Juma lililopita nilizungumzia kwa ufupi unyonge wa Mwafrika, ambao Mwalimu Julius Nyerere amesema unyonge huo uko wa aina mbili.  Unyonge wa kwanza amesema ni unyonge wa MOYO, unyonge wa ROHO.  Unyonge wa pili ni unyonge wa UMASKINI.

Leo nazungumzia unyonge wa pili ambao ni umaskini. Afrika ni bara tajiri lenye mali nyingi aina aina kuanzia ardhi yenye rutuba, milima yenye majabali, madini, misitu, mito, maziwa, wanyama, ndege na wadudu.

Mali yote hiyo imezungukwa na Waafrika, lakini Mwafrika huyo ni maskini. Sababu iliyomfanya kuwa hivyo ni unyonge. Unyonge wa kutawaliwa kimabavu na kifikra. Yaani unyonge wa moyo, wa roho na umaskini.

Mwalimu Nyerere aliliona suala hilo la unyonge wa Mwafrika, ndipo alipowataka walimu wenzake waondokane na unyonge wa moyo, wa roho na umaskini. Aliwaambia kufanya mapinduzi ya kuondoa unyonge wa Mwafrika.

Kwanza, walimu kuondoa wao unyonge, pili kufanya mapinduzi katika mafundisho yao kwa kufunza wanafunzi elimu ya kuondoa unyonge na kujenga elimu ya kujiamini na kujitegemea katika rasilimali zao.

Ukweli walimu walifanya mapinduzi hayo kwa kutoa elimu ya kujitegemea, mapinduzi ya kilimo, kuwaelekeza vijana shuleni kwenda vijijini, kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kusaidia kumjenga Mwafrika mpya; Mwafrika mwenye kujiamini.

Walimu walimkariri Mwalimu Nyerere aliposema, “Hatuna budi tujenge Mtanzania mpya. Tujenge Mwafrika mpya ambaye hana unyonge huu. Halafu nchi zetu tuziondoe katika hali ya kukosa chochote; ya umaskini”.  Je, Afrika iko hivyo?

Tanzania ni moja kati ya nchi zilizomo barani Afrika. Ni nchi tajiri, lakini wananchi wake ni maskini. Baada ya uhuru wa bendera, walimu na wananchi walijitahidi kuelewa falsafa za Mwalimu na kulikubali Azimio la Arusha.

Azimio la Arusha lilikuwa dira ya kuondoa unyonge wa Mwafrika, unyonge wa Mtanzania; nasema kwa kukosa bahati, Azimio hilo kumbe lilibebwa na watu wa aina mbili. Wana-Azimio na wapinga Azimio.

Wana-Azimio walionesha ari, lengo na mustakabali mzima wa kujitegemea. Hadi leo malengo na madhumuni ya Azimio hilo yanakubalika na hawa vijana wapya! Isipokuwa  wanakosa walimu na viongozi wa kuwapa hamasa juu ya Azimio.

Hamasa hiyo inakosekana kwa sababu hao waliorithishwa Azimio la kuondoa unyonge, hawataki kulisikia wala kulitekeleza. Wameondoa miiko, kanuni na maadili ya Mtanzania, kwa madai eti imepitwa na wakati.

Cha kushangaza, vinywa vyao vinaimba kujitegemea ndiyo njia pekee ya kuondoa unyonge wa Mtanzania. Wakati macho na miguu yao kila uchapo vinaelekea ughaibuni kwenda kuomba misaada, kunadi na kutoa zawadi mali za Watanzania.

Wanafanya hivyo si kwa kulazimishwa, la hasha! Ni unyonge wao wa moyo, wa roho na umaskini — umaskini wa fedha na umaskini wa fikra. Huu umaskini wa fikra ni mbaya, unanyonya mtu kuwa dhalili.

Si hivyo tu; walimu ambao walitakiwa kuwa walimu wa mapinduzi, si walimu wa kulaza watu usingizi, leo ndiyo wamekuwa wa kulaza watu usingizi mnono kwa sababu wananyanyaswa na kudhalilishwa katika kazi na haki zao.

Walimu wanajitahidi kufurukuta kutoka kwenye ufukara, Serikali inazidi kuwabana na kuwaahidi malipo kesho, mazingira duni ya kazi na nusu heri huo ndiyo unyonge wa umaskini.

Serikali inapothubutu kuuza mashirika ya umma kwa kisingizio eti cha kuwekeza, huo ndiyo unyonge wa umaskini, kugawana nyumba za Serikali kwa kisingizio cha kuuziana, kuondoa gharama za kuzitunza ndiyo unyonge wa moyo; wa roho.

Kiongozi unapolikoroga na kupindua tumaini la makabwela, unapobadili haramu kuwa halali, unapojikita kwenye biashara kwa kuchukua mali ya umma na unapokuwa mtalii na mchuuzi huo ndiyo unyonge wa umaskini.

Kiongozi anapojivisha majoho ya unyonge wa moyo, unyonge wa roho na unyonge wa umaskini na kuwaacha watu wako katika ufukara na umaskini, ukweli hafai kuwa kiongozi. Yeye ni sawa na Yohana Mtembezi.

Lini viongozi wa Serikali na vyama vya siasa, mtatambua unyonge wa Mwafrika? Wazee wetu (mababu) walikataa, lakini walishindwa kutokana na kutawaliwa kimabavu. Vipi leo ninyi viongozi mara mnatoa na kuruhusu unyonge wa moyo, wa roho na wa umaskini?  MTAFAKARI.