Miongoni mwa vichocheo vinavyoongeza tishio la ukame na mabadiliko ya tabia nchi linaloikumba dunia kwa muda mrefu sasa ni ukataji holela wa miti na uharibifu wa mazingira, hususan misitu.
Ongezeko la ukataji miti ni tatizo kubwa kwa dunia na hata Tanzania limekuwa likijidhihirisha waziwazi licha ya kuwapo kwa juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika nyakati tofauti.
Takwimu zinaonyesha kuwa mahitaji ya nishati, hasa ya kupikia, ndiyo husababisha kwa kiasi kikubwa uharibifu wa misitu na kwamba yapo maeneo, hasa ya Kanda ya Ziwa, ambayo tayari yamepoteza uoto wake wa asili.
Sote tunafahamu umuhimu wa misitu na faida zake katika maisha ya kila siku ya binadamu; lakini ni wazi kuwa hatujaonyesha moyo wa kushiriki katika kutunza misitu na kuhifadhi mazingira.
Jukumu la kulinda misitu limeachwa mikononi mwa Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS). Kana kwamba hilo halitoshi, wakala huo ndio pia umepewa jukumu la kupanda miti na hata kuhakikisha miti hiyo inakua na kudumu.
Hii si sahihi hata kidogo. Jukumu hili ni lazima sasa liwe la Watanzania wote, likipanua wigo na kujumuisha sekta nyingi zaidi badala ya kuliacha mikononi mwa wadau wachache kama TFS na Idara ya Misitu na Nyuki ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, anatukumbusha kuwa misitu ina mchango mkubwa katika kupatikana kwa maji; kwamba madakio (water catchment) mengi ya maji pamoja na vyanzo vya maji hupatikana misituni.
Maana yake ni kwamba, sekta ya maji inapaswa kushiriki katika ulinzi na uhifadhi wa misitu sambamba na upandaji miti. Sekta ya mifugo nayo inapaswa kushiriki katika suala hili kwa kuwa ni misitu ndiyo hutoa malisho kwa mifugo.
Na kwa hakika sekta hii ya mifugo ndiyo imechangia kwa kiwango kikubwa uharibifu wa uoto wa asili Kanda ya Ziwa, kwa maana hiyo sasa ni lazima kuwekwe sera maalumu ya kudhibiti uharibifu huo usifanyike katika maeneo mengine ya Tanzania ambako wafugaji wamehamia.
Sekta ya Nishati nayo sasa inapaswa kujipanga kwa kuleta nishati mbadala ya bei rahisi kuliko kuni na mkaa. Kuwapo kwa nishati mbadala kutaokoa uharibifu wa misitu huku pia kukitoa nafasi kwa TFS na wadau wengine kuotesha na kupanda miti zaidi bila hofu kwamba siku moja itakatwa.
Wigo huu pia unapaswa kujumuisha sekta ya elimu; si kwa kutoa elimu kwa jamii pekee, bali hasa kuwashirikisha watoto wa shule wafahamu hatari zinazokikabili kizazi kijacho iwapo miti haitapandwa na kutunzwa.
Tunaamini kwamba kila mmoja akitoa mchango wake katika nafasi aliyopo, kwa usimamizi na maelekezo ya TFS na wadau wengine wa misitu na mazingira, Tanzania ya kijani inawezekana.