Ndoto ya miaka mingi ya viongozi waasisi wa Umoja wa Afrika (awali OAU na sasa AU) ya kuliona bara hili likishirikiana katika kila nyanja, si kwamba tu haijatimia, bali pia haionekani kutimia katika miaka 10 au 20 ijayo.
Ukweli huu wa kusikitisha unalifanya Bara la Afrika kuendelea kuwa duni na maskini ilhali likitajwa na tafiti zikidhihirisha kuwa lina rasilimali nyingi zinazohitajika sana katika maendeleo ya kiuchumi duniani.
Katika miaka 60 au 62 ya uhuru wa taifa moja moja, Afrika imekuwa ikishuhudia na kutawaliwa kwa nyakati tofauti na viongozi wa kila aina; wanamajumui wa Afrika, wapigania uhuru, wapambanaji, wazalendo, wanaharakati na hata madikteta wenye ubinafsi wa ajabu.
Aina hii ya uongozi na viongozi imekuwa ikikwamisha maendeleo ya Bara la Afrika; ikilikosesha dira na mwelekeo bara letu na hata kukosa msimamo mmoja katika majukwaa ya kimataifa yanayojumuisha mataifa yaliyoendelea.
Mara kadhaa viongozi wa Afrika wamekuwa wakiitwa kwa mabwana wakubwa Ulaya, Marekani na Asia kwenda kuzungumzia kile wanachokiona kuwa ni namna sahihi ya kuliendeleza bara hili, lakini viongozi wetu huwa hawana ajenda ya pamoja ya ‘Kiafrika’.
Katika siku za karibuni, nyota ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa iking’ara nje na ndani ya Afrika, na kwa hakika haikuwa ajabu alipotajwa kuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi duniani, na baadaye kupewa tuzo ya Babacar Ndiaye, ya usimamizi na ujenzi wa miundombinu.
Kwamba kwa sasa Rais Samia ni maarufu Afrika hili lipo wazi na ndiyo maana tunatamani kuuona umaarufu wake ukitumika kwa manufaa si ya Watanzania pekee, bali kwa Waafrika wote, akibeba dhamana aliyokuwa nayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Yale yaliyoelezwa jijini Accra, Ghana na wasaidizi wake kuhusu matamanio ya Tanzania kuyaunganisha kwa miundombinu imara mataifa ya maziwa makuu na Afrika Masharika na Kati, yanapaswa kupiganiwa na Rais Samia na Watanzania wote ili bara zima liwe na mtandao imara na wa uhakika wa miundombinu.
Kauli ya mmoja wa watu waliomzungumzia Rais Samia akikumbusha hotuba aliyoitoa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari jijini Arusha kuhusu umuhimu wa wahariri na waandishi wa habari wa Afrika kushiriki katika kuimarisha uchumi na umoja wa Afrika, iwe chachu kwetu sote.
Itukumbushe kuwa sasa kauli za Rais Samia zinasikika hadi nje ya Tanzania na wapo wanaotamani zifanyiwe kazi. Tuzo anazotunukiwa huku na kule zitumike kama jukwaa la kutawanya ajenda ya miaka mingi ya Tanzania; kuliona Bara la Afrika linakuwa moja.