Kutofautiana kimtazamo na mtu ambaye amekuwa mwajiri, kaka na rafiki yako, ni jambo linalohitaji roho ngumu.
Lakini kwa kuwa tuko kwenye uwanja wa watani wa jadi, naomba leo nitofautiane kidogo na kaka yangu Rostam Aziz. Kabla ya kufanya hivyo, nitangaze masilahi mapema kwamba mimi ni mpenzi mtiifu wa Klabu ya Simba.
Komredi Rostam ametamka bayana kuwa yeye ni Yanga kindakindaki. Amekuwa mpenzi wa klabu hiyo kitambo – tangu akiwa darasa la kwanza.
Kwa namna ya uchokozi kwa watani zake, amesema anapinga vikali timu hiyo kumilikiwa na mtu mmoja! Hapa ametulenga Wana Msimbazi. Akaona maneno hayo hawezi kukaa nayo moyoni. Akawaita waandishi wa habari awaeleze akiamini yatatufikia sote, nikiwamo mimi!
Naomba ninukuu maneno yake: “Si sahihi hata kidogo mtu mmoja tu eti ndiye amiliki klabu kubwa kama Yanga. Hapana. Hata ufadhili ni njia ya mtu mmoja kumiliki klabu kwa mlango wa nyuma. Mimi nitaendelea kuisaidia klabu kama mwanachama na shabiki. Kikubwa ni namna ya uongozi kufanya mambo yaliyo sahihi lakini si kumilikisha klabu kubwa kama hii kwa mtu mmoja. Yanga inaweza kuingiza pesa nyingi sana kupitia udhamini, matangazo ya runinga na kadhalika, lakini pia kupitia suala la kuuza bidhaa zake kama jezi.”
Komredi Rostam ametoa maneno haya kipindi ambacho tayari amekwishamwaga mamilioni ndani ya klabu yake. Ametoa kauli hii kipindi ambacho Simba ni gumzo ndani na nje ya Afrika. Inameremeta mafanikio. Ameyazungumza haya akitambua wazi kuwa Simba sasa ina mwanachama aliyeona mbali na akaamua kuwekeza kwa kununua asilimia 49 ya hisa za klabu ili aongeze nguvu ya kuleta mafanikio.
Komredi Rostam kwa kutambua kuwa kauli yake ina maswali mengi, akafanya makusudi, akaacha kutualika kwenye mkutano wake wa waandishi wa habari. Sina hakika kama aliowaalika walimuuliza Yanga iliyoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1930 imepata mafanikio gani kwa mfumo anaotaka uendelee!
Hakutualika kwa kuwa alijua tutamuuliza ataje mifano ya walau klabu mbili duniani ambazo zimepata mafanikio makubwa kabisa kwa kuendelea kuwa na vikongwe na ajuza ambao kazi yao ni kusema: “Baba ndiye aliyetoa uwanja, mjomba alikuwa na kadi namba mbili, sisi ndio tumepigania uhuru, na kadhalika.” Anajua hazipo.
Kwa maneno mengine, Komredi Rostam anataka Yanga iendelee na mfumo wa analojia ilhali ulimwengu mzima ukiendesha klabu kisasa zaidi. Au anataka Yanga iendelee kukinga bakuli?
Mwekezaji Simba ana hisa asilimia 49; na yeye kama mtaalamu wa uchumi anajua idadi hiyo ya asilimia haimpi uhalali wowote mwekezaji kuwa ndiye mmiliki. Wapo wanaomiliki asilimia 100, lakini hizi 49 tu zinawakosesha watu usingizi.
Nchi yetu ‘ilikuwa’ ya Kijamaa. Tuliendesha mambo kijamaa kwa kuamini kuwa kila kitu kiwe cha wote. Hilo linawezekana kwa mambo mengine, lakini kwenye soka suala muhimu ni furaha ya wapenzi na wanachama inayotokana na mafanikio ya klabu. Tupo mashabiki wengi wa timu za Ulaya. Hatupati gawio lolote, lakini faraja yetu ni pale Man U, Arsenal, Liverpool, Barcelona au Real Madrid zinaposhinda. Vivyo hivyo, malipo na furaha ya wapenzi na mashabiki wa Simba ni pale ambapo timu yao inapofanya vizuri. Hilo ndilo kusudio la kwanza. Nani wa kutupa hiyo raha? Ni kina Kilomoni? Hapana.
