Duniani kote, vifo vya watoto wachanga bado viko juu sana kiasi cha kuwa tishio, hasa miongoni mwa nchi maskini zaidi ulimwenguni, UNICEF imesema katika ripoti yake mpya kuhusu vifo vya watoto iliyozinduliwa leo mjini New York. Ripoti hiyo imebainisha kuwa watoto wanaozaliwa katika nchi za Japani, Iceland na Singapore wana nafasi kubwa zaidi ya kuishi, wakati wale wanaozaliwa katika nchi za Pakistani, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Afghanistani wanakabiliana na hatma mbaya kabisa ya maisha yao.
“Wakati ambapo tumepunguza kwa zaidi ya nusu idadi ya vifo miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano katika robo karne iliyopita, bado hatujafaulu kwa kiwango kama hicho katika kukomesha vifo miongoni mwa watoto walio na umri wa chini ya mwezi mmoja,” alisema Henrietta H. Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF.
“Kwa kuwa vifo hivi vingi vinazuilika, ni wazi kwamba, tumewaangusha watoto walio maskini zaidi duniani,” alisisitiza mkurugenzi huyo wa UNICEF. Ulimwenguni, katika nchi za kipato cha chini, wastani wa vifo vya watoto wachanga ni vifo 27 katika kila vizazi hai 1,000, ripoti inasema. Katika nchi za kipato cha juu, kiwango ni vifo 3 kwa kila vizazi hai 1,000. Nchini Tanzania, viwango vya vifo vya watoto wachanga ni 25 katika kila vizazi hai 1,000, kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na Afya wa Tanzania (TDHS 2015-16).
Ikiwa kila nchi itapunguza viwango vya vifo vya watoto wake wachanga hadi katika viwango vya nchi za kipato cha juu ifikapo mwaka 2030, maisha ya watoto milioni 16 yataokolewa, ripoti hiyo imebainisha. Ripoti hiyo inaeleza pia kwamba miongoni mwa maeneo 8 kati ya 10 yaliyo hatari zaidi kwa mtu kuzaliwa, basi Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, ni mojawapo, ambapo wanawake wajawazito wana uwezekano mdogo wa kupata msaada wakati wa kujifungua kwa sababu ya umaskini, migogoro na taasisi zisizo na ufanisi. Watoto wanaozaliwa katika nchi zenye hatari zaidi wana uwezekano wa hadi mara 50 wa kufa kulinganisha na wale wanaozaliwa katika nchi zilizo salama.
Nchini Tanzania, kuna hatua kubwa imepigwa katika kupunguza vifo miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, hata hivyo hatua hiyo bado haijafikiwa katika kukomesha vifo vya watoto wachanga na akina mama. Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu sana vya vifo vya watoto wachanga duniani: takribani watoto 39,000 hufariki kila mwaka, miongoni mwao, 17,000 hufa katika siku yao ya kwanza duniani. Wengine zaidi 47,550 wanazaliwa wakiwa wameshakufa na akina mama wapatao 8,000 hufa kila mwaka wakati wa kujifungua. Kuna hatua kubwa imepigwa nchini inayowapa watoto wa Kitanzania nafasi kubwa zaidi ya kuishi hata baada ya kutimiza miaka mitano tangu kuzaliwa kwao.
Hata hivyo, bado kuna changamoto. Kila siku, watoto 270 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufa, wengi kutokana na magonjwa yanayozuilika kama vile malaria, homa ya mapafu na kuhara. “Karibu vifo 6 katika 10 hutokea katika siku yao ya kwanza ya maisha, wakati vifo 4 katika 10 hutokea katika mwezi wa kwanza wa maisha. Tunaweza kuokoa vifo hivi kwa huduma rahisi na nafuu, zilizo bora ambazo zinapaswa kumfikia na kufikiwa na kila mama na mtoto wake mchanga kote nchini.
UNICEF imedhamiria kuunga mkono juhudi za serikali katika kupunguza viwango vya vifo vya watoto wachanga. Sote tunapaswa kudhamiria kumpa kila mtoto nafasi stahiki ya kuanza maisha. Ni haki na jambo la maana la kufanya,” alisema Maniza Zaman, Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya asilimia 80 ya vifo vya watoto wachanga vinatokana na kuzaliwa njiti, matatizo wakati wa kujifungua au maambukizi kama vile homa ya mapafu na bakteria katika tishu.
Vifo hivi vinaweza kuzuiwa kama huduma ya zuazi itatolewa na wakunga wenye mafunzo, huku kukiwa na uhakika wa maji salama, dawa za kuzuia vijidudu, unyonyeshaji katika saa ya kwanza, kumkumbatia mtoto na lishe bora. Hata hivyo, upungufu wa watumishi wa afya wenye mafunzo bora na wakunga kunamaanisha kwamba maelfu hawapati msaada huu muhimu wa kuokoa maisha yao katika kipindi hiki muhimu.
Kwa mfano, wakati ambapo huko Norway kuna madaktari, manesi na wakunga 218 wa kuwahudumia watu 10,000 uwiano ni 1 kwa kila wahitaji huduma 10,000 kule Somalia. Mwezi huu, UNICEF inazindua kampeni kote duniani ya Every Child ALIVE (Kila Mtoto Abaki HAI), ambayo inataka na kutoa suluhisho kwa ajili ya watoto wachanga wa ulimwengu. Kupitia kampeni hiyo, UNICEF inatoa wito wa haraka kwa serikali, watoa huduma za afya, wafadhili, sekta binafsi, familia na biashara kuhakikisha kila mtoto anabaki hai. “Kila mwaka, watoto wachanga milioni 2.6 kote duniani huwa hawaishi zaidi ya mwezi wao wa kwanza. Watoto milioni moja hufa siku ileile wanapozaliwa,” alisema Fore.
“Tunajua kwamba tunaweza kuokoa uhai wa watoto walio wengi miongoni mwa hawa kwa suluhu rahisi na matunzo bora ya afya kwa ajili ya kila mama na kila mtoto mchanga. Hatua chache ndogondogo kutoka kwa kila mmoja wetu zinaweza kusaidia kuhakikisha kunakuwa na upigaji hatua kwa kila uhai mpya wa watoto hawa wachanga.” Nchini Tanzania, kampeni ya mwaka mzima imepangwa ili kusaidia upazaji sauti kuhusu masuala yanayohusua akina mama na watoto wachanga nchini. Lengo litakuwa ni kuunda vuguvugu la kitaifa kuhusiana na suala hili, kwa kulenga vijana walio kwenye balehe na walio hatarini zaidi, wanawake wajawazito na wanawake wanaonyonyesha.