Mwishoni mwa wiki nilikuwa Zanzibar. Nilibahatika kulala katika Hoteli ya Shangani. Nilibahatika pia kutembelea maskani mbili za wazee wa Zanzibar kama msikilizaji. Nilifika maskani ya Chama cha Wananchi (CUF), Mji Mkongwe. Huko wananchi wanakula mishikaki na wakati huo huo wanapepeta siasa kwenye chochoro, lakini pia nilifika maskani ya wazee ya Michenzani. Hii ni maskani ya CCM.
Inawezekana ni kwa sababu mwisho wa wiki hii uligongana na ujio wa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuwa ziarani Zanzibar au vinginevyo, lakini niliyoyasikia yanatia shaka. Nilipata pia bahati ya kuzungumza na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman. Nimepata fursa vilevile ya kubadilishana mawazo na wanahabari walioko Zanzibar na wananchi wa kawaida.
Si hao tu, nimepata fursa ya kusikiliza vikao vya Baraza la Wawakilishi chini ya Spika Pandu Ameir Kificho. Nimezisikiliza hoja za Wawakilishi na hamasa waliyokuwa nayo wakati wa kupitisha bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Hapa nimepata wasiwasi. Moyo wangu umekwenda mbio. Mizani yangu imeshindwa kuelewa nini kifanyike. Tunahitaji kukaa chini na kufikiri zaidi.
Moyo wangu umepata majonzi, nimeanza kuona ishara za Muungano kuvunjika. Hapa jamani mnisamehe. Bora nimwambie mfalme kuwa yu uchi kuliko kumsifia huku wapita njia wakimcheka. Nchi yetu imemwagiwa petroli. Kinachosubiriwa ni kichaa kuwasha kiberiti tu, moto usambae.
Sitanii, wakubwa hawa Zanzibar yapo wanayoanza nayo na haya naogopa hata kuyaandika. Sioni jinsi, kwani kazi yangu inanilazimu kufanya hivyo. Wanasema eti tuvunje aina ya Muungano tulionao, Zanzibar iwe na jeshi, iwe na uwezo wa kusaini mikataba ya kimataifa, iwe na mawaziri wake wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, iwe na polisi wake na mengine mengi sawa na yalivyo mataifa ya Ulaya.
Tena kwenye maskani nilizozitaja, wakubwa wanakwenda mbali zaidi kwa kusema hawahitaji tena Serikali ya Muungano, bali wanahitaji kuwa na Kamisheni kama ilivyo Kamisheni ya Ulaya. Zipo hoja nisizokubaliana nazo kwamba eti katika Jumuiya ya Afrika Mashariki wanawakilishwa na nani? Wanasema Wizara ya Afrika Mashariki anayoiongoza Samuel Sitta si ya Muungano.
Hapa sipendi kukubaliana nao sana. Wizara ya Afrika Mashariki ilikuwa idara chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, hivyo nathubutu kusema Idara hii imepewa nguvu zaidi ila bado ni katika muktadha ule ule wa mambo ya nje. Na hapa nadhani hawatalalamika sana kusema hawajapewa fursa ya kuongoza wizara hii, kwani yuko Mzanzibari mkongwe, Balozi Ahmed Hassan Diria, aliyepata kushika wadhifa wa uwaziri katika wizara hii tena kwa muda mrefu.
Sitanii, katika maskani zile yapo waliyoyazungumza ambayo nami nakubaliana nayo. Eti leo wanahoji ikiwa Jeshi la Polisi ni la Muungano nini kimeshindikana tangu enzi za Uhuru kumpata Mzanzibari angalau mmoja akawa Mkuu wa Jeshi la Polisi? Nini kimeshindikana kwa kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni mali ya Muungano, hadi leo tumekwamishwa na nini kumpata Mkuu wa Majeshi angalau mmoja kutoka Zanzibar? Usalama wa taifa je?
