Kumezushwa uongo katika vyombo vya habari vya Uingereza ambao mimi nasema usikubaliwe na ukemewe vikali.
Gazeti moja nchini Uingereza limeandika matokeo ya utafiti fulani na kuja na taarifa inayolichafua Taifa letu la Tanzania.
Magazeti, redio, runinga ndiyo njia nyepesi ya kutoa taarifa kwa walengwa. Zipo taarifa au habari elimishi, vipo vichekesho, kuna taarifa za kukashifu na pia kuna vikaragosi.
Kuna upuuzi umetolewa hivi karibuni unaolenga kulidhalilisha Taifa letu huko nje. Macho hayana mpaka wala masikio hayachoki kusikiliza ya ulimwenguni, lakini ubongo wa binadamu huwa unachoka na kuacha kupokea yale yanayoletwa na walimwengu.
Mimi baada ya kuona taarifa ninayoisemea hapa nilikerwa mno hata nikaamua kuwaelezeni wasomaji wenzangu. Kero yenyewe kama hamkubahatika kuisoma, basi niwashirikishe muisome, na kwa pamoja tuikemee inatudhalilisha.
Juzi juzi nilisoma mwenye gazeti moja la kila Jumapili maneno haya “Wazungu wawashika uongo Watanzania.” Mara moja nikajiuliza hii maana yake nini? Iweje Watanzania, Taifa la watu takribani milioni 50 sasa tuwe sote waongo? Sikuamini na wala sitaki kuamini hilo.
Ni vizuri basi niwaelezee na wenzangu yale yaliyojiri katika uongo huo? Mwandishi mmoja ameandika hivi, nanukuu: “Raia wa Tanzaia wametajwa kuongoza duniani katika orodha ya mataifa ambayo wananchi wake si wakweli.” Soma MTANZANIA toleo Na. 8191 la Jumapili tarehe 22 Mei, 2016 uk. 2).
Hivi ni kweli tukubali sisi kuwa ni vinara wa UONGO duniani? Kwa vigezo vipi na kwa uamuzi wa nani?
Sisi kama Taifa tuna hadhi yetu na tunatambulika kama taifa huru tangu usiku wa Desemba 09, 1961 na haijapata kutokea taifa lolote kutusuta kwa tabia mbaya. Iweje leo huko Uingereza gazeti liitwalo The Daily Mail litubandike (label) sifa hii mbaya tusiyostahili? Mimi binafsi nimeona nisikae kimya heri niwajulishe wasomaji wenzangu ili kwa pamoja tuweze kupinga tamko la udhalilishaji namna hii kwa taifa letu.
Kwanza neno UONGO ni nini? Tunalielewaje? Kwangu mimi niliyejifunza dini ya Kikristo nasema UONGO ni kosa baya sana, ni dhambi. Nimefunzwa hivyo shuleni katika somo lile la dini. Tujuavyo, Mwenyezi Mungu alifanya agano na Musa katika mlima ule wa Sinai. Na hapo Mwenyezi Mungu alimpa Musa (babu yetu) mwongozo wa maisha kwa Waisraeli.
Katika Agano la Kale tunasoma maneno haya: “Masharti ya agano: Amri Kumi” Mungu akanena maneno haya yote akasema: Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa…. (katika aya ile ya 16) akasema: “Usimshuhudie jirani yako uongo…” (Tazama Kut. 20:1 – 17). Hapo ndipo tunakuta hiyo AYA ya 16 yenye maneno kuhusu UONGO, Kanisa linafundisha Amri ya 8: “USISEME UONGO”.
Mwalimu wangu wa dini nikiwa Shule ya Sekondari pale St. Mary’s Tabora, Padre Burton W, F. alitutafsiria vizuri sana Amri hii ya Mungu. Ningali nakumbuka maelezo yake yale kuwa UONGO unaweza kutolewa katika njia mbalimbali. Upo uongo wa DHIHAKA (Jocose Lie), upo uongo wa kujinufaisha au kujilinda (officious lie) na upo uongo chafuzi (malicious lie) ambao ni wa kumdhuru mwingine. Lakini, uongo ni uongo tu (a lie is intrinsically wrong, is sinful) ni kosa; na ni dhambi.
Waingereza baada ya Vita Kuu ya II ya Dunia mwaka 1945 walibuni uongo wa dhihaka kwa siku ile ilipomalizika vita, nayo ikaangukia kuwa Aprili Mosi, mwaka ule. Wakatuambia, ruksa kumdhihaki mwenzio kati ya saa 7 usiku mpaka saa 6 mchana tu, kwa siku hiyo ya Aprili Mosi tu. Kwa mapokeo hayo vyombo vya habari BBC Radio na runinga vinaweza kutanganza dhihaka fulani hata kushtua watu.
