Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeombwa kuitisha mkutano wa dharura  kujadili hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump  kuuhamisha Ubalozi wa Marekani kutoka Telaviv hadi Jerusalem.

Maamuzi hayo yalisababisha maandamano makubwa yaliyosababisha watu 17 kujeruhiwa kwa risasi na jeshi la Israel wakati Wapalestina walipoandamana katika Ukingo wa Magharibi na ukanda wa Gaza.

Lengo kuu la maandamano hayo ilikuwa ni  kupinga tamko la Rais  Donald Trump ya  kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel hali iliyozua taharuki katika nchi nyingi za kiislamu Duniani kote.

Hali ilikuwa mbaya zaidi katika miji ya ukingo wa Mgharibi ya Hebron na Al Bireh ambako  maelfu ya waandamanaji walijitokeza huku wakisema kwa sauti kwamba Jerusalem ni mji mkuu wa Palestina.

 Upande wa ukanda wa Gaza nako waandamanaji walikusanyika karibu na mpaka wa Israel huku  wakiwarushia mawe wanajeshi na waandamanaji wawili walijeruhiwa huku mmoja akiwa katika hali mbaya.

Wakati hali ikiwa hivyo Mamlaka ya Palestina ilitoa  tangazo la harakati za mapambano ya intifada kupinga tangazo la Rais Trump ya kuitambua rasmi Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kusababisha mtafaruku.

Taifa hilo linahitaji mji mkuu wa taifa lao huru kuwa upande wa Mashariki  eneo lililonyakuliwa kwa mabavu na Israel tangia mwaka  1967 wakati wa vita vya Mashariki ya kati na kuliunganisha eneo la Jerusalem na Israel.

 Waziri wa mambo ya  nje wa Marekani Rex Tillerson ameutetea uamuzi wa Rais Trump kwa kusema  kuwa kiongozi huyo  amezingatia  matakwa ya raia wa Marekani katika uamuzi wake na hapashwi kulaumiwa.

Amesema Rais Trump ametoa maamuzi hayo kwa kuzingatia manufaa mapana ya taifa hilo dunia nzima kwa jumla hivyo hapaswi kulaumiwa yeye kama yeye lakini kinachotakiwa ni uwepo wa usala’ amesema Tillerson.

 Mmoja wa maafisa wa  Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema uamuzi wa Marekani unatia wasiwasi na huenda ukalirejesha eneo la Mashariki ya kati kizani na kuongeza kuwa hali ya Jerusalem inapaswa kuamuliwa na mataifa ya Israel na Palestina.

“Umoja wa Ulaya nayo  ina nafasi ya wazi kabisa na ya pamoja kutafuta  suluhu ya kweli dhiidi  ya mgogoro kati ya Israel na Palestina kinachotakiwa ni uwepo wa heshima dhidi ya pande zote mbili husika” amesema Mogherini.

Wakati wa hali ikiwa hivyo msemaji wa Serikali ya Urusi Dmitry Peskov, imesema uamuzi wa Trump umeifanya hali kuwa ngumu zaidi Mashariki ya kati na kusababisha mgawanyiko katika jamii ya Kimataifa.

 Waziri Mkuu wa Malaysia Najib Razak amewatolea wito waislamu kote duniani kupinga tamko la Trump la kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kusema kuwa Dunia ya kiislamu inapaswa kupaza sauti kulipinga hili.

“Waislamu wote Duniani tunapaswa kusimama wote kwa pamoja kupaza sauti zetu kulaani maamuzi haya ya Rais Trump yanayolenga kuikandamiza na kudhulumu haki za waislamu waliopo katika eneo hilo”amesema Razak.

  Wakati hali ikiwa hivyo nchi za Uswisi, Uingereza, Ufaransa, Bolivia, Misri, Italia, Senegal, na Uruguay  zimetoa wito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuitisha mkutano wa dharura wa baraza hilo kulishugulikia jambo hilo.