Wiki iliyopita katika sehemu ya kwanza ya makala hii, nilinakili baadhi ya maandishi kutoka kijitabu ‘TUJISAHIHISHE’, kichoandikwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kuhusu unafsi unavyovunja madhumuni ya umoja wa kundi lolote la binadamu.

Shabaha za kunakili maandishi yale ni mbili. Mosi, kukumbushana baadhi ya mambo Mwalimu Nyerere aliyotuasa ikiwamo unafsi ambao ukiendekezwa utavunja madhumuni ya umoja wetu Watanzania.

Pili, nipate mtiririko, mserereko na vigingi kuwaeleza vijana wetu unafsi unavyovunja umoja wa kundi lolote na kuleta hali ya malumbano, ubabe na kuondoa hisani baina ya viongozi na viongozi, na baina ya viongozi na wananchi, na wananchi kufarakanishwa na Serikali yao, mambo ambayo si mazuri.

Tumeshuhudia mara kwa mara matatizo katika taasisi za Serikali, dini, vyama vya siasa na kwenye vikundi vya michezo na burudani kutokana na unafsi. Nafsi hii inataka iridhishwe katika jambo fulani na nafsi nyingine haitaki hivyo. Sababu zinazotolewa na pande mbili hizo hazishabihiani na hoja husika.

Mathalani, nafsi fulani inaposema ukweli kuhusu maslahi ya Taifa letu, nafsi ya pili itapinga kwa misingi ya wivu, kinyongo na pengine dharau. Huyu anayepinga, watu watamuunga mkono na kumpa chereko. Yule aliyesema ukweli atapuuzwa na kuchekwa.

Mwalimu Nyerere anatuasa, “Ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo; haujali adui wala rafiki. Kwake wote ni sawa. Pia ukweli unao tabia ya kujilipiza kisasi kama ukiupuuza. Ukiona nataka kupiga teke jiwe kwa kuwa nafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo lako kwa sababu sikupendi, nikalipiga teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi kupuuzwa puuzwa.”

Ni mara kadhaa Watanzania tumeshuhudia na wengine wamekumbwa na matatizo katika vyama vyao vya siasa, kumtaka fulani na kumkataa fulani kwa sababu hastahili. Wanachama wanaona ukweli, fulani anastahili. Lakini mkubwa mmoja kasema yule fulani hastahili, basi na wao wanasema hastahili. Wanaukana ukweli.

Mwalimu anatuasa, “Matakwa ya wachache hujulikana katika majadiliano na mazungumzo. Bila wale wachache kusema wazi wazi matakwa yao, majadiliano hayana maana. Wakati mwingine, hata baada ya majadiliano, wachache japo wanakubali kutii uamuzi wa wengi – wanaweza kuendelea kuamini kwamba mawazo yao ni sawa, na ya walio wengi yamepotoka. Demokrasi inawapa haki, na ukweli unawapa wajibu wa kuendeleza mawazo yao mpaka wengi waone kuwa ni ya kweli.”

Hebu chekecha matatizo yaliyotokea hivi karibuni kati ya viongozi wa siasa, michezo na baadhi ya viongozi wa dini walivyotoa fukuto na joto kali kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa sababu tu Mkuu wa Mkoa huo amekanyaga “mahala patakatifu pa watakatifu.” Kelele na misuto imemshukia. Loo salala!

Hali hiyo imeleta myumbisho katika dhamira ya Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, myumbisho uliowagawa watu katika makundi mawili yanayokinzana juu ya utendaji kazi wa mkuu huyo; wenye uzuri na ubaya hata kufukua mambo yake binafsi ya elimu na maisha.

Mwalimu anatuasa, “Mungu ametupa akili ili tuweze kuzitumia kwa manufaa yetu na ya jumuiya. Makosa niliyoyataja, na mengine mengi ambayo kila mtu aweza kuyafikiri mwenyewe, huzinyima akili huru wa kufanya kazi yake baranara. Huwa kama na kutu inayokizuia chombo kufanya kazi vizuri, au kama uchafu unachokizuia kioo kuona vizuri.

“Ni wajibu wetu kujitahidi kadiri iwezekanavyo kuzipa akili zetu uhuru wa kufanya kazi bila kutu na uchafu wa aina nilioutaja.

“Kipofu akinivamia na kuniumiza, nikakasirika kwa sababu ya maumivu aliyonitia, ni jambo la kibinadamu. Lakini nikijitoboa macho ili na mimi nimvamie na kumuumiza, haitakuwa nimefanya jambo la busara.”

Narudia kusema nimenakili baadhi ya maandishi ya Mwalimu Nyerere, kwa nia ya kukumbushana Watanzania na kuwafahamisha vijana nafsi inavyoweza kuvunja madhumuni ya watu katika umoja wao. 

Kuna masuala mengi wakati huu, lazima tuyatazame na kuyapima kwa kina, kabla ya kuyasema na kuyatenda. Ifahamike kuwa unapokazia jambo la mwenzako, Mwenyezi Mungu atakazia la kwako.