Hakuna asiyefahamu kuwa kwa sasa ndani ya Klabu ya Simba ya Dar es Salaam hali si shwari, kutokana na aina ya matokeo inayoyapata timu hiyo kwa msimu minne sasa.
Simba imeshindwa kabisa kupata matokeo mazuri kutoka kwa Rais wa sasa klabu hiyo, Evans Aveva, aliyebeba mikoba ya Ismail Aden Rage.
Rage aliweza kuwachanganya Yanga katika kipindi chake na kuwafanya mashabiki wa Yanga kushindwa kuwa na raha kabisa wanaposikia maneno ya ‘kejeli’, ambayo yalikuwa yanaendana na matukio halisi.
Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Tabora Mjini, alikuwa na maneno yenye kuuma wakati Klabu ya Simba ilipokuwa inapata matokeo mazuri kila siku, tofauti kabisa na Simba hii ya waropokaji kama akina Haji Manara.
Tayari msimu huu wameshatoka ‘kapa’, maana Simba imeshindwa kubeba kombe lolote licha ya kutoa ushindani wa hali ya juu mwanzoni mwa ligi hizo.
Msimu huu ulikuwa ni tofauti kabisa na miaka iliyopita, maana klabu zetu zilikuwa zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho (FA), ambapo Wekundu hao wa Msimbazi wameambulia majonzi sehemu zote mbili.
Katika Kombe la FA, Simba ilitolewa hatua ya robo fainali baada ya kufungwa na Coastal Union mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Lakini kipindi hicho Simba inatolewa katika Kombe hilo la FA, ilikuwa katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania kama ingeendelea kuzichanga vizuri karata zake.
Ila ilishindwa kufanya kila mashabiki walichokitarajia na kujikuta ikifungwa na Toto African ya Mwanza bao 1-0, ikatoka suluhu na Azam FC, na kufungwa bao 1-0 na Mwadui FC hivyo kusababisha kupotea kabisa katika mbio hizo.
Mara ya mwisho kwa Simba kubeba Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwamsimu wa 2011/2012, hivyo kuifanya hadi kufikia leo haijagusa ubingwa huo kwa msimu minne.
Tunajua anguko la Simba ya Tanzania ni sawa na SC Villa ya Uganda, Tusker ya Kenya, ama AC Milan na Inter Milan za Italia, au hata Manchester United ya Uingereza lakini kwa ndugu zetu hawa hali imezidi.
Simba leo inashindwa kabisa kuwakosha mashabiki wao wanaokuwa wanaumia kila wanapokuwa uwanjani wakiangalia timu yao. Mashabiki hawa wanaambulia majonzi ya kufungwa kila kukicha hadi kufikia sasa hadi washindwe kwenda uwanjani kuangalia mpira wakihofia kufungwa.
Haya yote yanapatikana katika Simba ya Aveva na siyo ya enzi za Hassan Dalali na Rage, waliokuwa wanaambulia matusi kila siku mwishoni mwa uongozi wao wakishinikizwa kuachia ngazi.
Bila shaka matatizo ya Simba kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na uongozi uliopo madarakani chini ya Rais Aveva, ambaye anaonekana kabisa kushindwa kuitawala klabu hiyo.
Aveva sasa hakuna anayempenda katika Klabu ya Simba, uongozi wake umepasuka na hivi karibuni Mjumbe wa Kamati ya Usajili, Iddi Kajuna, amejiuzulu kutokana na mwenendo mbovu wa klabu.
Simba hivi sasa imekuwa ya kufungwa na kikosi cha kuungaunga cha Toto African, ambayo inashindwa kabisa hata kulipa mshahara wachezaji wake.
Simba inakubali kufungwa na Toto African Taifa, inafungwa na Coastal Union ambayo tayari imeshashuka daraja sasa, kwanini viongozi wasibebe lawama katika hili?
Hakuna anayefurahia kufungwa, hata Simba ya viongozi waliopita ilikuwa inafungwa lakini siyo kupotea kabisa katika ramani ya soka zaidi ya miaka mitatu.
Simba ni klabu kongwe na inayo historia pana ya soka hapa Tanzania na barani Afrika kwa ujumla, tangu enzi za akina Abdallah Kibadeni, ambayo iliifikisha fainali za Kombe la Shirikisho.
Uongozi wa Simba ulio chini ya Aveva umekumbwa na matatizo ya kila siku, wachezaji kudai mishahara, mchezaji kasimamishwa na makosa ambayo yapo nje kabisa na mambo ya soka. Hii kasumba imewatafuna viongozi waliokuwa wanahitaji maslahi yao binafsi ndani ya klabu na kuifikisha klabu walipoifikisha.
Sijaona nini Aveva atakachokuja kuwaeleza wanachama wa Klabu ya Simba hapo baadaye mara baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, ama atakapokuja kuomba kura ili achaguliwe tena. Hakika sioni kabisa licha kukaa pembeni na kupisha wengine.
Aveva huyu aliingia katika nafasi hiyo kwa kumuona Rage hakuna alichofanya, lakini Rage huyo huyo ndiye aliyewezesha Simba wapate fedha za Okwi na Samatta, ambazo sasa wanajinasibu wanataka kuzijengea uwanja Bunju.
Rage alikuwa mjanjamjanja ndani ya Simba lakini katika suala la kukisuka kikosi bora ambacho kitapata matokeo mazuri kwenye timu alijitahidi. Leo kushindwa kwake Aveva kuongoza klabu ya Simba kunamtakatisha Rage ambaye alionekana si lolote ndani ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Wanachama wengi wanamkumbuka Rage leo, kwanini ukiwauliza wanakwambia Simba ya Rage ilikuwa inapata matokeo licha kuwa na matatizo ya kibinadamu.
Wapenzi wengi wa Simba wanalilia klabu hiyo apewe Mohamed Dewji ambaye ni mnazi mkubwa wa timu hiyo ili iwe ya kisasa. Cha msingi ni wanachama kuangalia udhamini wa MO ni kiasi gani na wananufaika vipi hao wanachama ili Simba irudi kwenye mstari.