Msimamo wa Komredi Rostam ukiachwa upite kama baadhi yetu wanavyojitahidi kufanya, soka la Tanzania litabaki hili hili la kuamini ushirikina kama njia ya kuleta mafanikio, badala ya kuamini kuwa mafanikio yanatokana na uwekezaji, mazoezi, nidhamu na umoja wa wapenzi na wanachama.
Tangu mwaka 1935 Simba imetumia mfumo unaopigiwa debe na kaka yangu Rostam na matokeo yake yamekuwa mabaya japo kwenye rekodi za kimataifa Simba iko mbali sana ikilinganishwa na watani zetu Yanga. Kwa miaka karibu 90 sasa Yanga kwa kuutumia mfumo huu wameendelea kuwa taabani kimafanikio.
Wameendelea kuamini ushindi ni kuishinda Simba tu. Tafakuri yao imegotea Msimbazi, na ikivuka basi inafika kwa Mbao United. Mtu yeyote anayetaka mabadiliko chanya akiona mambo hayaendi vizuri hubadili mbinu. Simba wameliona hilo. Wamebadilika. Yanga nao walikuwa na watu makini waliotaka kuanzisha kampuni, lakini mizengwe ikawaangusha. Wakalemewa na vikongwe na ajuza wasio na ujuzi wowote wa soka isipokuwa kuamini safari za Mlingotini.
Klabu za Ulaya zilikuwa kwenye usingizi kama wetu, lakini zikafanya mapinduzi makubwa kwa kukaribisha uwekezaji. Yameuzwa mashirika ya umma kwa sababu kama hizi za Simba na Yanga. Kama mashirika ya nchi yameuzwa na sasa yanatengeneza faida, seuze klabu? Yaani yote haya hayatupi mwanga wa mambo yanayopaswa kuendeshwa katika ulimwengu wa leo?
Leo Arsenal, Liverpool, Man U na klabu kubwa zote barani Ulaya zinamilikiwa na matajiri. Klabu hizo ndizo zinazotamba katika sayari hii. Hazitambi kwa bahati mbaya, kwa imani za kishirikina, kwa upendeleo au kwa miujiza, la hasha! Zinatamba kwa sababu zina wawekezaji na mifumo ya kisasa ya kuziendesha.
Kwa kuwa Wana Simba hatujamuomba ushauri, ni vizuri Komredi Rostam akaendelea kusisitiza mawazo hayo katika Klabu ya Yanga ili mwishowe tukikaa tupime kina nani wamefaulu, kina nani waliofeli!
Anaweza kumchukua mzee Kilomoni wakafanya hayo wanayokusudia kuyafanya [maana wana mtazamo mmoja] na mwishowe matokeo ya uwanjani yawe ndiyo hukumu.
Mwisho, nimuombe Komredi Rostam kama watu wanaweza kufunga safari kwenda ng’ambo kujifunza mafanikio ya wengine, na kama kweli amenuia kuisaidia Yanga, basi afike Simba walau apate mawili au matatu atakayotumia kuijenga Yanga mpya. Vinginevyo Simba na Yanga [zinazofanana] zitakuwa vitu viwili tofauti miaka si mingi; kama Tanzania ilivyofanana na Korea Kusini miaka ya 1960; na ilivyo tofauti kubwa kati ya mataifa haya mawili kwa mwaka huu wa 2019. Hakuna kisichobadilika, isipokuwa mabadiliko pekee. Kwa kuwa ninamheshimu sana kaka yangu Rostam, basi niwaombe Simba tumsamehe, na tumuombe aachane na unabii wa mzee Kilomoni. Tubadili soka la Tanzania.