Na Mwandishi Wetu, JamahuriMedia ,Dodoma
Waziri wa afya Ummy Mwalimu amebainisha kuwa,katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madaktari bingwa katika baadhi ya hospitali za Rufaa za Mikoa, Wizara imelenga kugawa upya madaktari bingwa waliopo katika hospitali ili kukabiliana dhidi ya changamoto hiyo katika maeneo ya utoaji huduma.
Ummy amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akifafanua zaidi maswali atayoulizwa na Emmanuel Mwakasaka,katika mkutano wa kumi na moja kikao cha tisa.
“Hatua ya haraka ambayo tumeifanya, tumefanya tathimini ya madaktari bingwa, tumegundua baadhi ya hospitali za Rufaa za Mikoa kuna madaktari bingwa wengi kuliko baadhi ya hospitali nyingine, kwahiyo tunafanya ugawaji upya ili kukidhi mahitaji katika kila hospitali wakati tunasubiri walioenda kisoma” amesema Ummy.
Amesema kuwa, mwaka huu Wizara imepata kibali kipya cha ajira, hivyo imelenga kuajiri madaktari bingwa na kuwasambaza katika hospitali za Rufaa za Mikoa hasa zile zenye changamoto ya upungufu ili kukabiliana dhidi ya changamoto hiyo wa Wataalamu.
Aidha,Waziri Ummy amesema Serikali inaendelea na mkakati wa kusomesha Wataalamu kwa mfumo wa kujiendeleza katika fani za kibingwa na wanapomaliza wanarudi katika vituo vyao ili kuendelea na majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Amesema,Serikali ya Rais Samia imetenga zaidi ya Bilioni 8 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa “Samia Suluhu Super Specialists Programu” utaosomesha madaktari bingwa zaidi ya 400 ndani na nje ya nchi utaosomesha Wataalamu hao kwa muundo wa jumuhishi yaani daktari bingwa, muuguzi, mtu wa usingizi.
Nae, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akijibu juu ya uhaba wa madaktari bingwa katika hospitali ya Kitete Tabora amesema Wizara imepeleka kusoma jumla ya madaktari sita (6) kutoka hospitali hiyo ambao madaktari wawili (2) wanasomea ubingwa wa magonjwa ya ndani, daktari wa magonjwa ya Kinywa, Sikio na Koo mmoja (1), Ubingwa katika Mionzi 1, Ubingwa katika magonjwa ya dharura mmoja (1), na daktari bingwa wa Afya ya akina mama na uzazi mmoja (1).
Sambamba na hiyo, Dkt. Mollel amesema, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kitete hadi sasa ina jumla ya madaktari bingwa (5), ambapo daktari bingwa wa Afya ya akina mama na uzazi (1), madaktari bingwa wa watoto watatu (3) na Daktari bingwa wa upasuaji mmoja (1).