Wiki iliyopita tulichapisha sehemu ya pili ya Ripoti ya Rushwa ya Jaji Warioba. Pamoja na mambo mengine, iligusia ukaribu wa viongozi kwa wafanyabiashara nchini ulivyochochea ukuaji wa rushwa nchini. Leo tunakuletea sehemu ya tatu. Endelea…
(iii) Ukosefu wa uwazi (Transparency) katika utendaji
Miaka ya hivi karibuni taifa limeshuhudia kutoweka kwa uwazi katika uendeshaji wa shughuli za umma katika ngazi zote. Uwezo wa kuamua (discretionary powers) umetumika katika mazingira yanayotoa mianya ya upendeleo na ubaguzi kwa kutumia misingi isiyo wazi.
Misingi na vigezo vya maamuzi imekuwa haijulikani. Hali hii imezaa mianya mikubwa ya rushwa na imetumika kueneza rushwa. Mianya inayotokana na kutokuwepo uwazi imetumiwa kusamehe kodi bila kufuata taratibu zilizowekwa, utoaji wa zabuni, utoaji wa leseni na vibali mbalimbali, ugawaji wa nyumba za Serikali na za Shirika la Nyumba.
(iv) Uteuzi wa viongozi
Uteuzi wa viongozi unapaswa kuzingatia, kati ya sifa nyinginezo, uadilifu, uwezo na msimamo. Taratibu za uteuzi wa viongozi zinahitaji mtu kufanyiwa uchambuzi na kulinganisha sifa za watu waliopendekezwa ambao wameshafanyiwa upekuzi (vitted).
Hata hivyo kwenye miaka ya mwanzo ya 1990 uteuzi ulifanywa bila kuzingatia taratibu za uteuzi na kusababisha uteuzi wa viongozi wasio [na] safi jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa rushwa.
(v) Mmomonyoko wa maadili ya uongozi
Tangu kuondolewa miiko ya uongozi mwaka 1990, taifa limeshuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili ya uongozi. Viongozi wametumbukia katika shughuli za biashara ambazo wakati mwingine zimechangia katika usambaaji wa rushwa.
(vi) Kuibuka kwa mashindano ya mitindo ya maisha (Conspicuous Consumption)
Baada ya kuondoa miiko ya uongozi, yameibuka mashindano ya mitindo ya maisha kati ya viongozi. Vigezo vya maendeleo vimekuwa mali walizonazo viongozi na uwezo wa kuwasomesha watoto wao nje ya nchi.
Hali hii imechochea uongezekaji wa rushwa hasa inayohusisha wafanyabiashara waliokuwa wakihitaji misaada ya viongozi kuendeleza masilahi yao ya kibiashara.
(vii) Mabadiliko ya mfumo wa demokrasia nchini
Wakati wa mfumo wa chama kimoja cha siasa palikuwepo na mipaka dhahiri ya biashara na siasa. Baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, wafanyabiashara wamejiingiza kwenye siasa eneo ambalo hawakuwa na ujuzi nalo.
Matokeo yake ni kwamba walitumia kila mbinu na hasa fedha ili waweze kupata kura. Kwa mfano katika Uchaguzi Mkuu uliopita [Mwaka 1995] wafanyabiashara walitumia fedha nyingi kuwahonga watu ili wawapigie kura. Aidha, baadhi yao walitumia uwezo wao kifedha kuwafanyia watu binafsi kampeni za moja kwa moja badala ya kupitia kwenye vyama vyao.
MAONI YA WANANCHI
1. Hivi sasa rushwa imeshamiri katika sekta zote za uchumi, huduma na siasa katika nchi yetu. Imefikia hatua ambapo mwananchi wa kawaida analazimika kutoa rushwa ili kupata hata ile huduma ya msingi.
Sasa hivi mwananchi anaweza kukamtwa bila kosa lolote na kuwekwa rumande au kufunguliwa mashtaka makubwa na baadaye kudaiwa rushwa ili aachiliwe au kesi ya kusingiziwa ifutwe. Umma unasumbuliwa na kukerwa sana na rushwa.
