Dar es Salaam
NA ALEX KAZENGA
Viongozi wenye jukumu la kusimamia mchezo wa mpira wa miguu nchini wameshitakiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Wanashitakiwa kwa uzembe na kukosa uwajibikaji, hali inayotajwa kuwa kikwazo kwa ustawi wa soka.
Aliyefikisha mashitaka hayo kwa Rais ni Liston Katabazi, mdau na mwalimu wa soka ambaye kupitia barua aliyoandika kwa Rais Samia ya Oktoba 12, 2021, analitaja Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Ofisi ya Msajili wa Vyama na Vilabu vya Michezo kuwa wameshindwa kuyasimamia majukumu yao.
“Kama itafanyiwa kazi nina uhakika italeta mabadiliko kwenye sekta ya michezo, hasa mpira wa miguu,” anasema Katabazi.
Ndani ya barua hiyo, amebainisha kuwapo kwa baadhi ya viongozi wanaoendesha soka la Tanzania kwa matakwa binafsi badala ya kufuata kanuni na sheria zake.
Matokeo ya kutofuata kanuni na sheria anayahusisha na kitendo cha uongozi wa michezo Wilaya ya Ubungo na uongozi wa soka Mkoa wa Dar es Salaam kutoziheshimu taratibu na badala yake ofisi hizo zinatumia hujuma kuendesha mchezo huo.
Mbali na kuwa mwalimu mwenye elimu ya ngazi ya kati (Intermediate) ya mchezo wa mpira, Katabazi anasema ni mmiliki wa timu ya Changanyikeni FC yenye usajili Na. 11157.
Anasema mwaka jana ilihujumiwa na viongozi wa michezo wa Wilaya ya Ubungo ikashindwa kushiriki Ligi Daraja la Tatu, huku viongozi hao wakishindwa kumpa sababu za msingi za kuinyima timu yake nafasi ya kushiriki ligi hiyo.
“Kinachonishangaza ni kuzuiwa kwa timu yangu kwamba sina vigezo, wakati huo kuna timu 16 kati ya 30 zilizoruhusiwa kushiriki ligi hiyo zikiwa hazina usajili halali wa BMT, ” anasema.
Anazitaja timu zilizoshiriki ligi hiyo bila kuwa na usajili kuwa ni Talent FC ya Mbezi, Sisi kwa Sisi FC ya Manzese, Sea View Rangers, Via Sports Club na Temboni FC.
Nyingine zilizoshiriki ni Kibanda FC, Saranga Boys FC, Goba Ham FC, Mabibo Boys FC, Gold Youth FC, New Tegeta FC na Msakuzi FC.
Kitendo cha timu hizo kushiriki bila usajili anasema kimeisababishia hasara serikali kwa hushindwa kukusanya mapato yanayotokana na ada za usajili na ada za kila mwaka zilizopaswa kutolewa na timu hizo.
“Ada ya kusajili timu ni Sh 100,000 na kila mwaka timu hutakiwa kutoa ada ya Sh 50,000. Baada ya kuona hujuma hiyo nilifikisha malalamiko yangu BMT, Shirikisho la Mpira wa Miguu TFF, Wizara ya Michezo hadi Taasisi ya Kupamba na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), nimewafikishia taarifa zangu, ” anasema Katabazi.
Anaongeza kuwa pamoja na kufikisha taarifa hizo kwa wahusika, hakuna hatua yoyote inayochukuliwa huku akiamini kuwa kuna hali ya kulindana kwa baadhi ya viongozi wa soka.
Wakati Katabazi akiwatupia lawama viongozi wa mchezo wa mpira Wilaya ya Ubungo na viongozi wa kitaifa, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Ubungo, Frank Mchaki, anasema Katabazi amekuwa mtu wa kuzusha vitu bila kuwa na uelewa wa kutosha wala kuujua ukweli wake.
“Huyu kijana anahangaika, hatujui anahangaishwa na kitu gani, anaposema tumeendesha ligi bila kusajili timu anao uhakika?
“Sisi tunavyo vielelezo vyote kwamba timu zote zilizoshiriki ligi zilikuwa na sifa, yeye ndiye mwenye matatizo anafikiri mambo yanaweza kuendeshwa kwa urafiki na kujuana, ” anasema Mchaki.
Anasema Katabazi ameufikisha TAKUKURU uongozi wa mpira Wilaya ya Ubungo zaidi ya mara saba ambapo uchunguzi umefanyika na kubaini kwamba tuhuma anazozusha ni za uongo.
“Cha kwanza hana timu, hiyo Changanyikeni FC ni ya mtu mmoja anaitwa Kipese, yeye alipewa jukumu la kuifundisha tu, huo umiliki kautoa wapi? ” anahoji Mchaki.
Anasema usajili wa timu ya Changanyikeni FC upo Wilaya ya Kinondoni na kwamba baada ya Katabazi kuona ligi za wilaya hiyo hazieleweki aliamua kuhamia Ubungo bila kufuata utaratibu.
Baada ya kukataliwa, anasema Katabazi alianza kuwafuata viongozi akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Ubungo akiwataka kusimamisha ligi.
“Faili la Katabazi ninalo tangu mwaka 2016, huyo alikuwa na timu inaitwa Katabazi FC haikuwa na usajili, kwa sababu ya taaluma yake alipewa timu inaitwa Azania FC nayo ikamshinda. Leo anasumbua watu kwa hoja ipi?” anahoji Mchaki.
Anasema Septemba 23, 2020, Katabazi alifikishwa Kituo cha Polisi Urafiki na kufunguliwa mashikata kwa RB Na. 50412020 kwa kusababisha vurugu katika ofisi za michezo Ubungo.
Pia, Mchaki anasema hivi karibuni wameitwa ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kwenda kusuluhishwa lakini nako Katabazi ameonyesha utovu wa nidhamu kwa hoja kwamba uamuzi unatolewa kwa upendeleo.
Mchaki anaeleza kuwa kwa sasa Katabazi amefungiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF kutojihusisha na mpira wa miguu kwa sababu ya utovu wa nidhamu.
Kwa upande wake Ofisa Michezo wa Wilaya ya Ubungo, Wikansia Mwanga, amelieleza JAMHURI kuwa Katabazi kama anahisi hatua anazochukua dhidi yao ziko sahihi aendelee nazo.
Naye, Msajili wa Baraza la Michezo la Taifa, Patrick Kipangula, hakutaka kuzitolea ufafanuzi tuhuma hizo akidai kwamba yeye si msemaji wa baraza.