Jopo la wataalamu lililoundwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limewasili nchini Sudan kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa na Jeshi la wanamgambo wa (RSF) katika eneo la magharibi la Darfur.

Timu hiyo iliwasili katika mji wa mashariki wa Port Sudan jumapili wiki hii kwa ziara ya kwanza tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo Aprili 2023.

Jopo hilo limepanga kukutana na wajumbe wa Baraza Kuu linaloongozwa na jeshi na kamati inayofuatilia utekelezwaji wa vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa vilivyowekwa huko Darfur mwaka 2005.

Mnamo tarehe 8 Novemba, UNSC iliweka marufuku ya kusafiri na kufungia mali kwa makamanda wawili wakuu wa RSF kwa madai ya kuiyumbisha Sudan kupitia vurugu na ukiukaji wa haki za binadamu.

Vilikuwa vikwazo vya kwanza vya Umoja wa Mataifa katika vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Wakati huo huo, RSF imelishutumu jeshi la Sudan kwa kufanya mauaji katika majimbo ya Darfur Kaskazini na Darfur Kusini 9 Novemba hadi 10 Novemba, ikiwa ni pamoja na kuua zaidi ya watu 120 katika mashambulizi ya anga.