Macho na masikio sasa yapo nchini Qatar wengi wakingoja kwa hamu na gamu kushuhudia michuano ya kombe la Dunia inayotarajiwa kuanza ifikapo Novemba 20, 2022

Kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia linafanyika Mashariki ya Kati, nchini Qatar 2022, Michuano hii inatarajiwa kuwa ya aina yake nap engine ya kwanza katika historia kwa kuwa na mambo mbalimbali ambayo hayakuwahi kushuhudiwa katika michuona uliopita.

 Na haya ni baadhi ya mambo mapya ambayo mashabiki wa soka watarajie kuyashuhudia michuano hiyo itakapoanza

Teknokojia ya kuotea

Sheria ya kuotea (offside) imekuwa ikileta  utata mara kwa mara, sasa katika kuondoa sintofahamu hiyo FIFA imeamua kutumia teknolojia ya kutambua kuotea (semi-automated offside technology) katika Kombe la Dunia la Qatar kwa mara ya kwanza.

Teknolojia ya Semi-automated offside ambayo itakuwa ndani ya mipira itakayotumika

 “Teknolojia ya kutambua kuotea ni mapinduzi ya mfumo wa VAR unaotumika kwa sasa katika nchi mbalimbali duniani,” anasema Rais wa Fifa, Gianni Infantino.

 Mfumo wa teknolojia ya kutambua kuotea unatumika na tayari umefanyiwa majaribio

kadhaa na kuonyesha ufanisi mkubwa katika mashindano ya Fifa Arab Cup 2021 na Kombe la Dunia la Klabu la Fifa.

Katika mashindano haya teknolojia hii mpya itakuwa ikiwasaidia waamuzi wanaokaa katika VAR kufanya uamuzi wa mipira ya kuotea kwa usahihi ndani ya muda mfupi.

Kubadili mwisho wachezaji watano

Utaratibu huu ulianza  kutumika baada ya janga la Corona kwa timu kufanya mabadiliko ya wachezaj watano kwa mechi moja badala ya watatu, itarasimishwa katika Kombe la Dunia Qatar uamuzi huu utakuwa ni faida kwa makocha, kwani wataweza kubadilisha wachezaji wengi wakati wa Kombe la Dunia.

 Wachezaji 26

Kufuatia kubadilika kwa sheria ya kubadilisha wachezaji watano kwa mechi moja, katika Kombe la Dunia hili timu zimepewa nafasi ya kuteua nyota 26 badala ya 23 iliyozoeleka huko nyuma. Hii ilianza kutumika katika mashindano ya Euro na Copa America wakati wa janga la Corona.

 Waamuzi wanawake

 Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia, mechi zake zitachezeshwa na waamuzi wanawake. Katika orodha ya waamuzi 36 watakaochezesha fainali hizo, watatu ni wanawake ambao ni Yamashita Yoshimi, Salima Mukansanga na Stephanie Frappart.

Yamashita Yoshimi mmoja wa waamuzi wanawake kombe la Dunia 2022
Salima Mukasanga mmoja wa waamuzi wanawake kombe la Dunia 2022
Stephanie Frappart Mmoja wa waamuzi wanawake kombe la Dunia 2022

Mbali ya hao kuna Neuza Back, Karen Diaz Medina na Kathryn Nesbitt ni majina ya wanawake watatu waliopenya katika orodha ya waamuzi wasaidizi 69 watakaochezesha fainali za Qatar.