Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi
Serikali imefafanua kwamba kazi ya ujenzi wa madaraja matano kwenye barabara Kuu ya Dar es Salaam – Lindi zilikuwa zinaendelea na haitaathiriwa na juhudi za sasa za kukarabati maeneo yaliyoharibiwa na mafuriko ya mvua katika siku za karibuni.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alitoa kauli hiyo juzi akiwa Somanga na Matandu mkoani Lindi ambapo anasimamia ukarabati wa dharura wa barabara iliyoharibiwa na mvua.
Ulega alitumia fursa hiyo kutangaza pia kwamba serikali tayari imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja ya kudumu na ni kazi endelevu hadi itakapokamilika.

“Tutambue kuwa ujenzi wa madaraja sio suala la wakati mmoja ni la hatua kwa hatua. Niwatoe hofu Watanzania kwamba toka ilipotokea dharura mwaka jana ya kukatika maeneo hayo Serikali imechukua hatua madhubuti na kila mahali yupo Mkandarasi anafanya wajibu wake”, amesisitiza Ulega.
Aidha, Ulega amewahakikishia Watanzania kuwa huduma za usafiri na usafirishaji kwa mikoa ya kusini zimerejea tangu alfajiri na zinaendelea kuimarika ambapo magari madogo, mabasi ya abiria na magari makubwa ya mizigo yanaendelea kupita katika eneo la Somanga na Matandu ili wananchi waweze kuendelea na safari.
Hata hivyo, Ulega ametoa wito kwa wananchi waliosimama kituo cha mabasi yaendayo mikoa ya Kusini cha Mbagala kutokana na hofu ya kushindwa kuvuka katika eneo la Somanga – Mtama kuendelea na safari kwani eneo hilo sasa ni salama na linapitika.
Ulega aliwashukuru wananchi wote waliokumbwa na changamoto hiyo kwa uvumilivu na subira pamoja na kuwapongeza Wakandarasi na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na Tanroads kwa kushiriki zoezi hilo usiku na mchana ili kuhakikisha mawasiliano yanarajea.

