Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Dar es Salaam

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mhandisi Balozi Aisha Amour, kuwasimamisha kazi wasimamizi wote wa Mizani waliokuwa zamu katika Mizani zilizopo katika barabara kuu ya T1 inayoanzia Dar es Salaam – Zambia kupitia mpaka wa Tunduma kwa ajili ya kupisha uchunguzi wa malalamiko katika Mizani hizo.

Ulega amefanya maamuzi hayo mara baada ya kadhia iliyojitokeza hivi karibuni kwa dereva Pamela James Bukumbi mwenye gari ya mizigo namba T 137 DLQ likiwa na tela T 567 CUR iliyotokea katika kituo cha mizani ya Vigwaza akilalamika kuhusu kutozwa faini ya kuzidisha uzito katika mizani hiyo wakati mizani nyingine alizopita gari yake haikuwa imezidisha uzito.

Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma leo tarehe 20 Machi, 2025 mara baada ya kupata taarifa hiyo na kusikiliza pande zote mbili kutoka kwa mlalamikaji na mlalamikiwa ambaye ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kubaini kuwa lipo tatizo la wazi ambalo limesababisha kadhia hiyo na kutoa maelekezo makuu matano.

“Baada ya kugundua liko tatizo, nimeamua kuchukua hatua zifuatazo moja ni kuwasimamisha wale wasimamizi wetu wa mizani wa hii T1 barabara nzima kuanzia Tunduma mpaka inafika pale Vigwaza waliokuwa kwenye zamu kwa siku ile wakati tukio linatokea”, amesema Ulega.

Ulega ameeleza kuwa amewasimamisha wasimamizi hao kwa lengo la kufanya uchunguzi ambapo tayari timu ya wataalam ya kuchunguza tukio hilo imeundwa ili kufuatilia safari nzima ya gari hilo ili kupata hali halisi na kuwasilisha mapendekezo mengine ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa dhidi ya wale wote ambao watabainika na vitendo visivyoridhisha.

Aidha, Waziri Ulega ameuagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kuanza hatua za kubadilisha mifumo ya uendeshaji wa mizani 78 zote nchini haraka iwezekanavyo kwa kutangaza kwa watoa huduma wenye nia kuja na teknolojia ambazo ni ‘automated’ ili kupunguza muingiliano baina ya watu na watu na hivyo kumuwezesha dereva kujihudumia kwa kutumia mifumo.

Aidha Ulega ameielekeza TANROADS kuhakikisha mifumo ya mizani zote inasomana kutoka mizani moja hadi nyingine ambapo jambo hilo limekuwa likisemwa na kusisitizwa mara kwa mara na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu mifumo katika Serikali kusomana na kuagiza utekelekezaji huo ufanyike haraka iwezekanavyo.

Ulega amewalekeza mameneja wote wa TANROADS nchini kuwa nambari moja katika usimamizi wa mizani zilizopo katika mikoa yao na sio kuwaachia wasimamizi peke yake na mizani zitakazolalamikiwa na mameneja husika pia watachukuliwa hatua.

“Kwa muda mrefu mameneja wamekuwa wakijiweka kando sana katika usimamizi wa mizani lakini hapo mbele tutaanza mara moja mizani zitakazokuwa zikilalamikiwa tutaanza kuwachukulia hatua na Mameneja na sio wasimamizi tu”, amesisitiza Ulega.

Vilevile, Ulega ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara ambayo kwa ujenzi wa kilometa moja unaigharimu Bilioni moja hadi mbili kutegemea mazingira ya eneo husika ambazo zinahusisha fedha za umma na hivyo kutoa rai kwa wananchi kuona umuhimu wa kuilinda rasilimali hiyo kwa kutokana na uwekezaji wake pamoja na usalama wa watumiaji wa miundombinu hiyo.