Na Moshy Kiyungi,
Tabora
Wimbo uliojizolea umaarufu mkubwa miaka ya
nyuma ulikuwa wa ‘Whisky Soda’. Hapana
shaka wenzangu wenye umri mkubwa
watakuwa wanaukumbuka wimbo huo
uliopigwa katika mtindo wa aina yake.
Hiyo ilikuwa ni kazi nzuri ya bendi ya Bembeya
Jazz kutoka nchini Guinea, ambao ulipokuwa
ukipigwa katika redio yoyote, watu walikuwa
wakiufurahia kusikia sauti ya maneno
yasiyoeleweka ya mwimbaji mwenye sauti ya
aliyelewa ‘Chapombe’.
Bendi hiyo inatajwa kama nguzo ya historia ya
muziki wa kisasa katika nchi za Afrika
Magharibi. Mwaka 1958 kulikuweko na kura ya
maoni katika nchi zilizotawaliwa na Wafaransa
huko Afrika Magharibi, ambapo wananchi
waliulizwa kama wanataka kuendelea kuwa
chini ya Ufaransa. Nchi ya Guinea ndiyo pekee
iliyokataa.
Ahmed Sekou Toure akachaguliwa kuwa
rais wa nchi hiyo na miongoni mwa vitu
alivyoanzisha mara moja ilikuwa ni Bendi ya
Taifa iliyoitwa Syli National Orchestra.
Bendi hii iliyokuwa na maskani jijini Conakry,
iliendelea kukua na hatimaye mwaka 1961
ikagawanyika katika makundi mawili ya Bala et
ses Balladins na Keletigui et ses Tambourinis.
Kutokana na upenzi wake wa sanaa, Rais
Sekou Toure akatengeneza bendi za mikoani
ambazo alizifadhili.
Katika Jiji la Beyla, kusini mashariki mwa
Guinea kwenye mwaka 1961, Gavana wa mkoa
huo, Emile Conde, alianzisha kundi lake dogo
akiwa na gitaa moja tu.
Bendi hiyo kutoka mikoani ilishinda mashindano
mengi na kujulikana jijini Conakry. Hatimaye
chama tawala kiliitaka bendi ya Bembeya
ihamie Conakry mwaka 1965. Bendi
hiyo ikataifishwa na kufanywa bendi ya taifa
kama zile nyingine mbili.
Bendi hii ilianza kwa kuitwa Beyla Jazz, lakini
siku moja Aprili 1961, katika mkutano wa bendi
wakaamua kujiita Bembeya Jazz.
Wakati huo Guinea kulikuwa na aina mbili za
wanamuziki, wale waliopiga muziki kutumia
muziki wao wa asili na wale waliotoka kwenye
shule za Kifaransa ambao walipiga muziki wa
charanga, wenye asili ya Cuba.
Amri ilitolewa na serikali kuelekeza wanamuziki
wapige muziki kutokana na vionjo vyao katikati
ya miaka ya 1960. Hivyo ukisikia nyimbo za
Bembeya Jazz kabla ya hapo unasikia vionjo
vya Cuba kama zile za ‘Whisky Soda’ na
‘Mamiwata’
, ni mfano wa upigaji huo.
Baada ya hapo na mpaka ilipokuja kurekodi
mara ya mwisho bendi hiyo imekuwa na vionjo
vya muziki wa asili wa Guinea.
Wakati wa uhai wa Sekou Toure, nchi hiyo
ilianzisha nembo ya kurekodia iliyoitwa
Syliphone. Ilikuwa ni nembo ya taifa, jambo
kama hilo halikuwahi kufanyika popote barani
Afrika.
Tanzania ilijaribu kuiga mfumo huu na iliweza
kutoa kazi chache kwa kutumia Kampuni ya
Filamu Tanzania, kuwa na nembo za TFC na
Sindimba wakati huo.
Nembo hiyo iliweza kutoa albamu 80 na ikawa
ndiyo mwisho wa bendi hiyo. Uchumi wa nchi
ya Guinea uliporomoka miaka ya 1970.
Kutokana na hali ya uchumi kuwa mbaya,
baadhi ya wanamuziki nchini humo wakaanza
kuelekea nchini Ufaransa.
Rais Ahmed Sekou Toure alifanya kazi kubwa
kwa nchi yake kwenye sanaa kuweza kuifanya
Guinea kuwa kati ya nchi zilizoongoza Afrika
katika utamaduni wa muziki.
Kila kizuri hakikosi kasoro. Rais huyo taratibu
akaanza kufanya udikteta mkubwa kwa
watu waliompinga. Kila aliyefanya hivyo
alipotea au kuuawa.
Kama ilivyotokea kwa Fodeba Keita, msanii
aliyeanzisha kundi la kwanza la Ballet nchini
Guinea, Rais Sekou Toure akamfanya Waziri
wa Mambo ya Ndani, lakini kufikia mwishoni
mwa miaka ya 1960, rais huyo akawa na
wasiwasi wa kupinduliwa na Fodeba.
Kwa mamlaka aliyokuwa nayo, alimfunga na
hatimaye Fodeba akapotea wala haikujulikana
alikufa vipi au lini. Pamoja na udikteta huo,
alikuwa tofauti na aliyekuwa Rais wa Zaire,
sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC), Mobutu Sese Seko.
Rais Sekou Toure alikuwa mzalendo, hakuwa
fisadi wa kuiba mabilioni na kuyatorosha nje, ila
aligeuka akawa mkatili kwa kulinda utawala
wake.
Pamoja na maelfu ya Waguinea kuikimbia nchi
yao kutokana na utawala huo, wanamuziki
wachache walimlaani, wengine walifaidika na
fadhila zake katika tasnia ya muziki.
Kufikia mwaka 1980, Bembeya Jazz ilikuwa
haipigi tena maonyesho ya kawaida labda kwa
kukodiwa.
Kati ya mambo makubwa ya kusikitisha
yaliyokikumba kikundi hicho ni kifo cha
muimbaji wao, Demba Camara, aliyefariki dunia
katika ajali ya gari lililokuwa likiendeshwa na
dereva wa bendi hiyo baada ya kupinduka
wakiwa safarini.
Katika gari hilo pia alikuweko Sekou ‘Bembeya’
Diabate (Diamond Finger). Demba alikutwa
ametupwa nje ya gari walipowasili wanamuziki
wengine waliokuwa katika gari jingine.
Mwanamuziki Sekou ‘Bembeya’ Diabate bado
anafanya maonyesho lakini hasa nje ya
Guinea.
Hakuna ubishi kwamba historia ya sanaa ya
Tanzania iliiga baadhi ya taratibu za sanaa za
Rais Ahmed Sekou Toure wa Guinea kwa
kuanzishwa kwa kundi la Sanaa la Taifa.
Si hivyo tu, kwani kulianzishwa bendi ya
wanawake iliyotokana na ziara za rais huyo
hapa nchini, alikuja akisindikizana na kundi
kubwa la wasanii wa kundi la taifa.
Mwisho