Kila mwananchi anapotoa taarifa kwa viongozi na watendaji wakuu kuhusu watumishi walioko chini yao kudai ama kupokea rushwa, hakuna hatua za maana zinazochukuliwa dhidi yao kwa sababu viongozi nao au wametumbukia katika tatizo hili, tena kwa kiwango kikubwa ama wanaona ni kitu cha kawaida.
Aidha viongozi wanatoa taarifa za siri wanazozipokea kwa watu wanaotuhumiwa kwa kutaja majina ya watu waliowasilisha taarifa hizo. Matokeo ya haya ni hali iliyojitokeza ya wananchi kuamini kwamba walarushwa wanajulikana.
Wananchi wanahofu kwamba watakapotaja majina hayo, wao ndiyo watakaopata matatizo ama kwa kunyanyaswa na vyombo vya dola vikishirikisha watuhumiwa au kudhuriwa na watuhumiwa wenyewe.
Ubaya wa viongozi na watendaji wakuu kuhusika na aina hii ya rushwa, ni kwamba kunakuwa hakuna mtu wa kuchukua hatua madhubuti. Watumishi wa ngazi za chini na kati wanapoona mambo wanayofanya viongozi wao, wanaamini kwamba rushwa imehalalishwa.
Taifa limejikuta katika hali ambayo wananchi hawana imani kabisa na uongozi uliopo. Wananchi wanaamini wengi wa viongozi ama wanashiriki katika vitendo vya rushwa au wanavilea vitendo hivyo na kuvifumbia macho.
18.Wananchi wengi ambao wamejitokeza kutoa maoni yao ama kwa kukutana na Tume moja kwa moja au kwa maandishi, wana mawazo kwamba Serikali inaweza kabisa kumtokomeza adui rushwa kama viongozi wake wote watajifunga kibwebwe kwa nia na dhati kabisa ya kupambana na adui huyu.
Nia kama hiyo hapana budi itoke mioyoni mwa watu waliotosheka, wenye kulaani maovu na walio tayari kuweka matakwa yao binafsi pembeni kwa ajili ya wananchi. Aidha wanasema viongozi wa namna hiyo bado ni wachache mno, na kama kweli Serikali imedhamiria kuondoa maovu ya rushwa basi na ianze na usafishaji wa safu zake za uongozi.
19. Katika ziara za Tume huko mikoani, wananchi walisema kwamba hatua ya Rais ya kuunda Baraza la Mawaziri lenye sura nyingi mpya na ngeni katika macho ya wananchi ilipokewa kwa shangwe na watu wengi pamoja na vyama vya upinzani.
Kinachowasikitisha ni kwamba wananchi hao wamengojea karibu mwaka mmoja sasa na hakuna hatua zozote zilizokwishachukuliwa kupunguza tatizo la rushwa nchini ili kuwapunguzia wananchi hao kero.
Rais alitangaza bayana katika kampeni zake za uchaguzi kwamba atalipa kipaumbele saula hili, lakini bado viongozi wasiokuwa na aibu kwa waliyoyatenda huko nyuma, wanaendelea kushamiri katika jamii, wezi wa mali ya umma wameendelea kuheshimika na wengine kupewa nishani za kitaifa.
Wakwepaji kodi wakubwa ndio wanaenziwa na Serikali na kualikwa kwenye tafrija kubwa za kuchangisha fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Wahalifu bado wanalindwa na kuabudiwa na polisi, wahuni na matapeli wanatumia kila mbinu kuwania uongozi katika ngazi za juu, taratibu zinakiukwa kwa makusudi na tamaa kutawala; na mwananchi wa kawaida analazimika kutoa rushwa ili aweza kutibiwa, kumpeleka mtoto wake shule, kupata haki mahakamani n.k. wakati vyombo vya dola vipo, vinaona maovu haya yakitendeka lakini vinakaa kimya.
