Na Bashir Yakub
Uhaini ni kosa la jinai. Ni kosa kati ya
makosa makubwa ya jinai. Katika jinai yapo
makosa makubwa na yapo makosa
madogo. Yumkini udogo na ukubwa wa
kosa waweza kupimwa kwa kutizama
adhabu ya kosa. Kosa ambalo huadhibiwa
kwa adhabu ndogo huwa ni kosa dogo na
lile ambalo huadhibiwa kwa adhabu kubwa
huwa ni kosa kubwa.
1. Ni sheria ipi hueleza makosa ya jinai?
Sheria zinazofafanua makosa ya jinai zipo
nyingi. Hakuna sheria moja katika makosa
ya jinai. Hata hivyo sheria kuu katika
makosa ya jinai ipo. Ni sheria inayojulikana
kama Kanuni za Adhabu (Penal Code). Hii
ni sheria kuu katika makosa ya jinai.
Ni sheria inayoeleza karibia makosa yote ya
jinai. Mbali na sheria hiyo pia zipo sheria
nyingine kama Sheria ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa, Sheria ya
Uhujumu Uchumi, Sheria ya Ugaidi na
nyinginezo. Hizi nazo hueleza makosa ya
jinai.
Tofauti kubwa kati ya sheria hizi na ile ya
Kanuni za Adhabu ni kuwa hizi sheria
nyinginezo hueleza makosa rasmi ya jinai.
Kwa mfano Sheria ya Ugaidi itaeleza
mambo ya ugaidi tu na si vinginevyo, Sheria
ya Uhujumu Uchumi itaeleza makosa
yanayotokana na uchumi tu na si
vinginevyo, Sheria ya Utakatishaji Fedha
itaeleza utakatishaji fedha tu na si
vinginevyo.
Wakati Sheria ya Kanuni za Adhabu ndani
mwake utakuta makosa tofauti tofauti ya
jinai. Utakuta makosa ambayo hayafanani
na yasiyokuwa na uhusiano.
Utakuta kuhusu kubaka, kuiba, kupigana,
kuua, kuharibu mali, rushwa, kughushi,
uhaini na mengine mengi. Kwa hiyo mtu
anayehitaji kuyajua makosa ya jinai, asome
Sheria ya Kanuni za Adhabu.
2. Ukifanya haya utakuwa umetenda
uhaini
(a) Kifungu cha 39 (1) cha Kanuni za
Adhabu kinasema kuwa mtu yeyote ambaye
yumo ndani ya Jamhuri ya Muungano au
popote akajaribu kumuua Rais atakuwa
ametenda uhaini.
(b) Pia mtu yeyote aliye ndani ya Jamhuri
ya Muungano au popote na akaanzisha vita
dhidi ya Jamhuri ya Muungano atakuwa
naye ametenda kosa la uhaini.
(c) Mtu yeyote ambaye yuko ndani ya
Jamhuri ya Muungano au popote ambaye
atajenga, kusababisha au kuwezesha,
kuchochea, kushawishi, kushauri, kuhusu
kifo, kumlemaza, kumzuia au kufungwa kwa
Rais atakuwa ametenda uhaini.
(d) Mtu yeyote ambaye yuko ndani ya
Jamhuri ya Muungano au popote ambaye
atajenga, kusababisha au kuwezesha,
kuchochea, kushawishi, kushauri
kumwondoa Rais madarakani isivyo halali
atakuwa ametenda uhaini.
(e) Mtu yeyote ambaye yuko ndani ya
Jamhuri ya Muungano au popote ambaye
atajenga, kusababisha au kuwezesha,
kuchochea, kushawishi, kushauri
kumwondolea Rais heshima na jina la Mkuu
wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu au Kiongozi wa
Serikali atakuwa ametenda kosa la uhaini.
(f) Mtu yeyote ambaye yuko ndani ya
Jamhuri ya Muungano ambaye atajenga,
kusababisha au kuwezesha, kuchochea,
kushawishi, kushauri kupindua serikali iliyo
madarakani, kutishia serikali, bunge au
mahakama atakuwa ametenda kosa la
uhaini.
3. Ni ipi adhabu ya kosa la uhaini?
Vifungu vya 39 na 40 vya Kanuni ya
Adhabu ambavyo vimeeleza ni matendo
gani yanaweza kuitwa uhaini, vimeeleza pia
adhabu ya matendo hayo. Vimeeleza kuwa
adhabu ya kukutwa na hatia ya uhaini ni
kifo. Uhaini ni kati ya makosa machache
sana ambayo adhabu yake ni kifo.
Kwahiyo kwa namna yoyote ukijihusisha na
tendo lolote kati ya matendo yaliyotajwa
hapo juu ndipo utahesabika umetenda
uhaini na adhabu yake ni kifo ikiwa
itathibitika mahakamani. Kila kilichoelezwa
hapo juu katika A – F ni tafsiri halisi ya
uhaini.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi,
makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA
YAKUB BLOG.
Mwisho