“Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja” Hii ni ahadi ya kwanza ya mwana- TANU, kati ya kumi ambazo alizitii na kuzitimiza enzi za uanachama wake. Ukweli ahadi tisa zote zimebeba neno zuri na tamu katika kulitamka, nalo ni NDUGU ingawa halikuwekwa bayana katika maandishi yote ya ahadi hizo.
Kwa mfano ahadi ya pili inasema, “Nitatumikia Nchi yangu na watu wake wote” ….watu wake …inatoa mkazo wa ndugu kuwatumikia. Ahadi ya saba inasema, “Nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu.” …wenzangu wote…inahimiza ndugu.
Kadhalika ahadi ya kumi inasema, “Nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.” …..Rais na Serikali ya Jamhuri…bado ina sisitiza watu kwa maana ya ndugu. Udugu huo ni muhimu katika kufanya jambo lolote la maendeleo.
Nimetoa mifano hiyo kutaka kuonesha wana – TANU walivyotambua na kukubali kwamba udugu unavyoweza kuunganisha watu wa aina tofauti na wa kutoka sehemu mbali mbali kwa madhumuni ya kujenga au kufanya jambo. Wenzetu walifuata misingi ya udugu na kuifanyia kazi, leo tunajivunia.
Kuna udugu unaotokana na imani ya dini (itikadi). Dini inawaunganisha watu kuwa wana dini na waumini wa dini moja kujuana na kuchukuana kama ndugu katika shughuli zao bila ya kujali uzawa, rangi, utaifa na kadhalika. Umoja huo huwapa ari na maarifa ya kutenda jambo bila hiyana. Amani.
Pili, kuna udugu wa kibinadamu ambao unatokana na maumbile ya kiutu na kuishi pamoja kijamii na kijirani.( watanzania, wakenya, waganda n.k.) Ndiyo maana wana- TANU wamesema kuwa binadamu wote ni ndugu zake na Afrika ni moja.
Tatu, tunapata udugu wa kinasaba; familia, kaka dada. ukoo mtoto wa ami, binamu mtoto wa mjomba, shangazi n.k. Wote hawa wana asili moja ya kuzaliwa. Si kwa sababu ya kufanya shughuli moja (siasa) au kwa ajili ya kujenga taifa moja kama vile la wasomali, warusi na kadhalika.
Udugu una thamani kubwa sana katika kuelewana na kufanya kazi za maendeleo pamoja. Udugu unajenga umoja na mshikamano. Unadumisha amani na utulivu. Unaleta ushirikuano kati ya jamii moja ya watu na nyingine ya watu. Unajenga heshima na kuleta uhusiano wa kiuchumi na kimataifa.
Wana – CCM ni ndugu, wana – CUF ni ndugu, wana- CHADEMA ni ndugu na wengine katika vyama vya siasa nchini ni ndugu. Udugu wao ni wa kiitikadi. Itikadi zao haziwaruhusu kujenga chuki na uhasama baina ya chama na chama. Soma katiba zao uangalie zinavyozungumzia udugu na ushirikuano na vyama vingine vya siasa.
Ndiyo maana wakati fulani wanasiasa makini na waadilifu wanashambuliana kiitikadi majukwaani pindi wanapoana chama kimoja kina kwenda kombo badala ya kujenga udugu wa kiitikadi na kibinadamu. Ukweli pia wanahofia udugu wa kinasaba kuvunjika na kupotea.
Hata viongozi wa dini katika mahubiri yao wanapotamka maneno yanayoshawishi waumini wao kudharau au kukejeli waumini wengine, ukweli wanavunja udugu wa imani (itikadi ) na kupanda mbegu ya chuki, ugomvi na dhuluma. Hatuhitaji mbegu hizo, tunahitaji udugu wa kiitikadi.
Viongozi wa serikali na watumishi wa umma wanaposema na kutenda vitendo vya kufisidi mali na miundombinu ya taifa kwa nia ya kuwaumiza wananchi, ni kuukataa udugu wa kibinadamu. Matokeo yake ni kuchochea fujo. Hatuhitaji machafuko, tunahitaji udugu wa kibinadamu.
Raia na wananchi tunahitaji sana amani na utulivu kwa sababu tuweze kudumisha umoja na udugu wetu, tuimarishe mshikamano wetu na tujenge uchumi wetu katika kufanya kazi. Yote hayo ni katika kupalilia udugu wa kiitikadi, kibinadamu na kinasaba. Vipi mwenzetu unafanya hiyana kwenye majukwaa, kwenye membari na kwenye mikutano ya ndani kusaliti udugu wetu?
Leo duniani kote nchi zilizovunja misingi ya udugu zinajuta na kutapatapa. Zinajaribu sana kurudisha misingi hiyo lakini wanapata vikwazo vya ajabu kutoka kwa hao waliowalaghai kuvunja misingi ya udugu. Nakusihi kiongozi na ndugu yangu kuacha chokochoko za kuvunja udugu kwani sote tutalia.
Kumbuka ahadi za mwana – TANU:
1. Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.
2. Nitatumikia Nchi yangu na watu wake wote.
3, Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga na magonjwa.
4. Rushwa ni adui wa haki; sitapokea au kutoa rushwa.
5, Cheo ni dhamana; sitatumia cheo changu au cha mtu mwingine kwa faida yangu.
6, Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote.
7. Nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu.
8. Nitasema kweli daima. Fitina kwangu mwiko.
9. Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU na raia mwena wa Tanzania na Afrika.
10. Nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.