Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Mhanga, amenunua gari maalumu lililotengenezwa mahsusi kwa vionjo alivyovitaka yeye kwa gharama ya Sh milioni 500.
Kiasi hicho cha fedha kama kingetumika kingelekezwa shuleni, kingeweza kutengeneza madawati 10,000 kwa gharama ya Sh 50,000 kwa kila dawati.
Kama kila dawati lingekaliwa na wanafunzi watatu, kwa idadi hiyo wanafunzi 30,000 wangenufaika. Kama kila shule ingekuwa na wanafunzi 2,000; kwa idadi hiyo ya madawati maana yake shule 15 za msingi kusingekuwa na mwanafunzi anayeketi chini.
Mhanga anafanya haya ilhali akiwa anahusishwa na Kampuni ya Hai Sub Suppliers iliyopendelewa kufanya kazi ya kutoa huduma za kushusha na kupakia mizigo melini katika Bandari hiyo.
Taarifa zinasema kampuni hiyo inayolipwa shilingi zaidi ya nusu bilioni kila mwezi, ndiyo inayompa jeuri ya kifedha ya kuagiza gari hilo la anasa aina ya Land Cruiser 200 V8.
Ingawa amekuwa akikana kuwa mshirika kwenye Kampuni ya Hai Sub Suppliers, taarifa zinaonesha kwamba Mhanga ana unasaba na kampuni hiyo iliyopewa asilimi 90 ya zabuni zote za kazi za utoaji na upakiaji mizigo bandarini hapo.
Taarifa zilizothibitishwa na Mhanga mwenyewe alipozungumza na JAMHURI Alhamisi iliyopita ni kwamba alilitoa gari hilo jipya kutoka yadi ya Alu-Usum iliyoko Barabara ya Mandela, Dar es Salaam.
“Kwani hiyo nayo ni habari?” Alihoji na kuongeza: “Jamani, jamani, jamani mambo mengine ni private (binafsi). Ni vema ikafika hatua tukazungumza issues (masuala), nami natoa ushiriano, lakini naona sasa hata haya ya binafsi.
“Lakini labda niseme hivi, nami nimshukuru mwajiri wangu. Maana ndiye aliyenikopesha fedha nikanunua usafiri huu,” amesema Mhanga.
Alipohojiwa mwajiri anawezaje kumkopesha Sh milioni 500 akanunua gari, akajibu: “Wewe usitake kujua bei. Ok, mimi kwa sasa niko msibani Iringa, nadhani nitarudi wikiendi hii, wewe jitahidi Jumatatu uje ofisini nikupe maelezo ya kina kuhusu hayo yote na mengine unayohitaji kuyajua.
“Mimi huwa natoa sana ushirikiano wa kuzungumza na waandishi wa habari, lakini nashangaa mnachopenda kuandika, kwani watu watapenda habari kama hizi? Nasubiri nione utakavyoandika.”
Hoja ya ufafanuzi ya kununua gari ilitokana na Gazeti la JAMHURI kutaka kuelezwa sababu za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kukata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa na Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma (PPAA).
Kwa namna isiyo ya kawaida, TPA imetumia gharama zake kukata rufaa Mahakama Kuu katika kesi ya madai inayohusu kampuni ya Hai Sub Suppliers inayotoa huduma za kushusha na kupakia mizigo bandarini.
Januari 19, mwaka huu PPAA ilitoa hukumu juu ya kesi iliyofunguliwa na kampuni za Nagla General Services Limited, Portable Enterprises Limited na Carnival Investment Limited zikipinga upendeleo unaovunja sheria kwa kuipatia zabuni Kampuni ya Hai Sub Suppliers wakisema ikiwa haina sifa.
Kwa kuwa Mhanga anatajwa kuwamo kwenye Hai Sub Supplier na Bandari ya Dar es Salaam iko chini yake, JAMHURI likamuomba kujua sababu zilizoifanya TPA itumie mapato yake kufungua kesi, kitu ambacho kingeweza kufanywa na kampuni hiyo yenyewe.
“Kukata rufaa ni masuala ya kisheria. Huo ni uamuzi na mtazamo wa mwanasheria wetu. Yeye ameona kuna haja na hoja ya kukataa rufaa,” anatetea Mhanga.
Mwanasheria wa TPA, Koku Kazaura alipotafutwa kwa muda wote bandarini, wasaidizi wake akiwamo mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jacqueline, alisema: “Mawakili wote wako mahakamani. Wana kesi nyingi huko.”
Mhanga alipoambiwa kwamba wanasheria hawajapatikana kuzungumzia hilo, alishutumu tu Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 inayowapa nafasi wazabuni walioshindwa kulalamika, akisema imezaa mvutano usio na ukomo kwa maana waliokosa zabuni hawakubali kushindwa.