Kuanzia mwaka 1945 mpaka leo hii, tabia hii bado inaonekana katika nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth countries)
Mwaka huu, Aprili Mosi kuna dhihaka ilisikika kwenye vyombo vya habari hata mimi nilitumiwa meseji kwenye simu yangu ya kiganja, kuelezwa kuwa Baba Mtakatifu Francis I ameamua kuzuru Tanzania mwezi Juni mwaka huu eti ni safari yake ya kwanza nje ya Vatican tangu kuteuliwa kuwa Papa.
Taarifa za dhihaka namna hii zinavumishwa kila mwezi Aprili. Waingereza wanaita siku hiyo “FOOLS DAY” – SIKU YA WAJINGA. Pamoja na kuwa na mapokeo hayo bado uongo wa aina hiyo ni dhambi tu.
Mimi makala yangu inazungumzia ule UONGO chafuzi (malicious lie) uliotuhusu Watanzania. Mwandishi wa habari hii aliandika hivi: “Raia wa Tanzania wametajwa kuongoza duniani katika orodha ya mataifa ambayo wananchi wake si wakweli”. Maneno haya yameandikwa katika gazeti moja la Uingereza liitwalo The Daily Mail la tarehe 09 Machi, na kurudiwa katika Daily Mail la Machi 11, 2016. Msingi wa maneno yale umetokana na utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Nottingham, Uingereza na umeongozwa na mtaalamu anayeitwa Simon Gächter.
Gazeti la Mtanzania la Jumapili toleo No. 8191 uk. 2 la Mei 22, 2016 hii liliandika kuwa Chuo kile kiliwahojii watu 2,586 kutoka nchi 159 mwaka 2003 na ndipo wakaja na majumlishi yao hayo kuwa miongoni mwa nchi hizo 159 wakaona nchi kinara wa uongo miongoni mwa wananchi wake ni Tanzania.
Nchi yetu inafuatiwa na Morocco, kisha nchi ya Uchina, ikifuatiwa na Uturuki na mwisho ni nchi ya Poland. Mataifa hayo ndiyo watu wake hawasemi kweli – maana yake ni WAONGO.
Kuthibitisha hilo wakatoa vigezo kadhaa walivyotumia katika utafiti wao huo. Gazeti la Daily Mail liliainisha vigezo vilivyotumika kuwa (1) Hali ya Siasa ya nchi hizo (2) Taarifa za ukusanyaji mapato, yaani kodi zinazolipwa na wananchi, na (3) Hali ya Rushwa katika nchi hizo.
Baada ya kuangalia yote hayo na kupata takwimu au data walizohitaji kutoka kwa watu 2,586, miongoni mwa hao waliwasaili Watanzania wangapi? Kama idadi hiyo kutoka nchi 159 ni wazi kwa hesabu yangu kamati yao iliweza kuhoji watu 15 tu kila nchi. Hapo kweli ni sahihi kutoa mabandiko ya jumla jumla namna hii? Wanathubutuje watafiti hawa kutamka kuwa Wazungu wawashika uongo Watanzania? Huu ni utafiti wa kipuuzi.
Ili kupata takwimu barabara ni lazima kuonana na wananchi wa kutosha kutoka maeneo mbalimbali ya nchi (cross cutting interview) walau utoe, jumlisho la kisayansi (a scientific analysis is required to justify such a conclusion). Waingereza wanasema kutoa matamshi ya ujumla ni kuropoka (to give a sweeping statement or to generalize a statement is very unacceptable phenomenon) na uropokaji namna hiyo basi upuuzwe.
Utafiti ule umeendelea kwa kujipendelea. Wakasema kuwa katika ulimwengu nchi inayoongoza kwa wananchi wake kusema ukweli ni Uingereza, ikifuatiwa na Uholanzi. Aidha, nchi nyingine kama Lithuania, Sweden, Ujerumani na Italia ni safi kwa maana watu wake wanasema kweli. Mataifa haya yanafanya vizuri katika mambo yao ya siasa, wanakusanya kodi vizuri na wanadhibiti mambo ya rushwa. Kwa vigezo hivyo nchi hizo zinaaminika kuwa hawasemi uongo.
