Tangu zamani watu wamekuwa wakitumia shairi au wimbo kufikishiana taarifa inayohusu kitu fulani. Pia shairi au wimbo umetumika kama hifadhi ya maarifa, hekima na sifa ya mtu maarufu.
Wasanii wa muziki, watunzi na waghani wa mashairi na ngonjera, waandishi wa vitabu na habari, wanatumia shairi au wimbo kufikisha ujumbe fulani kwa jamii. Ushuhuda wa mambo haya unapatikana katika historia, hadithi na simulizi za wahenga.
Watanzania tunatumia shairi au wimbo kufikishiana habari ya msiba, sherehe, kazi, siasa na kadhalika. Tungo hizi zinajaa maneno ya hekima ambayo yameandaliwa kwa ustadi kutoa maana pana na makini kwa msikilizaji na mtumiaji. Ukweli hizi ni njia muhimu za kufikisha ujumbe haraka sana.
Leo natumia nyimbo mbili za wasanii wa kikundi cha taarabu cha Black Star kutoka mkoani Tanga ambacho kilishakufa. Wimbo ‘Jongoo Acha Makuu’ utunzi wake Ali Salim (Jinamizi) na ‘Bunduki Bila Risasi’ uliotungwa na Kibwana Saidi. Nyimbo zote zimeimbwa na Tatu Saidi (Shakila). Wasanii wote hawa ni marehemu.
Wimbo:
Ulipokuwa ukipanda, nimeyasifu maguu,
Utakako ulikwenda, kwa mchana na usiku,
Mbona leo wakushinda, kupanda mtungi huu.
Jongoo acha makuu, kuchota maji ni kazi.
Ni mengi uliyatenda, tena shafuu shafuu,
Tena kuparamia vibanda, milima na vichuguu,
Mbona leo wakushinda, kupanda mtungi huu,
Jongoo acha makuu, kuchota maji ni kazi.
Ulikuwa ukifyonza, maembe na zambarau,
Tunda ulipolipata, Mungu ulimsahau,
Nimedhani umeganda, na kumbe u-juu juu,
Jongoo acha makuu, kuchota maji ni kazi.
Mtunzi Ali Salim, anataja chombo mtungi na kiumbe jongoo. Mtungi na jongoo ni vielelezo kutoa fasili ya ujumbe. Ni fumbo. Salim amekusudia kuelezea tabia ya mtu fulani. Hii ni hisia yangu. Mantiki inakuwaje jongoo kushindwa kupanda mtungi ilhali ni hodari kuparamia vibanda, milima na vichuguu?
Wimbo unabembea maeneo ya mapenzi, kazi hata maeneo ya siasa. Kwa mujibu wa wimbo si busara mtu kujinasifu ni hodari kutenda mambo. Kila mtu anafanya jambo kwa uwezo alionao na kufika ukomo wa jambo. Mtunzi anatufahamisha tuache tabia ya kujiona tunaweza kufanya kila jambo.
Mtunzi mwingine ni Kibwana Saidi. Katika wimbo ‘Bunduki Bila Risasi’ anasema maneno yafuatayo:
Bunduki naidadisi, mliopo sikizeni,
Haya si kama nahisi, ya kweli yashikeni,
Bunduki bila risasi, yaua namna gani?
Yaua namna gani, bunduki bila risasi?
Bunduki yajulikana, kama chombo cha thamani,
Na kuwinda yatakana, muwe na risasi ndani,
Lakini mwako hamna, atakaye hofu nani?
Yaua namna gani, bunduki bila risasi?
Somo acha utukutu, msitu kuuchezea,
Hivyo si vema mwenzetu, mabaya kujitakia,
Bunduki isiyo kitu, huwezi kujivunia,
Yaua namna gani, bunduki bila risasi?
Ni fumbo jingine linalobembea maeneo yale yale. Mtunzi anatumia bunduki na risasi kuelezea hisia zake kwa jamii. Ili bunduki ijeruhi au kuua ni lazima iwe na risasi ndani. Binadamu hapaswi kujisifu anapofanya jambo na kujigamba anao uwezo na nguvu.
Ni mila na desturi kwa watu waungwana kufanya jambo na kuwaachia watu waseme na kusifu. Ni kweli pia watu hawatakuogopa na kukuheshimu iwapo hauna uwezo na nguvu.
Watanzania wenzangu, nyimbo hizi zimetufikishia ujumbe unaoasa baadhi yetu tusiwe na tabia ya kujisifu kwa watu, tukiwa hatuna uwezo na nguvu katika kulitaka au kulitenda jambo. Maneno si matendo. Tuwaache wenye dhamiri, uwezo na nguvu kuleta mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo nchini. Tafakari!