Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema kuwa dhamira ya serikali ya awamu ya sita inaendelea kuunga mkono sekta ya Kuku kupitia miradi inayolenga vijana, ubunifu, na uendelevu.
Ameyasema hayo wakati wa mkutano wa Jukwaa la Tasnia ya Kuku na Ndege wafugwao ambapo Tanzania ni mwenyeji wa mkutano chini ya ufadhili wa Muungano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA).
Ulega amesema sekta ya kuku ina umuhimu katika kufanikisha usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi nchini.
“Takwimu zinaonesha kuwa ifikapo mwaka 2030 kuku watachangia asilimia 41 ya protini na asilimia 55 ya Kaya nchini na katika nchi mbalimbali ni ufugaji unaofanywa zaidi na wanawake na vijana na kuwa Tanzania ina kuku milioni 103.1 wakiwemo kuku wa asili na kisasa” amesema.
Aidha Waziri Ulega, ametoa wito kwa watafiti nchini washirikiane na Serikali wanapotoa matokeo ili kutoleta taharuki kwa jamii kupitia matokeo ya tafiti zao.
“Hivi karibuni watafiti walifanya utafiti kwa kutumia sampuli chache juu ya ulishaji wa kuku wanaofugwa na akina mama na vijana tafiti ile ilileta taharuki, kupitia Jukwaa hili nitumie fursa hii kuwaambia watafiti washirikiane na Wizara ili kutotoa taarifa za taharuki kwa jamii na kuwa Serikali inaweza kudhibiti wafugaji wasiofuata taratibu hivyo tusiharibu jitihada zinazofanywa na kukuza tasnia hii,” amesema na kuongeza:
“Tunawaheshimu na kuthamini kazi zao ila tuone wanapofanya tafiti na kupeleka kwa jamii tuwe na mkakati wa pamoja wa kufikisha tafiti hizo kwa jamii,” amesema Ulega.
Amefafanua kuwa, mkutano huo ni matokeo ya mkutano wa AGRA uliofanyika Dar es alaam na kuongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo AGRA walielezwa juu ya kuipa kipaumbele sekta ya ufugaji wa kuku kwa kuwa nchini Tanzania familia nyingi zinafuga kuku.
“ Tunawashukuru AGRA na Food Alliance kwa kutukubalia na ndio maana leo jukwaa la kwanza limefanyika nchini Tanzania na kutoa fursa kwa wafugaji wetu kujifunza na kujenga mahusiano,” alisema Ulega.
Kwa Upande wake , Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia na Mwenyekiti wa Bodi ya Muungano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA), Dkt. Hailemariam Dessalegn, alisema kuwa fursa muhimu zilizopo kupitia ufugaji wa kuku ni chanzo cha protini, soko la uhakika na ajira kwa vijana na kushiriki katika mnyororo wa thamani.
“Jukwaa hili linatoa fursa ya kujifunza faida na changamoto katika tasnia hii na kuongeza ushirikiano,Kukuza tasnia hii katika nchi yetu inahitaji majukwaa kama haya na inahitaji utayari wa wadau mbalimbali kwa kuwa wana uwezo wa kuwekeza ili kukuza tasnia hii,” amesema na kuongeza
“Tanzania ni kinara wa kuwa na njia shirikishi na ni imani yangu itaendelea hivi chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia ili kufikia ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), haswa dhamira ya kumaliza njaa na umasikini ifikapo 2030. Hakuna nchi inayoweza kufikia mafanikio haya peke yake hivyo sera ya ukanda, mafunzo na majadiliano na mawasiliano ni muhimu kufikia malengo,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Nchi wa AGRA Tanzania, Vianey Rweyendela, amesisitiza umuhimu wa sekta ya kuku kama sehemu ya mifumo ya chakula nchini.
“AGRA imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na wadau kuendeleza sekta hii yenye ahadi kubwa katika kuboresha lishe, kuongeza mapato ya kaya, na kukuza uchumi wa taifa,” amesema.
Jukwaa hilo limewakutanisha wadau muhimu, wakiwemo vijana, watunga sera, na viongozi wa sekta kutoka Kusini mwa Afrika, ili kujadili mustakabali wa sekta ya kuku na mchango wake katika kufanikisha usalama wa chakula.
Tukio hilo la siku mbili linalenga kuwawezesha vijana na kukuza ujumuishaji wa kijinsia kama sehemu muhimu za kuendeleza ufugaji wa kuku kikanda.
Wawakilishi kutoka nchi 23, zikiwemo Malawi, Botswana, Msumbiji, na Tanzania, walishiriki mawazo kuhusu ubunifu, uendelevu, na umuhimu wa ushirikiano katika kubadili sekta ya kuku kuwa yenye faida kibiashara.