Unaweza kukubali kosa polisi au popote kama serikali za mitaa, sungusungu na baadaye kulikataa kosa hilo mahakamani. Kitu hiki si jambo la kushangaza na tayari sheria imeweka mazingira ya jambo kama hili.
Makala hii hailengi kuwaelekeza wahalifu mbinu, bali kueleza sheria inavyosema. Wapo watu wengi ambao akiwa chini ya ulinzi wa polisi au wananchi wenye hasira hujikuta analazimika au analazimishwa kukiri kosa.
Kwa sababu ya mazingira, mhusika hujikuta amekiri hata kama hakutenda ili kunusuru maisha yake kwa wakati huo. Lakini pia wengine huwa wamepigwa sana, hasa huko mahabusu za polisi. Ni katika mazingira ya namna hii ambapo mtu anaweza kukiri lakini baadaye mahakamani akakataa.
Hata hivyo nitoe angalizo na msisitizo kuwa si vema kukiri kama kweli hujatenda kosa, itokee tu katika mazingira magumu na ya kulazimishwa. Hii ni kwa sababu kunaweza kukawa na ugumu wa kujinasua katika kukiri huko mbeleni mahakamani.
Aidha, yapo maamuzi mengi ya Mahakama Kuu na ya Rufaa yanayoongelea kukiri polisi na kukataa mahakamani, ila tuangalie haya mapya katika kesi ya jinai namba 6/2017 kati ya JAMHURI dhidi ya MUHANGWA SIMON Mahakama Kuu ya Bukoba chini ya Jaji I.C. Mugeta iliyotolewa uamuzi hivi karibuni tarehe 25/9 /2019.
Katika kesi hiyo mtuhumiwa Muhangwa alikiri kosa la kuua mbele ya polisi huko Biharamulo na akaandikishwa maelezo ya kukiri mbele ya hakimu wa Mahakama ya Mwanzo huko Biharamulo. Alipoletwa Mahakama Kuu mjini Bukoba kwa ajili ya kusikilizwa kesi yake akakataa kuwa hajawahi kukiri.
Kawaida katika mazingira kama haya, mahakama hujielekeza katika misingi mikuu mitatu ambayo hutakiwa kuthibitishwa na upande wa mashitaka ili kuonyesha kuwa mtuhumiwa ameamua tu kubadilika lakini alikiri kweli.
Upande wa mashitaka ndio wenye wajibu wa kuitosheleza mahakama kupitia misingi hii kuwa mtuhumiwa alikiri japo sasa anakataa kuwa hakukiri.
Misingi hii ya mahakama nitaieleza ili ikusaidie ikiwa ikatokea ukalazimika kukiri na baadaye kukataa, uweze kujua wanaokushitaki wanatakiwa kuthibitisha nini, au wewe uwahoji/uwaulize nini na katika lipi. Misingi yenyewe ni kama ifuatavyo:
Mosi, wanaokushitaki wawe na ushahidi mwingine unaojitegemea unaoonyesha kuwa kweli umetenda kosa (collaboration). Wasitegemee ushahidi huu wa kukiri pekee, kwa sababu huo tayari umekwisha kuukataa.
Watafute ushahidi mwingine wa kuusaidia huu kuonyesha kuwa hata kama umekataa kuwa ulikiri, bado kuna hili na lile linakuingiza kwenye kutenda kosa.
Ni wajibu wako kuwahoji kuhusu uwepo wa ushahidi mwingine tofauti na huu wa kukiri. Wakikosa, basi kukiri kwako kunakosa nguvu, hivyo kuleta uwezekano wa kuachiwa huru.
Pili, wanaokushitaki wathibitishe kuwa ulikiri bila kulazimishwa. Hii ni kwa sababu kukiri kwa kulazimisha au kushawishiwa ni sawa na kuwa hujakiri/hukukiri. Wathibitishe kuwa hakukuwa na kulazimishwa.
Hapa pia na wewe unayo kazi ya kufanya, kazi yenyewe ni kujitahidi kuonyesha mazingira ya kulazimishwa kukiri, mfano alama za kipigo na mateso mwilini mwako, au mazingira ya hatari kama kuzingirwa na wananchi wenye hasira au kundi, na mazingira mengine yanayofanana na hayo. Ukifanikiwa katika hili, basi umefanikiwa kufuta kukiri kwako na umekaribia kuachiwa huru.
Tatu, wanaokushitaki wathibitishe kuwa ulichokiri ulikuwa ukimaanisha hicho na si vinginevyo. Kwa maana kuwa kukiri kwako hakukulenga kitu kingine chochote bali lile kosa uliloshitakiwa nalo.
Hii ni kwa sababu waweza kuwa ulikiri lakini hukuwa umeelewa kile unachokiri. Ni kazi yao wanaokushitaki kuthibitisha kuwa ulichokiri ulilenga kosa husika, lakini pia ni wajibu wako kama ulikiri bila kuelewa kuonyesha kuwa haukuwa umeelewa unakiri nini au mazingira hayakuwa rafiki kukupa nafasi ya kuelewa ulichokuwa unakiri.
Kwa ujumla wakishindwa kuthibitisha lolote katika haya matatu niliyoeleza, basi ni shaka la msingi katika ushahidi wao hata kama ulikuwa umekiri yafaa mahakama ikubaliane na wewe kuwa hukukiri na uachiliwe huru.
Mwisho, kukiri nilikozungumzia hapa kunajumuisha maelezo unayoandika polisi (cautioned statement), na yale yote unayoandika au kusaini popote nje ya mahakama kabla kesi yako kuanza (extra judicial statement). Hivi ndivyo sheria inavyotaka.