WAZIRI wa Ujenzi Abdallah Ulega ametoa miezi mitatu kwa Mkandarasi M/s China Railway 15 Bureau Group Cooperation anayejenga Barabara ya Nachingwea-Ruangwa-Nanganga (KM 106), kukamilisha ujenzi wa daraja la Lukuledi.
Agizo hilo amelitoa leo wakati akikagua Barabara na Madaraja katika barabara hiyo na kusisitiza kuwa fedha zipo hivyo ni wajibu wa mkandarasi kuongeza kasi ili wana Ruangwa na Nachingwea wanufaike na mradi huo.
” Mtendaji Mkuu wa TANROADS simamieni mradi huu ukamilike kwa wakati na ujengwe kwa ubora ili udumu kwa muda na kuwawezesha wananchi wa wilaya za Ruangwa na Nachingwea kunufaika kwa kuyafikia masoko ya mazao yao kwa urahisi”, amesema Waziri Ulega.
Amesema Ujenzi wa Barabara hiyo uendane na uwekaji taa za barabarani ili kuondoa giza na kuchochea ukuaji wa miji na hivyo kuwawezesha wananchi kufanya Biashara muda wote.
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza katika miradi hii vijana na wanawake wa maeneo inapopita miradi hii wapewe kipaumbele kwa kazi wanazoweza kuzifanya ili wanufaike kiuchumi”, amesisitiza Waziri Ulega.
Naye Msimamizi wa mradi huo kutoka TECU Mhandisi Simon Makala amesema jumla ya wenyeji wa eneo la Ruangwa 165 wamepewa ajira za muda mfupi kutokana na mradi huo na utaratibu huo ni endelevu kadri fursa zinavyojitokeza.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea ambaye pia ni Kaimu mkuu wa wilaya ya Ruangwa Mohamed Moyo amewataka wananchi kulinda miundombinu ya barabara na madaraja kwa kuepuka wizi wa alama za barabarani na uchimbaji mchanga pembezoni mwa barabara.
Barabara ya Nachingwea-Ruangwa-Nanganga Km 106 ni moja ya Barabara ya kimkakati ambayo katika kuharakisha ujenzi wake imegawanywa sehemu mbili Nachingwea-Ruangwa Km 57.6 na Ruangwa-Nanganga Km 53.2 ambapo kukamilika kwake kutafungua mtandao wa barabara mkoani Lindi na kuchochea uzalishaji wa mazao ya ufuta, mbaazi, korosho na alizeti na hivyo kukuza uchumi wa wananchi wa wilaya za Ruangwa na Nachingwea na kuimarisha sekta ya Usafirishaji na Uchukuzi mkoani Lindi.