Umoja wa Mataifa (UN) umezitaka mamlaka za
kisheria nchini Uganda kuitisha uchunguzi huru
dhidi ya machafuko yaliyotokea nchini humo na
kusababisha kukamatwa na kuteswa kwa wabunge,
akiwemo nyota wa zamani wa muziki, Robert
Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.
Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu wa
umoja huo, Zeid Ra’ad Al Hussein, ametoa wito kwa
serikali ya Rais Yoweri Museveni kuhakikisha
inafanya uchunguzi huru kuhusu madai ya mauaji
ya makusudi, matumizi ya nguvu kupita kiasi na
mateso yaliyofanywa na Jeshi la Polisi.
Amesema umoja huo una wasiwasi juu ya tuhuma
dhidi ya vikosi vya usalama vilivyo watesa na
kuwatendea vibaya mahabusu na kuongeza kuwa
umoja huo umepokea taarifa za namna mauaji
yaliyotokana na ukamataji wa ovyo wa raia wakati
wa maandamano.
Amesema taarifa zilizoufikia umoja huo
zinaonyesha matukio yalivyotokea nchini humo
tangu yalipoanza kujiri kuanzia Agosti 13,
mwaka huu hadi ilipofikia hatua ya baadhi ya watu
kukamatwa, kupigwa na wengine kuuawa kikatili na
vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo.
Amesema kitendo cha dereva wa Mbunge
Kyagulanyi kuuawa na Jeshi la Polisi akiwa kwenye
maegesho ya magari mjini Arua kisha
kumkamata akiwa na wenzie watatu walipokuwa
kwenye chumba cha hoteli ni ukatili usioweza
kuvumiliwa na ulimwengu wa wapenda amani na
unatakiwa kukemewa.
Amesema taarifa kutoka ofisi ya Haki za Binadamu
ya umoja huo zinasema wakati wa ghasia nchini
humo kuna watu zaidi ya wanne walipoteza maisha
na wengine 28 kukamatwa, wakiwemo waandishi
wawili wa habari na kina mama wawili huku taarifa
nyingine zikisema huenda kuna maafa mengi zaidi.
Bobi Wine augua figo
Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa kutoka nchini humo
zinasema mbunge huyo ana tatizo la figo ambalo
linahitaji kushughulikiwa kwa haraka nje ya nchi,
hiyo ni kwa mujibu wa wakili wake ambaye
alizungumza na waandishi wa habari siku mbili
baada ya mwanasiasa huyo kuachiwa kwa
dhamana.
Wakili Medard Sseggona ameliambia Shirika la
Habari la AP kwamba ripoti ya daktari huru
inaonyesha kuwa mteja wake anasumbuliwa
na maradhi ya figo. Taarifa zaidi zinasema kuwa
akiwa mikononi mwa vyombo vya dola mbunge
huyo alipigwa na kuvunjwa mbavu pamoja na
kuvutwa uume wake.
Tangu achaguliwe kuwa mbunge mwaka jana, Bobi
Wine amejipatia umaaarufu mkubwa ndani na nje
ya nchi kwa kuwapigia kampeni wagombea wa
upinzani ambao kila mara hushinda kutokana na
uwezo wake mkubwa wa kupambana na Rais
Museveni, mmoja wa marais wa muda mrefu barani
Afrika.
Mwisho