11215697_1167859589910086_8793861981273459784_nKatika kijitabu chake kidogo “Tujisahihishe” alichokiandika Mei 1962, Baba wa Taifa, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwaonya viongozi na wananchi juu ya madhara ya ubinafsi kwa nchi changa kama Tanzania iliyodhamiria kuleta demokrasia na maendeleo kwa wananchi wake.

Mwalimu Nyerere ameandika katika kitabu hicho kuwa ukweli una tabia ya kujilipiza kisasi ukipuuzwa. Mwalimu anasema mtu anaweza kuamua kulipiga teke jiwe, lakini watu wenye busara watamuonya kuwa hilo siyo dongo ni jiwe. Kwa ukaidi, kibri na dharau mtu huyo akapuuza ushauri huo akaendelea na uamuzi wake akalipiga teke hilo jiwe, Mwalimu anasema mtu huyo atavunja dole ama mguu. Ukweli haupendi kupuuzwa.

Kitabu hicho kidogo chenye hazina kubwa ya busara na hekima, Mwalimu anapinga na kukosoa tabia ya ubinafsi iliyojitokeza kwa viongozi na wananchi ambayo aliiona ni hatari na adui mkubwa wa umoja, mshikamano na ustawi wa nchi.

Akifafanua Mwalimu anasema, mtu anaweza akasimama na kutoa hoja kuwa mbili na mbili ni tano, wao watakubali. Lakini “fulani” wa pili akisema sivyo, mbili na mbili nne watamwona ni mtu mbaya kabisa ambaye hastahili hata kusikilizwa. Hawa hawajali ukweli, hujali nafsi tu. Kwao, ukweli ni maono yao na matakwa yao.

Mwalimu anaonya kuwa tabia hiyo ni hatari na maradhi mabaya kwa nchi inayojenga demokrasia yenye dhamira ya kuwakomboa wananchi wake kiuchumi.

Mtazamo na hoja hiyo ya Baba wa Taifa bado hai na yenye mantiki kubwa hivi sasa katika demokrasia ya mfumo wa vyama vingi kuliko wakati ule. 

Tatizo la ubinafsi uliokubuhu unasababisha kubomoa misingi ya mshikamano na umoja wa Taifa letu, ni ugonjwa uliokumba kada zote, hususan wanasiasa. Kutokana na uchu, uroho wa madaraka wa watu hao bila aibu au woga, wamekuwa wakipita huku na kule kupandikiza mbegu za chuki, fitna miongoni mwa wananchi ili kutimiza malengo yao.

Nchi nyingi zilizotumbukia katika migogoro, vurugu na vita ya wenyewe kwa wenyewe ni kutokana na maradhi au gonjwa hilo la ubinafsi ambao umesababisha hasadi/ husuda. Upo msemo kuwa kipele huzaa jipu na mbuyu ulianza kama mchicha.

Watanzania tunapaswa kuwa makini na kukataa hadaa na propaganda za baadhi ya wanansiasa uchwara, wabinafsi wenye uchu na uroho wa madaraka.

 

 Husuda ni maradhi makubwa

Husuda ni neno fupi lenye herufi sita, lakini lina madhara makubwa kwa nchi iliyotumbukia au kukumbwa na ugonjwa huo. Wanasiasa, wasomi, watumishi wa umma, wafanyabiashara, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida wenye kukumbwa na maradhi ya husuda huwa ni sumu mbaya kwa uhai, umoja na mshikamano wa nchi yoyote ile. Watu wa aina hiyo kutokana na maradhi hayo hupandikiza fitna, chuki, utengano kisha kuleta vurugu na hata vita ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi zao.

Mfalme mmoja wa Baghdad, inawezekana akawa Mfalme Harun Rashidi enzi hizo za kuchipuka ustaarabu, alijiwa na wazee waadilifu kumshauri. Wazee wale walimjulisha mfalme yule juu ya kuenea kwa husuda katika nchi ile wakati ule, mfalme yule aliwauliza husuda inashinda uchawi? Wakamwambia tena si kwa mara moja, lakini hata mara kumi, wakasisitiza. Husuda ni mbaya sana, ni zaidi ya ubinafsi na roho mbaya iliyokubuhu. Wakamshauri atafute watu wawili maskini sana na kuwaahidi kuwafadhili waondokane na shida zao.

Walipoletwa watu wale wawili mbele ya mfalme awafadhili waondokane na umaskini wao, mfalme akawaambia masharti ya msaada wake. Mmoja wao akatamka aina ya msaada anaoomba apewe, atakachotamka chochote kile kama vile fedha, nyumba, mashamba n.k basi yeye atapata kiasi kile kile alichosema, lakini yule mwenzake atapewa mara mbili yake. 

Yule aliyepewa fursa ya kutamka hitajio aliingiwa na husuda, badala ya kuomba fedha yeye alimwomba mfalme amng’oe jicho moja ili yule mwenzake ang’olewe yote mawili awe kipofu kabisa. Hiyo ndio husuda ilivyo, ni ubinafsi na roho mbaya iliyopitiliza.

Afrika, hususan Tanzania maradhi ya hasadi yametapakaa na kuwa tishio la ustawi na uhai wa nchi yetu- ni ubinafsi na chuki iliyopitiliza- ni ugonjwa hatari kwa umoja, mshikamano na ustawi wa nchi. Ugonjwa huu usipoangaliwa kwa makini madhara yake yanaweza yakawa makubwa hasa katika kipindi hiki cha awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, aliyedhamiria kuikomboa nchi yetu kiuchumi kwa kuendesha mapambano dhidi ya wala rushwa, mafisadi na wahujumu uchumi.