Kuna utani unasemwa mitaani, eti askari wa Zanzibar ni ‘mdebwedo’. ‘Wengine wanasema hata wakati ule wa mapambano ya kisiasa Pemba, askari wa Zanzibar ilikuwa hawezi kunyoosha mkono kumuonyesha askari wa Bara wapi walikojificha wahalifu. ‘Nakwambia askari wa Zanzibar walikuwa wanaonyesha wahalifu kwa ulimi badala ya mikono. Nia ni kwamba wasionekane kuwa wao ndiyo waliowachongea wenzao’,’ anasema mwanasiasa mmoja.
Kauli kama hizi zinatisha. Napenda kuamini kuwa wapo askari mahiri kutoka Zanzibar wenye uwezo sawa na wale waliovuta ‘sigara ya Musoma’ au zaidi yao. Askari kuwa na macho ya kurembua haimfanyi asiwe na moyo wa uzalendo au ukakamavu wa kutoa amri. Hapa tatizo ni kutowapa nafasi, kwani wapo Wabara wengi wenye mwonekano huo na wana vyeo vya juu jeshini.
Tumefikaje hapa?
Kichwa cha makala haya kinasema ‘Unahitaji moyo wa mwendawazimu kumtetea Kikwete’. Chokochoko tunazozishuhudia leo ni matunda ya uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Dhana aliyoitumia ya kuwaacha watendaji na viongozi waliopo ndani ya Serikali yake kuumana kama senene au kugeuka sawa na kambare mdogo na mkubwa wote kuwa na sharubu, imeifikisha Serikali yetu hapo ilipo.
Akina Sitta walianza kidogo kidogo, tena mbele ya umma mchana kweupe, kwa kumshushua Rais Kikwete bungeni naye akawanyamazia. “Mheshimiwa Rais wewe ni mpole mno, hawa watu walete huku kwetu tuwashughulikie maana wamekushinda,” maneno haya ni ya Samuel Sitta wakati Kikwete alipokwenda bungeni kuhutubia Bunge.
Huu ulikuwa mshangao kwa wengi. Sitta alikuwa anawaambia wananchi kuwa Kikwete ni dhaifu. Hakuchukuliwa hatua wala kukemewa. Kama vile haitoshi, Sitta akiwa Mbeya akatamka kuwa Serikali inapaswa kuwaomba wananchi radhi kutokana na tatizo la umeme. Sitta akapingana hadharani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika suala la kisheria la Dowans, akidiriki hata kuitaja Serikali kama kichaka cha wahuni.
Kikwete akaendelea kumzawadia vyeo, akidhani kwa kufanya hivyo anamweka karibu kumpunguza makali kumbe anampa mipini. Leo kauli zilezile za Sitta zimeigwa na akina John Mnyika, Tundu Lisu na wengine lakini zinaonekana ni za kumdhalilisha Rais. Mimi nasema Rais alichagua kujidhalilisha mwenyewe alipoamua kutodhibiti kauli hizi, wananchi na wanasiasa wakaamini kuwa anazipenda na si muda mrefu asipoangalia zitasambaa kama wimbo wa taifa.
Sitanii, staili ya Kikwete kuongoza nchi inahitaji utafiti utakaoongozwa na Mwanafalsafa kama Plato. Yanatokea mambo makubwa yanayogusa hisia za wananchi, lakini anakaa kimya hadi nchi inachanwa vipande. Wakati wa migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu, ametoa kauli ya kufunga zizi wakati hadi ndama waliishapotelea porini.
Jipe muda, weka kando jazba za kisiasa na ujiulize; Kikwete na wasaidizi wake walivyolipangua suala la Richmond wakitumaini wanamrushia mzigo Edward Lowassa, leo Kikwete hajawahi kuwaambia Watanzania kama Lowassa alimsingizia kwenye kikao cha NEC au la.
