Kwanza, naomba nitangaze maslahi yangu kwenye makala hii. Nayo ni kwamba naamini Mungu yupo. Sijawahi kutilia shaka uwepo wa Muumba kwa sababu ni vigumu mno kuamini kuwa haya yote tunayoyashuhudia, kuanzia kwenye uumbaji, ni mambo yaliyojitokeza yenyewe tu! Haiwezekani. Mungu yupo.
Mungu ametujalia wanadamu maarifa na vipawa mbalimbali. Ni kwa sababu hiyo, kuna watu wenye huruma, ilhali wapo wengine ambao ni katili kweli kweli.
Naandika makala hii si kwa kuwakatisha tamaa waamini mbalimbali au kuonesha utovu kwa Muumba wetu, bali kwa kujaribu kuwashirikisha wasomaji wenzangu kuyatafakari haya yanayoendelea nchini mwetu na kwingine Afrika na sehemu mbalimbali duniani.
Dini, ukiacha maana yake njema ya kuwaandaa wanadamu kuishi maisha ya kidunia na ya ahera, inaweza kutumika kama njia ya kukwaza maendeleo ya wanadamu. Hapa ninaowalenga ni wale manabii na mitume ambao kwa kweli ni wa uongo tu.
Nahadharisha hili jambo kutokana na ukweli kwamba mwanadamu mwenye matatizo, hasa ya kiuchumi, ni rahisi sana kumbadili akili na hivyo kumfanya aamini au atumikie jambo ambalo si jema kwake.
Mathalani, nchini mwetu wapo waliotambua kuwa Watanzania hawawezi kufarakanishwa kwa ukabila, udini na aina nyingine za ubaguzi. Wanajua si rahisi sana kwa vijana wa Tanzania leo kuwatumia kwenye machafuko kama ilivyo kwa NRA kule nchini Uganda au kwa waasi wa M23 kule DRC.
Kwa maana hiyo, mbinu ya wao kunufaishwa na aina hiyo ya ‘mapato ya kivita’, wameona ni finyu ingawa kwa kweli hatupaswi kutopea kwenye imani hiyo kwa sababu wahenga walisema “hakuna kisichobadilika, isipokuwa mabadiliko yenyewe”.
Ni kwa maana hiyo sasa tunashuhudia mamia kwa mamia ya mitume na manabii wa uongo. Hawa wameamua kutumia njia hii isiyokuwa na maswali ya kodi, kujipatia ukwasi mkubwa sana.
Wameamua kutajirika kupitia kwa maelfu ya makabwela katika nchi yetu wenye kuamini kuwa sala za hao ‘mitume’ na ‘manabii’ zinatosha kabisa kuwaondoa kwenye lindi la umaskini.
Kama nilivyosema awali, kumbadili akili maskini hata aweze kuamini anachoambiwa si kazi ngumu hata kidogo. Ni kazi inayohitaji uwezo wa kushawishi kwa ghiliba, uwezo wa kutumia mazingaombwe na uwezo wa kutoa matumaini ambayo mtu mwenye akili isiyo na njaa hawezi kukubaliana nayo.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa uhuru kwa Watanzania kuabudu kadri wanavyotaka. Imetoa uhuru kwa watu wenye uwezo wa kuhubiri, kufanya hivyo iwe makanisani, kwenye misikiti na kadhalika.
Wataalamu wa kuchuma fedha wameona hawana sababu ya kutumia nguvu nyingi kujipatia fedha, kwa hiyo walichofanya ni kwenda kusajili makanisa yasiyo na idadi ili wayatumie kujipatia fedha.
Fedha wanazopata zina jasho la kwenye ‘madhabahu’ tu. Wanajua makanisani hakuna ofisa wa TRA anayekwenda kuwadai kodi kulingana na mapato ya sadaka wanazokusanya. Wanajua hawana michango wanayodaiwa na halmashauri za miji au majiji. Tena kabla ya Serikali kutoka usingizini, walitumia mwanya wa kuingiza magari na mali nyingine nchini bila kuzilipia kodi kwa kutumia mgongo wa ‘utumishi wa Bwana’. Mali nyingi sana ziliingizwa nchini kwa mbinu hiyo zikitajwa kuwa zinakwenda kuwasaidia ‘kondoo wa Bwana’, lakini ukweli ukawa kwamba zilipelekwa kwenye maduka na miradi ya hao ‘mitume’, ‘manabii’ na ‘watumishi’ matapeli.
Tofauti na fani nyingine kama udaktari ambazo huchunguzwa mara kwa mara ili kujiridhisha kuwa watoa huduma wana sifa, huku kwenye dini hakuna hilo. Mke na mme wanapanga, wanaanzisha kanisa; na wao hao hao ndio wanakuwa wamiliki wa mali zote, zikiwamo akaunti.
