Viongozi mbalimbali wa dunia wamehutubia mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa wakiutahadharisha ulimwengu kutokana na kuanza kutanuka kwa vita vya Mashariki ya Kati.
Mbali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres, Rais wa Marekani, Joe Biden, na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, takribani viongozi wote ambao wamekuwa wakizungumza tangu kufunguliwa kwa mkutano huu wa 79 wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne (Septemba 24) wamekuwa wakijielekeza kwenye mzozo huo wa Asia ya Magharibi ama Mashariki ya Kati kwa umaarufu wake.
Rais Luiz Inacio Lula da Silva, ambaye nchi yake huwa ya kwanza kuzungumza kutokana na utamaduni wa muda mrefu wa Umoja wa Mataifa, aliyakosowa mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza na Lebanon, akisma haki ya kujilinda imegeuka kuwa haki ya kisasi ambayo inazuwia ‘kufikiwa makubaliano ya kuachiliwa mateka na kusitisha mapigano’
Kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamin bin Hamad Al-Thani, ambaye nchi yake miongoni mwa waongozaji wa mazungumzo ya kusaka amani, aliishutumu moja kwa moja Israel kwa kuwa kizuizi cha mazungumzo ya kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza, akisema kwamba ‘hakuna mshirika amani’ ndani ya serikali ya Benjamin Netanyahu.
Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, alisema ingawa Israel ina haki ya kuwepo na kujilinda lakini sio kwa kusababisha mateso ya jumla jamala kwa raia wanaoishi kwenye maeneo yanayolengwa na jeshi lake.