20. Wananchi walieleza kwamba Tume hii ilipoteuliwa waliipokea kwa hisia ya matumaini makubwa sana na sasa wanangojea kwa hamu kubwa matokeo yake. Wao waliamini kwamba hatua za mara moja zingekuwa zinachukuliwa kadiri Tume itakavyokuwa inawasilisha mapendekezo yake kuhusu walarushwa katika Serikali kwa sababu wengine wanajulikana.
Uamuzi wa Rais kubadilisha uongozi katika Jeshi la Polisi uliwapa matumaini makubwa, lakini sasa hawaoni hatua zinazochukuliwa dhidi ya wale wanaofahamika kupokea rushwa serikalini.
Na ndiyo maana baadhi ya wananchi wenye mashaka wanahoji uhalali wa kuteua Tume wakati watoaji na wapokeaji rushwa wanajulikana! Wananchi wengi walitegemea kwamba pamoja na kuteua Tume, Rais angeanza kuwashughulikia wale wote ambao tayari walikuwa wanatuhumiwa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa na Idara ya Usalama wa Taifa kwa kudai na kupokea rushwa.
Vivyo hivyo mawaziri aliowateua walitegemewa kuchukua jukumu la kusafisha wizara zao badala ya kungojea matokeo ya Tume. Kwa kuwa haya yote hayajafanyika. Wananchi hawana imani na viongozi wao kwa sababu ya kukithiri kwa rushwa nchini jambo ambalo linawalazimisha wananchi wanyonge kununua haki zao!
21. Hata hivyo, tegemeo la wananchi wengi ni kwamba Serikali itachukua hatua baada ya kupata taarifa ya Tume bila ya haya au upendeleo ili taifa liweze kupambana na “ADUI RUSHWA” ambaye amepotosha haki na heshima katika nchi yetu.
Hata hivyo, wametahadharisha kwamba azma hii haiwezi kufikiwa bila kusafisha safu za uongozi wa juu wa Serikali. Mashirika na hata vyama vya siasa na mashirika au taasisi zisizo za kiserikali. Uongozi usio safi hauwezi kukemea vitendo viovu vya rushwa vinavyofanywa na maofisa wa chini yao.
JITIHADA ZA KUPAMBANA NA RUSHWA
22. Rushwa kwa mara ya kwanza ilianza kuonekana kama kosa la jinai kwenye miaka ya 1930 wakati Serikali ya Mkoloni ilizifanyia marekebisho Kanuni za Adhabu (Penal Code) kwa kuweka kifungu kilichosema kudai, kushawishi, kutoa na kupokea hongo ni kosa la jinai.
Mwaka 1958 baada ya kuona kuwa Kanuni za Adhabu hazikidhi matarajio ya kupambana na rushwa, Serikali ya Mkoloni ilipitisha Sheria ya Kuzuia Rushwa, Sura Na. 400 ambayo kwa mara ya kwanza ilipanua uwanja wa makosa ya rushwa kwa kuingiza upokeaji wa zawadi na kamisheni kwenye makosa mengine.
23. Tanzania ilipojitawala ilirithi sheria hiyo pamoja na muundo wa utumishi ulioachwa na wakoloni. Kwa vile kwenye miaka ya 1960 vitendo vingi vya rushwa viliwahusu maofisa wa chini na wa kati, hasa waliokuwa wanatoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi, sheria ilitosheleza. Wakati huu maadili yaliyokuwa yakitawala utumishi wa umma na masuala ya zawadi na kamisheni hayakuwepo.
24. Kwenye mwisho wa miaka ya 1960 hali ilibadilika. Utumishi wa Umma ulipanuka sana kutokana na utaifishaji wa makampuni binafsi. Uadilifu nao ulianza kutoweka sambamba na utovu wa nidhamu. Watumishi wengi walianza kusaliti dhamana waliyokabidhiwa na taifa. Walianza kutumia nafasi zao kama kitega uchumi. Rushwa ikasambaa.
