi wetu wakibakia kupokea taarifa za makaratasi bila kufika ‘field’, na haya yamekuwa mazoea ya viongozi wengi kutokuchukulia mambo kwa uzito stahiki, na ndio yanayochangia nchi kutokwenda mbele.

 Mradi huu hatukatai ni mradi muhimu sana kwa taifa hili ukizingatia uwanja tajwa ndio uwanja maarufu Tanzania, ivyo kutanuliwa ilikua ni muhimu sana, tena sana kwa ajili ya taifa letu, lakini Maendeleo hayo nasikitika kusema yamekua furaha inayokwenda sambamba na machungu.

Furaha kubwa ya mradi kwa wakazi wote: Kipawa, Kigilagila na Wenyeji wa Pugu ni ardhi kupimwa; hii ni faida kubwa sana iliyotokana na mradi huu watu wa kipato cha chini wasingeweza kupima ardhi zao wenyewe, lakini pia kuwasaidia wengine viwanja hivyo kukopea kwenye Taasisi za fedha kwa kutumia ‘offer’ zao walizopatiwa na serikali (sio wote tuliokwisha zipata na zoezi kama vile alipo tena).

Pia imepunguza matukio ya uhalifu kama tujuavyo uswahilini kwa waliokuwa wakazi wa Kipawa na Kigilagila ile kuwa na namba ya watu wengi kwenye eneo dogo ilichochoea matatizo mengi, lakini sasa unakuta eneo la eka moja zinakaa familia nne au tano, kwa haraka haraka ni kama watu 20 – 30 kwa eneo la eka moja.

Ni Maendeleo na Serikali inawezekana bila kujitambua inajenga ustaharabu kwa watu wake kwa kuwatoa watu kwenye maeneo yasiopimwa na yenye vurugu nyingi na kuwapeleka kwenye maeneo yaliopimwa ambayo ujenga ustaharabu wa mtu hasa malezi mazuri ya watoto. Hii inaendana na kukusanya kodi/ushuru mbalimbali kwa urahisi.

 Mradi huu una matatizo ya aina mbili; makubwa na madogo.

Matatizo mabwa katika mradi huu yaliyofumbiwa macho, na viongozi ama kutokana na kuwa wanufaika au wanaogopa kuchokonoa hivyo hawajali wananchi.

Kwenye matatizo madogo; waliokuwa wakazi wa Kipawa na Kigilagila jinsi ya kuishi imebadilika mno hasa kwenye shughuli zao za kila siku kwa wale waliozoea idadi kubwa ya watu kuwazunguka, kwa mfano mama mwenye shughuli ya kupika chapati, vitumbua, andazi na kuuza kwa kutoa beseni nje ya nyumba,  huku akiendelea na shughuli hiyo sikio moja akisikilizia wateja, kwa sasa imekuwa ngumu.

Ni lazima atembeze kwa sababu watu wametapanywa kwenye eneo kubwa hivyo si wote wanaopita tena karibu na yeye, hivyo kufanya punguzo la wateja wake. Hili limewakumba wengi, mpaka sasa wanafuta ‘watoke vipi’.

Lakini pia, huzuni nyingine ndogo kama sio kubwa ni kwa wenyeji kuchukuliwa maeneo yao makubwa na kisha kupelekwa kwa ‘tabu na kwa kubembeleza’ kwenda kupewa ‘kakiwanja’ kadogo na ni bora ukapewa viwili unapewa kamoja ambacho akifanani na ulikotolewa. Huu si uungwana hata kidogo.

Huzuni kubwa ambayo imebeba dhima ya andiko hili ni matatizo makuu tunayotaka yatatuliwe haraka iwezekanavyo na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kama mhusika mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya Ilala/Kamati ya Ulinzi na Usalama, Waziri Mkuu na ikibidi Rais ambaye ameamua kuyavalia njuga mambo yote yanayokandamiza ‘uhai’ wa wananchi, na naomba kuorodhesha matatizo hayo kama ifuatavyo:-

1.       Kuna wananchi mpaka sasa wamethaminiwa ila hawajalipwa fedha wala kupewa maeneo

2.       Kuna wananchi wamelipwa, lakini awajapewa maeneo

3.       Miundombinu

4.       Hati za viwanja

5.       Mradi wa barabara ya kutoka Mbagala mpaka Kibaha/Chalinze

6.   Kuna wananchi maeneo yao yamechukuliwa awajathaminiwa na hakuna kinachoendelea

Nasikitika wakati Bunge la bajeti likielekea ukingoni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Injinia Edwin Ngonyani alitangaza kusitisha malipo ya uthamini huku akitaja vipindi tofauti vilivyokuwa vya usitishaji wakati akieleza juu ya mradi wa utanuzi wa uwanja wa ndege JKA.

Kuna watu wapo wamethaminiwa, lakini hawajalipwa na sasa hivi wameamua kuendeleza ujenzi. Mbaya zaidi wanafanya ujenzi holela kwa sababu hawaoni wala kusikia tena uhai wa mradi, na ardhi wanayo.

Mipango miji wameshapitisha ramani, wakazi hawa hawajalipwa wameamua kuendelea na ujenzi holela, sasa kiwanja kimoja kina majengo ya watu wawili au watatu. Kweli Serikali imekusudia kutatua matatizo au kuongeza migogoro ya ardhi? Tunaiomba Serikali iingilie haraka kwani hata barabara za mitaa zimeanza kujengwa nyumba, viwanja vya shule vimevamiwa, n.k.

Tatizo la pili la wananchi kulipwa, lakini kutokupewa maeneo, hili naomba kushusha lawama kwa wasimamizi wa mradi huu wa ugawaji viwanja, wakiongozwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege waliosimamia kazi hii (shutuma zipo wazi na wananchi wakihojiwa wanaweza kueleza zaidi) baadhi ya shutuma hizo wanadaiwa kuhodhi/kujimilikisha viwanja wao au ndugu zao, huku wakiacha wanaostahili kupewa viwanja.

Wakifuatwa wanakuwa watu wa kuzungusha wananchi. Sasa hii inachangia watu kugoma kupisha wageni kwenye maeneo yao mpaka watakapoonyeshwa kiwanja alichopewa vinginevyo wanafia kwenye maeneo yao. Tunaiomba Serikali ya Awamu ya Tano kulifanyia kazi hili haraka sana.

Mradi wa barabara ya kulipia kutoka Mbagala mpaka Kibaha/Chalinze, inasikitisha kuona mradi huu unafanyika kimya kimya watu wanapita kwenye maeneo ya watu kuonyesha barabara itapita hapa mara itapita kule. Maumivu juu ya maumivu. Maeneo ya shule, maeneo ya huduma

za jamii kama posta, polisi, benki, n.k yamevamiwa.

Tumefanya jitihada za kuonana na Waziri wa Ardhi na Mkuu wa Mkoa kipindi cha nyuma ila mpaka sasa tumekwama. Tunaamini kwa mabadiliko ya sasa wakazi wa Nyeburu, Zavala, Kinyamwezi na Pugu Mwakanga tutapata suluhisho ikiwamo uthamini na upimaji kufanyika kwa wakati.