Na Mwandishi Wetu,Arusha
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) kupitia Programu ya miradi midogo(SGP) nchini, limeahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya kusaidia jamii za Pembezoni(MAIPAC) katika kutekeleza miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa mazingira na Misitu na Vyanzo vya maji.
Maafisa wa UNDP kupitia programu ya miradi midogo(GSP),pamoja na maafisa wa Taasisi ya Jumuiko la Maliasili Tanzania(TNRF) leo Julai 25,2023, wametembelea Ofisi ya MAIPAC jijini Arusha, kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi wa uhifadhi wa misitu,Maji na Mazingira kwa maarifa ya asili, uliokuwa unatekelezwa na MAIPAC katika wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro.
Akizungumza watendaji wa MAIPAC, Afisa Programu ya miradi midogo(SGP) wa UNDP Tanzania, Faustine Ninga, amesema wameridhishwa na MAIPAC jinsi ilivyotekeleza mradi huo, ambao ulikuwa unadhaminiwa na mfuko wa mazingira duniani(GEF) na wadau wengine wa maendeleo.
“Tumekuja hapa kuona jinsi ambavyo mmetekeleza mradi wenu, kwa ujumla tunawapongeza sana MAIPAC, mmefanyakazi nzuri kuzifikia jamii za pembezoni na kukusanya maarifa mengi ya asili na baadaye kutoa katika vyombo vya habari na kuandaa vitabu”amesema
Amesema MAIPAC imeweza kufikisha ujumbe maeneo mbalimbali juu ya umuhimu wa maarifa ya asili katika uhifadhi wa mazingira, vyanzo vya maji na misitu lakini pia kushirikiana na taasisi nyingine ikiwepo za serikali kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira.
“Tutaendelea kufanyakazi pamoja,kikubwa muendeleze kutoa elimu kwa maarifa ambayo mmekusanya lakini pia kubainisha fursa nyingine ambazo mnaona tunaweza kushirikiana ili kusaidia jamii”amesema
Kaimu Mkurugenzi wa TNRF, Steve Ngoi ambao walikuwa waratibu wa miradi amesema MAIPAC imefanyakazi nzuri ikiwepo kushirikiana vizuri kutoa habari na machapisho za mashirika mengine, ambayo yalikuwa katika progamu ya miradi inayosaidiwa na UNDP.
“Kama walivyosema wenzangu, sisi tumeridhika na utekelezaji wa mradi wenu na tunaimani zikitokea fursa nyingine, mtashiriki vizuri na kuendelea pale ambapo mmeishia”amesema
Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma amesema wanashukuru UNDP kupitia programu ya miradi midogo(SGP) na TNRF kuamua kushirikiana na MAIPAC katika kutekeleza mradi wa uhifadhi wa mazingira,Vyanzo vya maji na Misitu kwa maarifa ya asili.
Juma amesema mradi huo, ambao umetekelezwa kwa mwaka mmoja, umekuwa na manufaa makubwa, kwani jamii imeshirikisha, halmashauri za wilaya ya Longido, Monduli na Ngorongoro lakini pia serikali kuu.
“Mradi huu umekuwa na manufaa makubwa kwani tulimshirikisha hadi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira Dk Suleiman Jaffo ambaye alizindua vitabu ambavyo tulichapa juu ya maafisa ya asili ya asili na kuahidi kuendelea kushirikiana na MAIPAC na wadau wengine katika uhifadhi wa mazingira”amesema
Juma pia amesema pia wanahabari wameshiriki vyema katika kutangaza, kuandaa vipindi na makala maalum juu ya mradi huo ambao ni mara ya kwanza kutekelezwa nchini.
Meneja miradi na Utawala wa MAIPAC, Andrea Ngobole amesema wanaimani wataendelea kushirikiana zaidi na UNDP, TRNF, GEF na serikali ya Ujerumani na wadau wengine katika kutekeleza miradi ya kusaidia jamii, zikiwepo za pembezoni.
Watendaji wa UNDP na kushirikiana TNRF, wapo katika ziara ya kukagua na kufanya tathimini ya utekelezwaji miradi midogo kwa mashirika 13 ambayo yalipatiwa fedha na UNDP kutekeleza miradi midogo nchini