Viongozi wa Umoja wa Ulaya walikutana mjini Brussels Alhamisi na kukubaliana kuongeza matumizi ya ulinzi kufikia mwaka 2030, huku wakiafikiana pia kuendelea kutoa msaada zaidi kwa Ukraine.
Katika mkutano huo wa kilele mjini Brussels Alhamisi jioni (20.03.2025), viongozi hao wa Umoja wa Ulaya walikubaliana kuchukua hatua zote muhimu ili kuimarisha utayari wao kiulinzi ifikapo mwaka 2030, huku juhudi hizo pia zikilenga kuongeza msaada waijeshi kwa Ukraine ambayo inaendelea kukabiliana na uvamizi wa Urusi.
Umoja huo unapanga kuongeza kasi ya matumizi yake kwenye sekta ya ulinzi, kwa kutenga euro bilioni 800 katika kipindi cha miaka minne ijayo, ikiwa ni pamoja na euro bilioni 150 za mikopo kwa ajili ya miradi ya manunuzi na utengenezaji wa silaha, fedha ambazo zinaweza kupatikana kutokana na mabadiliko ya sheria za ukomo wa kukopa kwa mataifa ya Umoja wa Ulaya katika suala zima la uwekezaji katika ulinzi.
Hatua hii ya kuongeza matumizi kwenye sekta ya ulinzi imechukuliwa huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka ndani ya Tume ya Ulaya kwamba ni lazima Umoja huo ujiandae kikamilifu na kwa haraka juu ya uwezekano wa migogoro mikubwa ijayo na Urusi.
Kulingana na waraka uliyowasilishwa kabla ya mkutano huo, tume ya Umoja wa Ulaya ilitahadharisha kwamba historia isingewasamehe viongozi wa Ulaya kwa kushindwa kwao kuchukua hatua ukisisitiza kuwa ikiwa Urusi itafanikisha azma yake nchini Ukraine, basi kuna uwezekano ifikapo mwaka 2030, Moscow ikaendeleza na matarajio yake ya kunyakua maeneo zaidi. Kauli iliyokuwa ikijirudia mara kadhaa ni kwamba Ulaya inapaswa kujizatiti vinginevyo itakuwa muhanga wa uvamizi wa Urusi.