Njoo kwenye mgomo wa madaktari. Zamu iliyopita alisubiri vijana hawa wakamdhalilisha hadi Waziri Mkuu wake, Mizengo Pinda, ndipo alipoliingilia. Hivi baada ya kukubali kutekeleza mambo matano kati ya 10, alishindwa nini kuwaita tena madaktari kule Ikulu kama alivyowaita awali kupoza mambo – wakazungumza na kukubaliana mwelekeo? Kipindi kilichopita mawaziri wamekuwa wakituhumiana bila yeye kutoa kauli na katika baraza jipya tunashuhudia wengine wakifitiniana bila yeye kuwakemea.
Kikundi cha Uamsho kinatamba Zanzibar kikitoa kauli zenye ishara za wazi ya kuvunja Muungano, lakini Kikwete hajitokezi kuwakemea. Eti jamani, hivi enzi za Mwalimu Julius Nyerere hawa Uamsho wasingekwishakemewa kama pepo mchafu na maji yakatulia baharini? Kikwete anasubiri waingie mitaani kuandamana ndipo atoe kauli za kuwaomba.
Sitanii, maswali mengi yanayoulizwa sasa yanahitaji majibu kutoka kwa Rais Kikwete. Marekani suala dogo tu Rais analitolea kauli, lakini sisi hoja ya deni la taifa kukua ghafla kutoka Sh trilioni 9 ndani ya miaka miwili na kufikia trilioni 22 Rais wetu yuko kimya! Mbona mzee Benjamin Mkapa alikuwa akitueleza tumefikia wapi katika kulipa madeni na deni letu likawa linashuka? Mkapa alilishusha hadi trilioni 5, leo Dk. Kikwete kalikuza hadi trilioni 22!
Jamani, nieleweni. Haya ni masuala ‘serious’. Watendaji waliopo chini yake wanalalamika. Leo tunayaona wazi matunda ya watendaji walioamua kuchapa kazi. Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakim Maswi, ameiwezesha Tanesco kupata mita 85,000 za luku. Fedha hizi zilikuwa wapi? Nehemia Mchechu kalibali Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) hadi tunafikiria kumwazima akafufue ATCL. Wako wapi watendaji wengine? Wanafanya nini?
Vuruguru hizi tunazoziona ameziasisi Kikwete. Niliwahi kuumuliza swali wakati tukiwa Ikulu kuwa haoni kama mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yanavunja Katiba ya Muungano? Yeye akasema: “Kama yamewapa amani na watu wanayapenda tuyaache.” Kauli hii haikuzingatia kuwa yeye ameapa kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ina maana hata Bukoba wakiamua kujitenga na kujenga Jamhuri ya Bukoba, basi Kikwete atasema kama inawapendeza waache waendelee!
Sitanii. Mwalimu Nyerere alikuwa kionambali. Kikwete sasa ameasisi ukabila kwa kuunda mikoa mipya. Mkoa kama Katavi una wilaya mbili tu. Kabila moja – Wafipa. Mkoa kama Geita umegeuka wa Wasukuma asilimia 100. Hata Wilaya kama Chato yenye Wasukuma ambayo Mwalimu Nyerere aliipeleka Kagera kwa makusudi kufuta ukabila, leo imerejeshwa Usukumani. Sitataja Simiyu. Tumerejesha ukabila kwa kuunda wilaya za ukoo.
Ukurasa unazidi kuwa mdogo. Ninayo mengi ya kusema ila navilia moyoni. Rais wetu simama. Waambie watendaji wachape kazi kama Mchechu, Maswi, Lowassa na Magufuli. Maendeleo hayatakuja kwa ngonjera ‘brother’. Tanzania tulipo si watu wa kuvaa suti. Yatupasa sote tununuliwe kombati.
Mwisho, nimalizie kama nilivyoanza kwamba Muungano wetu ni muhimu kuliko upungufu unaohusishwa nao. Ninapodai Serikali ya Tanganyika sidai kuvunjwa kwa Muungano. Nataka iwepo mizania sawa ili Zanzibar nao waone tofauti kati ya Serikali ya Muungano na utumishi katika Serikali ya Tanganyika. Tusikubali hata kidogo kuvunja Muungano.