Kumetokea jambo ambalo nimejitahidi nibaki nalo moyoni lakini nafsi imegoma kabisa.
Nafsi imegoma kwa sababu naamini kulinyamazia kutahalalisha matukio mengine mengi ya aina hii yaendelee kufanywa.
Wiki iliyopita tulipata taarifa ya msiba wa mtu tunayemfahamu. Hana umaarufu, lakini ni binadamu mwenzetu. Huyu alikuwa mfanyakazi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO), Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Jina lake ni Emmanuel Mlangwa. Kama nitakuwa nimekosea jina lake nitaomba radhi. Tulizoea kumwita ‘Ima’ tukifupisha jina lake. Naambiwa hilo jina Emmanuel ndilo linalosomeka kwenye kitambulisho chake cha kazi.
Huyu bwana alikuwa mwenyeji wa Korogwe mkoani Tanga. Amefanya kazi yake kwa uadilifu hadi alipofikisha muda wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Ni raha kuona mtumishi wa umma anafanya kazi na kustaafu akiwa hana doa.
Kumbukumbu zinaonyesha alistaafu rasmi Novemba 19, mwaka huu (2018). Siku mbili baada ya kustaafu, yaani Novemba 21, mwaka huu akatoweka.
Haikuwa kawaida yake kutoonekana nyumbani. Kwa sababu hiyo familia ikaingiwa shaka. Wapo waliotania wakisema huyu bwana kustaafu tu siku mbili keshapata mafao na kuamua kuoa mke mwingine! Kulisemwa maneno mengi ya mizaha na hata ndugu wengine wakafikia hatua ya kumshutumu ndugu yao kwa ‘kuikimbia’ familia baada ya kupata mafao [japo alikuwa hajapata hata chapa moja]. Wapo waliogoma kusadiki mabadiliko ya ghafla ya tabia ya Mlangwa; mtu ambaye kila alikoenda aliiaga familia.
Ndugu na marafiki wakaanza kuhangaika huku na kule kumtafuta mpendwa wao. Wakapita katika vituo vya polisi vyote walivyoweza. Hawakuambua kitu. Wakapita hospitali nyingi, wakianzia Muhimbili. Hawakupata taarifa yoyote ya kuwasaidia.
Wakaenda hadi kazini kwake alikostaafu ‘juzi’ kuuliza ni wapi ndugu yao alikoenda kuishi. Wakaambiwa hapo ameshaondoka, na hajarejea tena.
Mwishowe ndugu wakakata shauri wapite kwenye hospitali mbalimbali kadiri inavyowezekana. Wakafika Hospitali ya Amana, Ilala. Wakajieleza. Waliowapokea wakaanza kupitia vitabu vya kumbukumbu. Mungu ni mwema, wakaliona jina la Emmanuel Mlangwa kwenye kitabu cha orodha ya majina ya marehemu!
Wakaambiwa huo mwili umefikishwa hospitalini hapo baada ya kuokotwa eneo la Kigogo. Inasadikika kuwa kifo chake kilisababishwa na kugongwa gari. Mwili, hasa upande wa kichwani kulivurugwa kabisa. Nani aliyemgonga? Hajulikani. Damu ya mtu asiye na hatia huwa haipotei bure. Kuna siku mhusika atajulikana. Hapo Amana waliutambuaje huo mwili? Mlangwa alitambuliwa kwa sababu alikuwa na kitambulisho mfukoni – kitambulisho cha DAWASA. Aligongwa akiwa na kitambulisho mfukoni.
Hadi wana ndugu wanatambua kuwa ndugu yao amefariki dunia kwa kugongwa gari, na mwili wake uko mochwari ya Amana, hiyo ilishakuwa siku ya sita. Haraka haraka taratibu za kuuchukua mwili kwa ajili ya kuusafirisha zikaanza.
Ikaamuliwa mwili ukazikwe Korogwe. Ndugu wakaomba siku mbili wajiandae. Jumatano wakakutana Amana kwa ajili ya kuuaga na kuanza safari. Nami nikawapo, maana nilimfahamu. Sijui kitu gani kinasubiriwa kupanua mochwari ya Amana! Hali ni mbaya mno. Maiti wanachukuliwa kwa foleni. Majeneza 10 hadi 15 yako kwenye foleni.
Hapa wana ndugu wakakutana na kikwazo cha kwanza cha kuuchukua mwili. Wakatakiwa walipe Sh 240,000 hivi zikiwa ni gharama za kuutunza mwili kwa siku zote nane. Mwili ulikuwa katika hali mbaya, hivyo usingeweza kuenea katika jeneza. Ikatakiwa ndugu watoe Sh 40,000 za dawa ya kusaidia upungue maana ulikwishavimba mno; hali inayoashiria haukupata huduma stahiki wakati wote ukiwa mochwari.
Ndugu zangu, nimejaribu kuyaeleza haya kwa urefu ili yanisaidie kujenga hoja ya kile nilichokusudia kukisema.
Nchi yetu imekamilika kila idara. Nasema hivyo nikimaanisha kuwa vipo vyombo vinavyopaswa kushughulikia masuala ya watu wote bila ubaguzi wala visingizio.
Mlangwa alikuwa na kitambulisho mfukoni mwake. Kwa hiyo mwili ulipofikishwa Amana, mara moja pale mapokezi walitambua mwili wanaoupokea ni wa mtu anayeitwa Emmanuel Mlangwa. Swali, kitu gani kiliwazuia mapokezi kuujulisha uongozi wa Hospitali ya Amana kuwa kuna mwili umeokotwa na kwa bahati nzuri una kitambulisho?
