UMOJA wa Ulaya umeituhumu Urusi kwa kutumia “gesi kama silaha” na kuanzisha vita vya kila upande nchini Moldova, ambako jimbo lililojitenga la Transnistria limekuwa halina gesi kutoka Urusi tangu tarehe Januari Mosi.

Kupitia ujumbe kwenye mtandao wa X hapo jana, mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisema Umoja huo unaendelea kuiunga mkono Moldova wakati huu ikikabiliwa na uchokozi wa Urusi.

Kallas alizungumza kwa simu na Waziri Mkuu wa Moldova, Dorin Recean, alisema nchi hiyo inapata msaada kupitia kuunganishwa na mitandao ya nishati ya Ulaya.

Soma zaidi: Ukraine yafunga mabomba ya gesi ya Urusi kwenda Ulaya

Jamhuri hiyo ndogo inayopakana na Ukraine imeshindwa kuwapatia wakaazi wake gesi wala maji moto tangu Mkesha wa Mwaka Mpya, baada ya kampuni ya nishati ya Urusi, Gazprom, kuizimia mabomba ya gesi kutokana na mzozo wa kifedha na serikali ya Moldova.

Siku hiyo hiyo, makubaliano ya kusafirisha gesi kati ya Ukraine na Urusi yalihitimishwa. Transnistria inatawaliwa na vikosi vinavyoiunga mkono Urusi ingawa kimataifa inatambuliwa kuwa sehemu ya Moldova.