Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) baada ya kufanya uchaguzi wake na kuwapata viongozi wapya, sasa limeelekeza umakini wake kwenye utekelezaji wa vipaumbele vyake vitakavyo saidia kukuza na kuyainua mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali .

Mwenyekiti wa Baraza hilo Jasper Makala ameeleza hayo leo June 27,2024 Jijini Dodoma kwenye mkutano wake na waandishi wa habari na kueleza kuwa lengo ni kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika hayo .

Hatua hii imekuja baada ya Baraza hilo kuzinduliwa Juni 26,2024 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,Dkt.Dorothy Gwajima.

Amevitaja vipaumbele vya Baraza hilo katika kipindi cha kutekeleza majukumu yao kwa mwaka 2024 hadi ifikapo mwaka 2027 kuwa ni pamoja na kurekebisha mapungufu yote ya Baraza lilopita kwa kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ikiwa ni pamoja na kujipanga kusaidia mashirika yasiyokuwa ya kiserikali katika nyaja mbalimbali .

Vingine ni kuhakikisha mashirika yanajiendesha kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi,kuimarisha mashirikiano kati ya serikali na mashirika yasiyokuwa yakiserikali,kuimarisha Ushiriki wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali katika kuchangia katika Dira za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Africa (SADC) Jumuiya ya Umoja wa Africa (AU) na Malengo endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa (UN).

“Vipaumbele vyetu vingine ni kupashana taarifa mbali mbali zitakazo chagiza uwepo wa fursa na kuongeza ujuzi na weledi wa mashirika na umma kiujumla ambapo kama mnavofahamu, kama taifa kuna mikakati na mipango ambayo tunajiwekea kama nchi, na kushirikiana katika kuleta maendeleo ya Taifa,”amesema.

Mbali na hayo amesema kuwa wao kama Baraza wamejipanga kuongeza juhudi katika kutekeleza mipango ya Taifa kama Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, mikakati mbali mbali katika kuwa na Tanzania Bora kwa watanzania wote.