Kama uongozi ulijulishwa kuwa kwenye orodha ya maiti waliookotwa kuna mmoja ametambuliwa kwa jina la Mlangwa; uongozi wa Amana ulishindwa nini kwa wiki nzima kuwasiliana na uongozi wa DAWASA kuutaarifu kifo cha mtu mwenye kitambulisho chao?
Uongozi wa Hospitali ya Amana, kama waliona kuwatafuta DAWASA ni kazi ngumu, ulishindwa nini kutumia mitandao ya kijamii kutoa taarifa kwa umma ya kuokotwa kwa mwili wa mtu mwenye kitambulisho chenye jina la Mlangwa?
Wafanyakazi wa Hospitali ya Amana, hakuna hata mmoja aliyeingiwa huruma akaona ni busara kutoa taarifa kwenye mtandao ili walau ndugu wanaohangaika kumtafuta ndugu yao wasiendelee kuhangaika?
Uongozi wa Hospitali ya Amana siyo ulioufuata huo mwili eneo la tukio. Sina hakika, lakini kwa tukio la aina hii, bila shaka polisi ndio waliofika, wakauchukua mwili na kuupeleka Amana. Kama hivyo ndivyo, polisi walishindwa nini kuwasiliana na DAWASA kuwataarifu juu ya kuokotwa kwa mwili wa mtu anayedhaniwa kuwa ni mtumishi wao?
Ule utaratibu wa polisi kutoa taarifa kwa vyombo vya habari hasa kwa matukio ya kuokotwa au kupotea watu na vitu, umefutwa kwa amri ya nani? Kuna OCS, OCD, RPC, IGP au waziri aliyepiga marufuku kutangaza matukio ya aina hii kwenye vyombo vya habari? Redio, televisheni au gazeti gani litadai malipo kutangaza habari kama hii ambayo ni ya kiutu?
Mlolongo mzima wa tukio hili una vimelea vya uzembe na kutojali. Watanzania hatukuwa na roho mbaya za aina hii. Hili ni zao la ubinafsi na kutojali. Baadhi yetu tumekuwa na roho na akili za kuamini kuwa shida ni shida ya yule aliyefikwa na hiyo shida. Tunapotoka.
Uongozi wa Hospitali ya Amana, kitengo cha mochwari, baada ya kutambua kuwa mwili wa Mlangwa umejulikana, ukawaeleza ndugu kwamba ulipanga uzikwe na manispaa Novemba 27. Sijajua kuna utaratibu gani wa kuzika miili isiyojulikana. Ninachoweza kubashiri hapa ni kuwa manispaa haiwezi kugharimia malipo kwa mwili au miili kwa siku iliyokaa mochwari. Sina hakika. Nadhani kinachofanywa ni huduma tu ya kibinadamu na kwa kweli huo ndio utu.
Kama hivyo ndivyo, kwanini busara hiyo haikutumiwa na uongozi wa Hospitali ya Amana kuutoa mwili kwa ndugu bila malipo? Kwanini walidai takriban Sh 300,000 kwa mwili uliotafutwa na ndugu kwa siku zote hizo? Utu uko wapi kwamba mwili unaokotwa, ndugu hawajui kilichomfika ndugu yao halafu watozwe fedha za kuuweka mochwari? Kodi zinazolipwa na Watanzania haziwezi kweli kuondoa baadhi ya mambo ya aina hii hasa kwa watu wanaookotwa?
Mwisho, tunalalamika watu wengi kutoweka kwa mazingira ya kutatanisha. Kifo cha Mlangwa na staili nzima ya kuupata mwili wake vinanishawishi niamini kuwa kuna Watanzania au binadamu wengi wanaokufa kwa mfumo huu na mwishowe tunasema wanatekwa na kuuawa.
Kweli inawezekana yakawapo matukio ya watu kutekwa na ‘kupotezwa’ lakini kama Manispaa ya Ilala ingemzika Mlangwa na ndugu wasijue kuwa amezikwa, hoja gani ingewaondolea imani kwamba ametekwa na kuuawa?
Huyu ni mmoja, je, kuna watu wangapi wanakufa kwa namna hii na miili yao ikazikwa licha ya kuwa wanavyo vitambulisho? Nisingependa kuhukumu, lakini kwa tukio hili ni wazi kuwa kuna uzembe na roho mbaya vilivyofanywa na watumishi wa Amana na Jeshi la Polisi. Tujenge moyo wa kupendana na kuthaminiana hasa pindi mwenzetu au wenzetu wanapofikwa matatizo.
Ningekuwa na mamlaka ningeuamuru uongozi wa Hospitali ya Amana uwarejeshee ndugu fedha zile Sh takriban 300,000 walizotozwa ili waruhusiwe kuuchukua mwili wa ndugu yao aliyeokotwa akiwa ameuawa kwa gari.
Uongozi wa hospitali zote pamoja na polisi wawe na utaratibu wa kutumia vyombo vya habari kutangaza taarifa za kuokotwa wagonjwa au marehemu bila kujali wana vitambulisho au hawana. Faida za vyombo vya habari, na sasa mitandao ya kijamii, ni pamoja na kufanya kazi kama hizi za kibinadamu.
Poleni wana familia. Emmanuel Mlangwa pumzika kwa amani. Umekufa siku mbili baada ya kustaafu. Inasikitisha, lakini zaidi inasikitisha kuona mchango wako wala haukutambuliwa na watumishi wenzako wa Hospitali ya Amana licha ya kuona kitambulisho chako. Ulikuwa wa maana pale ulipohakikisha wananchi tunapata maji. Umekufa na wema wako umekufa. Umeonekana hauna maana wala faida tena japo ‘umehakikisha’ hauzikwi na manispaa kana kwamba ulikuwa kibaka. Mungu akupokee na upumzike kwa amani. Amina.