Serikali haikubaki nyuma katika kukabiliana na hali hii. Mwaka 1971 ilitunga Sheria ya Kuzuia Rushwa. Sheria hii pamoja na kuimarisha makosa yaliyoainishwa katika Sheria ya 1958, ilitamka pia kuwa ni kosa kupatikana na mali inayodhaniwa kuwa imepatikana kwa njia ya rushwa. Sheria hii pia iliongeza adhabu za makosa.
25. Pamoja na jitihada hizi za Serikali za kupambana na rushwa kwa kutumia sheria, rushwa iliendelea kushamiri kwenye miaka ya 1970, hasa kutokana na uhaba wa bidhaa muhimu. Magendo pia yalichochea ueneaji wa rushwa.
Rushwa ikaanza kulikumba pia Jeshi la Polisi. Serikali ikaona umuhimu wa kuwepo chombo maalumu cha kitalaamu cha kupambana na rushwa. Mwaka 1974 Sheria ya Kuzuia Rushwa ilifanyiwa marekebisho kumwezesha Rais kuunda Taasisi ya Kuzuia Rushwa. 1975 Rais aliunda Taasisi ya Kuzuia Rushwa yenye jukumu la kupambana na rushwa.
26. Kuwepo kwa sheria na taasisi hakukuzuia ueneaji wa rushwa nchini. Ni kweli taasisi wakati huo ikiitwa Kikosi cha Kuzuia Rushwa kilifanya kazi kwa vishindo kwenye miaka ya 1970 na kukamata watu wengi. Hata hivyo vishindo hivyo havikufua dafu.
Wimbi la rushwa liliendelea mpaka ilipofika mwanzoni mwa miaka ya 1980 ilikuwepo hatari ya kuvunjika kwa amani na utulivu (law and order). Wahalifu hasa wafanya magendo, walikuwa hawaheshimu vyombo vya dola tena. Serikali iliamua kufanya msako wa kile kilichoitwa “wahujumu uchumi” mwaka 1983. Hii pia ilikuwa ni jitihada za kupambana na rushwa. Watu wengi walikamatwa na kuzuiwa. Mali nyingi zilikamatwa.
27. Kwa nini matumizi ya sheria na kuwepo Kikosi cha Kuzuia Rushwa kulishindwa kupambana na rushwa? Tume imebaini kuwa juhudi za Serikali zililenga kwenye matukio na si kupambana na viini vya tatizo. Hivyo ukamataji wa walarushwa haukuondoa sababu zilizofanya rushwa iwepo.
Aidha ilitarajiwa kuwa adhabu kali zilizoainishwa na sheria zingekuwa tishio kwa wale wanaotarajia kujihusisha katika vitendo vya rushwa na kusahau kuwa adhabu itakuwa na msukumo pale tu ambapo patakuwepo na uhakika wa kugundulika kwa kosa na uhakika wa kuadhibu kosa hilo. Kwa lugha nyingine Serikali haikuchukua hatua mahsusi kuzuia rushwa.
28. Zoezi zima la kampeni dhidi ya wahujumu uchumi halikuzaa matunda yaliyotarajiwa. Wengi waliofikishwa kwenye mabaraza waliachiwa. Wengine ambao mali zao zilikamatwa ilibidi wafidiwe na Serikali. Maofisa kadhaa wa vyombo vya dola vilivyohusika walitumia mamlaka waliyokuwa nayo kujilimbikizia mali. Jitihada zote za Serikali zilikuwa ni bure.
29. Baada ya kutambua upungufu uliojitokeza mwaka 1984 Serikali iliamua kuruhusu wenye fedha za kigeni kuingiza bidhaa nchini bila kuulizwa walikopata fedha hizo. Hali hii ilifanya tatizo la uadimu wa uhaba wa bidhaa, hasa kwenye mashirika ya umma, ilitoweka pia.
Uamuzi wa Serikali kufungua milango uliweza kumaliza aina ya rushwa ambayo matumizi ya sheria yalikuwa yameshindwa kukabiliana nayo. Aidha ulegezaji wa masharti ya biashara ulileta aina nyingine ya rushwa na matatizo mapya katika jamii yetu.
