Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Manyara

Mkoa wa Manyara unatajwa kuwa kwa sasa una jumla ya idadi ya watu millioni moja, laki nane na elfu sabini na tano sawa na ongezeko la asilimia 3.2.

Ameyaeleza hayo Mkuu wa Mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere leo Julai 19,2022 katika kongamano la wiki ya maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani ambalo limekutanisha makundi mbalimbali ya watu na viongozi kutoka Tanzania Zanzibar na Bara.

Kwa upande wake katibu tawala Mkoa wa Manyara Carolina Mthapula amesema kilele cha maadhimisho hayo kitaifa kitafanyika wilayani Hanang’ na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania majaliwa kasim majaliwa.

Naye mwakilishi mkazi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani Ramadhani Hangwa, amesema changamoto ambazo wamezibaini ndani ya mkoa wa Manyara ni ukeketaji, ubakaji pamoja na ulawiti ambapo amesema ili kukabiliana nazo ni kuendelea kuwekeza kwa makundi maalum.

Mchambuzi wa masuala ya idadi ya watu na maendeleo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Wtu (UNFPA),amadhani Hangwa amesema muda wa kuishi kwa Watanzania umeongezeka kutoka wastani wa miaka 61 hadi miaka 66 mwaka 2022.

Hangwa amesema uboreshwaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya na maji ni miongoni mwa sababu za ongezeko hilo.

Siku ya Idadi ya watu Duniani kwa Tanzania itaadhimisha Julai 20,2022 katika viwanja vya shule ya Msingi Katesh B Wilayani Hanan’g mkoani Manyara ambapo kumetanguliwa na kongamano maalum la kujadili fursa na changamoto za ongezeko la idadi ya watu Duniani.

Tanzania pia inatajwa kunufaika na maboresho makubwa yaliyofanyika katika huduma za kijamii ikiwemo Afya na Maji.

Kamishna wa tume ya Mipango Zanzibar Salma Makame amesema Suala la ongezeko la idadi ya watu hapa Tanzania ni baraka na kwamba kupitia uchumi wa buluu wameshaandaa mpango maalum wa Kilimo halisi kwa ajili ya vijana.

Siku ya Idadi ya watu Duniani huadhimishwa kila Julai 11 ambapo hapa nchini maadhimisho hayo yalipisha Sikukuu ya Idi.

Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu” Dunia ya watu Bilioni nane kuhimili wakati ujao ni fursa ya haki kwa wote,Shiriki Sensa kwa Maendeleo Endelevu”