Tumeshuhudia mara kwa mara mke na mume wakitofautiana na hivyo mmoja kuamua kwenda kuanzisha kanisa lake.
Ndugu zangu, anayehubiriwa kwenye makanisa mengi sasa si Mungu, bali ni ‘mungu’. Mungu gani wa kweli ambaye atamtuma ‘mtumishi’ wake kuwapanga waumini kanisani kulingana na wingi au uzito wa sadaka wanazotoa? Mungu gani wa kweli anayeamuru wenye ukwasi waketi viti vya mbele wakikanyaga kwenye mazulia mazuri, na wale makabwela waketi mwisho kabisa?
Mungu gani anayemwagiza mtumishi wake ambariki muumini kulingana na ukubwa wa sadaka aliyotoa-kwa maana aliyetoa kikubwa anabarikiwa zaidi, aliyetoa kidogo anapokea baraka kidogo? Najiuliza, huyu ni Mungu kweli?
Ndugu zangu, naomba msikilize mahubiri ya ‘mitume’ na ‘manabii’ wengi. Karibu wote wanahubiri kuwapa utajiri waumini wao. Wengi wanajitangaza kwenye TV wakiwahimiza watu kwenda makanisani mwao kupokea uponyaji na utajiri! Nimemsikia mmoja akisema “Mungu hana agano na maskini”. Sipendi kuwa Tomaso, lakini itoshe tu kusema huu ni ulaghai wa hali ya juu.
Haya mambo ya kuaminisha watu kuwa kwa kuomba tu wanaweza kuwa matajiri, yanafificha juhudi za binadamu za kuondokana na umaskini.
Hivi karibuni tulishiriki msiba wa ndugu yetu aliyekufa kwa sababu tu ya mafundisho haya ya ajabu. Ndugu yetu alikuwa mgonjwa aliyesumbuliwa na kifua kikuu. Akaanza kutumia dawa hospitalini. Afya ikaanza kutengemaa. Mara ‘mtume’ akamwamuru anaache kutumia hizo dawa kwa sababu Mungu angemponya! Ndugu yetu akaziacha. Akadhoofu, na ndugu walipoamua kumpeleka hospitali akatibiwe, tukawa tumechelewa. Kweli kila mtu ana aina yake ya kifo, lakini kifo cha aina hii hatuwezi kusema kimetokana na ‘mapenzi ya Mungu!’
Tunafundishwa kuwa Yesu aliweza kuponya bila kutumia dawa, lakini si mara zote aliponya kwa maneno. Ndio maana kuna mahali watu walipobanwa njaa aliweza kuchukua samaki na mkate akavibariki na watu maelfu kwa maelfu wakaweza kula na kusaza.
Yohana 6: 3-15 tunasoma maneno haya:
3 Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. 4 Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. 5 Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula?
6 Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. 7 Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. 8 Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, 9 Yupo hapa mtoto, tuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? 10 Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. 11 Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. 12 Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. 13 Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. 14 Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. 15 Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.”
Hii maana yake ni nini? Maana yake bila shaka ni kwamba Yesu alikuwa na uwezo wa kutamka tu wale watu washibe, nao wakashiba; lakini aliamua kutumia samaki na mikate. Kwa maneno mengine si kosa kutumia dawa ambayo ndani yake nguvu ya Mungu iyapenya na kufanya kazi mwilini. Kuwazuia waumini kutumia dawa za miti shamba au za hospitalini ni kuwafanyia maangamizi.
Kule Kenya kuna ‘mitume na manabii’ wengi wanaotoa ushuhuda wa namna walivyoshiriki kuwaibia watu kupitia maombi ya uongo. Wametoa ushuhuda namna wanavyowaandaa ‘viwete’ ili waweze kutembea tena. Ukiwasikiliza na kutazama wanachofanywa, hakina tofauti na hapa Tanzania. Unajiuliza, kama kweli mtu anaweza kuponya kwa miujiza namna hii, iweje asiende Ocean Road, Muhimbili, Bugando, Mbeya, au katika hospitali yoyote nchini ambako kuna maelfu kwa maelfu ya wagonjwa wanataabika kwa maumivu makali? Wanasema kupona kunategemeana na imani, je, huko kote hakuna wenye imani?
Serikali yetu imetoa uhuru wa kuabudu kwa watu wote. Pamoja na ukweli huo, nadhani kuna haja ya kuyakagua baadhi ya makanisa ambayo yanaonekana dhahiri kabisa kuwa ni ya matapeli.
Narejea kusema namwamini Mungu wa kweli; Mungu asiye na upendeleo; Mungu asiyebagua matajiri na maskini, Mungu asiye wa sadaka kupitia M-pesa, Tigo-Pesa, Airtel Money, Easy Money, Halo Money wala aina nyingine za aina hiyo.
Mathayo 24:11 kunazungumzwa siku za mwisho. Neno la Mungu linasema: “ Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi.”