Bidhaa nyingi zilizoingizwa hazikuwa zinalipiwa kodi ya ushuru na hata ongezeko kubwa la biashara halikwenda sambamba na ulipaji wa kodi ya mapato. Pia fedha nyingi ziliingia nchini na kutolewa kwa njia ambazo uhalali wake hauwezi kudhibitiwa.
Hii iliongeza nchini mzunguko wa fedha kutoka nje (money laundering) na hii ikawa chanzo cha biashara ya madawa ya kulevya. Madhara mengine yaliyotokana na uamuzi huu bila ya kuweka masharti sahihi ilikuwa ni kuua viwanda vyetu, kama vya nguo, kwa kuingiza bidhaa hafifu ambazo hazihitajiki nchi nyingine (dumping).
SURA YA TATU
UONGOZI NA MAADILI
1. Azimio la Arusha la mwaka 1967 lilitamka kwamba, ili tuendelee tulihitaji Ardhi; Watu; Siasa Safi; na Uongozi Bora. Ardhi na watu tunavyo kwa wingi sana. Aidha pamoja na makosa ya hapa na pale ya utekelezaji, siasa na sera za Azimio la Arusha zililenga kumwendeleza mwananchi bila ubaguzi na upendeleo.
2. Kwahiyo dhahiri kuwa tatizo lililolikumba taifa kwa kiwango kikubwa ni kupata “VIONGOZI BORA”. Kushamiri kwa rushwa katika nchi ambayo viongozi wake walikula kiapo cha kutojihusisha na vitendo vya rushwa, kunadhihirisha wazi wazi kwamba mwelekeo wa Taifa ulipotoshwa na viongozi waliosaliti ahadi na uaminifu wao kwa wanaowaongoza kwa manufaa ya binafsi.
3. Imedhihirika wazi kwamba chanzo kikubwa cha rushwa kukithiri hapa nchini sio uchumi na mishahara duni ingawa haya pia yamechangia. Lakini ni dhahiri kwamba chimbuko lake hasa ni udhaifu wa uongozi katika kusimamia taratibu chimbuko lake, hasa ni udhaifu wa uongozi katika kusimamia taratibu zilizowekwa. Kutokuwa na kanuni za wazi wazi juu ya kuwajibika kwa viongozi katika nafasi zao, iwe ni uongozi wa kisiasa au wa kiutendaji, ni sehemu ya udhaifu huo.
4. Mathalan kanuni za utendaji serikalini (Standing Orders; Financial Orders, na kadhalika) ndizo zilikuwako tangu nyakati za mkoloni. Sehemu kubwa ya Sheria ya Ukusanyaji ya Kodi ya Mapato ni ile ile. Aidha, sehemu kubwa ya sheria ya ukusanyaji wa ushuru wa forodha pia ni ile ile. Kilichobadilika ni viwango vya ushuru na kodi, na upana wa wigo wa kodi ambao kwa kweli umepanuka kuliko hata wakati wa miaka ya mwanzo wa uhuru.
5. Kwa kutumia sheria na kanuni hizo, tangu mwaka 1961 na kabla na hadi kufikia mwaka 1978, Serikali ilikuwa inakusanya mapato ya kutosha kulipia gharama za kuiendesha Serikali na kuacha ziada kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Mpaka mwaka 1978, misaada yote toka nchi za nje ilikuwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
6. Ingawa kwa sehemu fulani matatizo ya upungufu wa mapato yalisababishwa na vita vya Uganda, lakini kwa sehemu kubwa upungufu huu umeletwa na utovu wa nidhamu kwa watendaji na usimamizi duni wa vyombo vyetu vya kukusanya kodi ambao umesababisha pia rushwa kukithiri katika vyombo hivyo.