Wanasiasa uchwara hivi sasa kazi yao kubwa imekuwa kupandikiza mbegu za fitna, chuki na husuda miongoni mwa wananchi ili kuleta vurugu, uhasama na hata vita. Watu hao hawajali wala hawana mapenzi ya nchi yao, watu hao ni mabingwa wa kukejeli, kudharau, kubeza na kudhalilisha kila kitu na kudai hakuna jema, yote ni mabaya.

Kutokana na ubinafsi uliokubuhu, kila kitu kilichofanywa, kinachofanywa na Watanzania na viongozi wao waadilifu hukebehi na kudhalilisha. Imefikia hata hatua ya aina ya watu hao hudai waonyeshwe hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar baada ya kufikia zaidi ya umri wa miaka 50! Mtu mwenye akili timamu kweli anaweza kutaka kupima uhalali wa kuwapo kwake, kuwataka wazazi wake wamuonyeshe hati ya ndoa yao baada ya kutimiza miaka 50 ili kuthibitisha kama kweli amezaliwa na wazazi hao. Hiki ni kielelezo cha husuda/ubinafsi uliokubuhu humfanya mtu kukosa busara na utu.

Roho mbaya imechangia Taifa letu kudumaa kimaendeleo kutokana na ubinafsi wa baadhi ya viongozi wetu wakiwamo wanasiasa, wafanyabiashara, watumishi wa umma, wasomi na wananchi wa kawaida.

Watanzania hao wamekuwa na roho mbaya kuwachukia wenzao na kudiriki kuwanyima fursa ya kuchangia maendeleo ya nchi yao, mifano michache ni kampuni binafsi zilizoanzishwa na wazalendo kupigwa vita. 

Mfano; kampuni ya kutengeneza vifaa vya umeme ya Sahara iliyopo Arusha, kampuni hiyo ya mwekezaji inayomilikiwa na Mtanzania imeonesha uwezo mkubwa wa kutengeneza vifaa vya umeme zikiwamo transfoma za kiwango cha kimataifa, lakini haikupewa ushirikiano wa kutosha na kampuni zetu kama Tanesco. 

Tumeua kiwanda cha General Tyre, lakini tunanunua matairi ya YANA kutoka Kenya kwa fedha nyingi. Tumeua viwanda vyetu vingi kama kile cha betri za gari YUASA, kiwanda cha mashine TOOL, Mang’ula n.k kutokana na ubifasi na roho mbaya.

Kiongozi wetu Rais Dk. Magufuli ameonesha kuchukizwa na tabia hiyo na kuanza kuchukua hatua kurekebisha, sasa wanatokea wanasiasa uchwara wanaponda na kubeza jitihada kubwa zinazofanywa na uongozi wa awamu ya tano badala ya kupongeza na kumtia nguvu kiongozi wetu.

Katika kipindi kifupi cha takriban miezi minane ya uongozi wake, Dk. Magufuli amechukua hatua nyingi na ngumu kupambana na vitendo vya ubadhirifu, rushwa na ufisadi. Ameokoa mabilioni ya fedha za umma.

Kitendo hicho kimewaudhi na kuwaumbua mafisadi na mawakala wao ambao miongoni mwao ndio hao wanasiasa uchwara wanaopotosha ukweli na kuendesha propaganda chafu dhidi ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Wanasiasa hao hawalitakii mema Taifa letu na hawana huruma na Watanzania.

Tuchukue tahadhari ya watu aina hiyo, wenye uroho wa fedha na madaraka. Wanataka kuwaaminisha wananchi kuwa maandamano na vurugu ndiyo demokrasia na ukombozi wa umaskini wetu. Watu hao wanapaswa kuogopwa kama ukoma. Ni hatari kwa ustawi wa maendeleo ya nchi yetu.

Watanzania tuchukue tahadhali kwa kukataa hadaa hizo. Waswahili wana msemo: “Kama hujui kufa, chungulia kaburi.” Tunashuhudia vurugu, vita ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi mbalimbali duniani na madhara yake. Chanzo kikubwa ni wanasiasa uchwara, vibaraka wenye uchu na uroho wa madaraka na mali.

 

Kanali mstaafu Dk. Harun Ramadhan Kondo, Mhariri/mtafiti/mchambuzi masuala ya habari na jamii. Ni mjumbe wa NEC ya CCM.

Ana Master of Art katika Uandishi wa Habari aliyochukua University of Wales; na PhD Mass Communication aliyoipata nchini India.

Post Graduate Dip. Political economy- SOFIA, Bulgaria; Diploma Uandishi wa Habari- Nyegezi Siocial Tr. Centre (sasa St. Augustine University) Mwnza. Amekuwa mwandishi wa habari katika magazeti na majarida mbalimbali nchini kwa miaka zaidi ya 25. Ameandika habari na makala mbalimbali za siasa/uchumi/jamii katika magazeti ya Uhuru, Mzalendo, Daily News, Rai, Mtanzania n.k.

Amekuwa Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano na Msemaji wa JWTZ. Amekuwa Mhariri Mkuu wa majarida ya Jeshi (JWTZ) ‘Ulinzi’ na ‘Vijana Leo’