Inashangaza kupata ripoti namna hii. Sisi Watanzania tunawajua Waingereza kuwa walitutapeli katika mauzo ya radar. Tuna mgogoro nao katika ukopeshaji fedha kupitia moja ya benki zao (Standard Chartered Bank). Hao ni wababaishaji, na ubabaishaji au utapeli ni aina ya udanganyifu ambao ni uongo. Hapo utafiti wao kule Nottingham ni wazi umeegemea upande fulani yaani ni “biased” na umewasakama Watanzania. Ni mtazamo usio sahihi kwa maoni na mtazamo wangu.
Kusema Watanzania wanaonesha kiwango kikubwa cha rushwa miongoni mwao si kweli. Waafrika kwa asili yao hawajui kuhonga. Makabila yote ya Wabantu hayana tabia ya kuhonga. Kumbe rushwa imeletwa na Wazungu hao hao, na wageni wengine enzi za utumwa na ukoloni walipowalaghai machifu ili kupata ardhi na hao watumwa.
Nirejee maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema haya: “Safari moja, Mgiriki mmoja alipita pita anajitapatapa humu anasema mimi Serikali yote ya Tanzania iko mfukoni mwangu. Nikasema, ‘mshenzi sana huyu. Serikali yote ya Tanzania iko mfukoni mwake? Ana mfuko mpana kiasi gani?….. nikajua anahonga watu. Hawezi kusema hivyo bila kuhonga watu, lakini vigumu kumpata. Lakini nikaona hata hivyo nitamfundisha tu. Nikamtia ndani.’” (Nyerere: NYUFA uk. 17).
Hapo tu inaonekana mhongaji au mtoa rushwa ni Mzungu na mpinga rushwa (Baba wa Taifa) ni Mtanzania. Huo ni mfano wa kuwakemea watafiti wale waliotangaza kuwa Watanzania ni vinara wa kusema uongo duniani huku Wazungu ni wasema ukweli daima. Basi, Wazungu wasitutangaze kuwa sisi si wasema ukweli. Chuo Kikuu cha Nottingham kimetudhalilisha kama Taifa, mamlaka husika iwakemee na kutaka wasahihishe tamko lao.
Hatukatai katika kila taifa wapo baadhi ya wenye tabia ya kusema uongo. Hivi karibuni tumejiona katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, maofisa kadhaa walivyojikanyaga kusema uongo wa kujiokoa (officious lies) pale Rais alipowataka wamwelezee mashine zile za kukagua mizigo ya abiria wanaoingia nchini (arrivals) zinafanya kazi au hazifanyi. Ulikuwa ni uongo wa kujiokoa tu. Mheshimiwa Rais aliwaelewa akabaki anasema: “Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Nielezeni ukweli tu.”
Kule Ulaya Wazungu wapo wa aina mbalimbali. Wapo waongo na wasema kweli. Tabia moja Wazungu wanayo ni pale wanapoona kosa ni wepesi kuomba msamaha na kujirekebisha. Kwa tabia namna hiyo tumeona wameweza kuturudishia fedha zetu za radar walizotutapeli na ndizo fedha zilizopelekwa elimu kununua vitabu kwa watoto wetu.
Mimi kinachoniuma ni watafiti wale wa Nottingham kutoa majumuisho kwa Watanzania wote kuwa wasema uongo wakati wamepata mawazo na maoni ya watu wachache tu! Pili, kuonesha kuwa Waingereza hawasemi uongo limenishangaza maana walitudanganya katika ununuzi wa radar. Hivyo si sahihi kutangaza sifa mbaya kwa taifa zima wakati utafiti haukuwa wa kisayansi. Huu ulikuwa ni uongo chafuzi kwa Taifa letu. Nishauri wahusika walikemee hili na kutaka Chuo Kikuu cha Nottingham wafute matokeo yale ya utafiti wao.
Watanzania wengi ni wacha Mungu na hivyo wanashika amri za Mungu. Ni wa kweli. Tusikubali kamwe kusingiziwa uongo huu nchini mwetu na hata duniani kote. Uongo wowote ule ni kitu kibaya – “A LIE IS INTRINSICALLY WRONG”. Kama wasomaji mliwahi kuyasoma haya, basi tusimame kidete kuomba mamlaka husika (hapa ni Serikali yetu) kupitia Ofisi ya Mambo ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoa dokezo la kupinga kauli ya utafiti ule (a note of protest diplomatically) uliofanywa na kutangazwa na Chuo Kikuu cha Nottingham, Uingereza, Machi mwaka huu.
Tanzania, Tanzania, nakupenda kwa moyo wote. Nchi yangu Tanzania, jina lako ni tamu sana. ADIOS.