7. Hali hiyo iliongezewa ubovu na kushuka kwa maadili katika idara kuu za Serikali hasa HAZINA ambao ndio wenye jukumu la kuweka sera za ukusanyaji mapato ya Serikali na kudhibiti matumizi. Aidha, ubadhirifu katika idara za Serikali limekuwa ni jambo la kawaida na la kujivunia kwa wale wanaonufaika kutokana na ulegevu huo wa udhibiti wa HAZINA. Utoaji na hifadhi ya stakabadhi za mapato haudhibitiwi ipasavyo; wakati taratibu za udhibiti wa fedha – yaani mapato na matumizi hazifuatwi kwa ukamilifu.
8. Ni dhahiri kwamba kama tunataka kuondokana na rushwa, lazima tuanze na usafishaji wa safu za uongozi wa juu. Tukumbuke kwamba kazi kubwa ya uogozi ni “kutatua matatizo.” Kwahiyo kiongozi bora ni yule anayeandaa taratibu nzuri za kutatua matatizo ya jamii, yaani matatizo ya maendeleo, uchumi, ulinzi na usalama, na kadhalika.
Sharti moja muhimu la taratibu nzuri ni kwamba ziwe wazi na ziwawezeshe viongozi kufanya maamuzi ya haraka na ya haki. Aidha taratibu nzuri za kazi katika chombo chochote kiwe ni cha umma au cha binafsi ambacho kinatoa huduma kwa umma, lazima ziwe ni taratibu ambazo zinaeleweka na kutekelezeka kwa urahisi na hivyo zisiwe ni mzigo kwa wananchi hasa wanyonge ambao upeo wao wa kufahamu mambo ni mdogo.
9. Kwa hali hiyo, ingawa si kazi ya Tume hii kuwanyooshea vidole watu, Tume inawajibika kushauri juu ya njia nzuri za uongozi wa nchi yetu. Tume inaamini kwamba nchi inaweza pia ikaweka vigezo vinavyoeleweka na kila mmoja kuwa ndivyo kipimo kizuri cha uongozi bora na kumhitaji kila kiongozi ajipime mwenyewe kwa vigezo hivyo ambavyo vinajulikana kwa wote; na halafu ajihukumu kama anadhani bado ana sifa za kuendelea kuwa kiongozi au la.
Wananchi na chombo au vyombo vinavyohusika vimhukumu kila mmoja baada ya hukumu yake binafsi kujulikana na wote. Dhana ya zoezi hili ni kuhakikisha viongozi sio tu wanaonekena ni safi mbele ya wananchi, bali matendo yao yanaashiria heshima kwa dhamana waliyopewa na wananchi.
10. Kazi kubwa inayolikabili Taifa ni kuhakikisha kwamba nchi inaongozwa na watu wanaofuata na kuheshimu maadili. Uamuzi huo ndio ambao wananchi wanaungoja kwa hamu na ndio utakaoamua pia hatima ya nchi yetu. Huu ni uamuzi unaolitaka Taifa kuwa na utamaduni utakaoliwezesha kutambua wazi wazi ni nani kati ya viongozi wake wakiwemo wale wa vyama vya upinzani atakayeliongoza Taifa hili.
Tunasema na “hata wa upinzani” kwa sababu viongozi wote hawa wana dhamana ya heshima ya Taifa letu. Kama viongozi wa vyama vya upinzani watakuwa ni watu wanaotoa au kupokea rushwa hawawezi kuikosoa Serikali na kauli zao zikaheshimika.
Wanaotoa na kupokea rushwa si viongozi wa Serikali peke yao, bali wahusika ni umma wote wa Watanzania. Wananchi ni lazima wakatae kutoa au kupokea rushwa ndipo nchi yetu itakapoondokana na janga la rushwa.
Mpendwa msomaji. Wiki ijayo tutakuletea sehemu ya nne ya ripoti hii ya Jaji Warioba ambayo aliitoa mwaka 1996, lakini hadi leo ina maudhui yenye uhalisia katika maisha ya Tanzania na yanapaswa kufanyia kazi. Usikose toleo lijalo la JAMHURI kila Jumanne. Mhariri.