Katika hatua nyingine, kuna taarifa kuwa kampuni ya Hai imepewa zabuni ya kufanya kazi kama hizo katika Bandari ya Mtwara. Mhanga anakataa kulizungumza suala hilo kwa undani kwa maelezo kuwa yeye si msemaji wa TPA.
Mtoa habari wetu anasema kilichoiangusha Kampuni ya Hai Sub Supplier katika Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma ni kukosa vigezo.
“Pia tender document ya Mtwara vigezo vyake ni sawa na vile vya Dar es Salaam Port (Bandari ya Dar es Salaam), iweje apewe Mtwara na kampuni haijakidhi vigezo?” Anahoji mtoa habari na kuongeza:
“Zabuni ya Mtwara nayo ichunguzwe. Upendeleo kwa hii kampuni umezidi sana na hii ni kwa maslahi ya wakubwa.”
Mhanga anakataa kuzungumzia Bandari ya Mtwara kwa kigezo kuwa Bandari hiyo ina menejimenti yake, lakini anasisitiza Hai Sub Suppliers walishinda kihalali na wamekuwa wakifanya nayo kazi tangu mwaka 2012.
Kwa kigezo cha muda mrefu, anashangaa kuona hawaitambui iliposajiliwa rasmi mwaka 2015.
Baada ya hukumu hiyo ya Januari 19, mwaka huu iliichukua TPA hadi Februari 17, mwaka huu kukata rufaa iliyosajiliwa kama shauri la madai Na. 6 la mwaka 2016 kuhusu uamuzi wa PPAA.
Katika hukumu ya PPAA, Bandari ya Dar es Salaam imetakiwa kusimamisha utoaji zabuni kwa kampuni ya Hai Sub Suppliers Limited kwa sababu haikuwa na uzoefu wa miaka miwili unaotakiwa kisheria.
Uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam umeendelea kuing’ang’ania Hai Sub Suppliers ikiwa ni taasisi ile ile kwani ilichofanya ni kujiondoa katika kufanya biashara na Bandari kama mtu binafsi (sole proprietor) iliyokuwa ikimilikiwa na Hidaya Amri na kugeuka kampuni Mei, mwaka jana.
Mwenendo wa kesi kortini
TPA imejitambulisha Mahakama Kuu kama mwombaji au mkata rufaa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu rufaa wa kwanza, na PPAA kama mjibu rufaa wa pili.
Kwa mujibu wa rufaa hiyo iliyosajiliwa Febrauri 18, mwaka huu Mahakama Kuu iliziita pande zote mbili za mkata rufaa na wajibu rufaa Februari 25, mwaka huu kwa mara ya kwanza.
Mahakama ilitoa taarifa ya nafasi ya Mahakama Kuu kutoa amri ya kimamlaka dhidi ya uamuzi wa PPAA katika hadhi ya kutoa uamuzi kisheria.
Pia Mahakama Kuu ilifafanua uwezo wa kutoa uamuzi wa wenye hadhi dhidi ya zabuni iliyotolewa na kuilinda kubaki hivyo hadi mwisho wa shauri lililofunguliwa mahakamani.
Aliyekula kiapo cha rufaa hiyo ni Mwanasheria wa TPA, Alex Seneu anayejitambulisha kuwa ni Ofisa wa Idara ya Sheria ya TPA, akitaka afahamike hivyo mbele ya Mahakama.
Anakiri kwamba TPA ilitangaza zabuni Na. AE/016/2012/DSM/NC/01B Septemba 10, mwaka jana na kuifungua Oktoba 6, mwaka huu ingawa gazeti la JAMHURI lina taarifa kwamba zabuni hiyo ilitangazwa mwaka 2013.
Mwanasheria huyo anaapa akisema watoa huduma 18 waliomba zabuni hiyo na walihudhuria hafla ya ufunguzi wa zabuni.
Katika sehemu ya sita, mla kiapo anasema mtoa zabuni alitia nia ya kutaka kumpa zabuni kwa mshindi aliyestahili. Tarehe iliyotangazwa ni ni Aprili 10, 2014 ilihali katika sehemu ya kiapo chake ameapa kuwa zabuni ilifunguliwa Oktoba 6, mwaka jana.
Anasema wakati wa kuthaminisha wazabuni, kampuni 16 zilionekana kutokuwa na sifa katika maeneo mbalimbali.
Bodi ya zabuni katika mkutano wake wa Novemba 10, mwaka jana iliridhia maoni ya kamati ya tathmini na hivyo kutoa zabuni kwa aliyestahili. Japo hataji, lakini ni Kampuni ya Hai Sub Suppliers.
Mwanasheria anaapa kwamba kati ya Novemba 25, mwaka jana na Desemba 4, mwaka jana baadhi ya waomba zabuni (walioshindwa) hawakuridhika na matokeo ndipo walipoomba ufafanuzi PPAA kuhusu uhalali wa Kampuni ya Hai Sub Suppliers kupewa zabuni.
Anasema kati ya Novemba 30, mwaka jana na Januari 4, mwaka huu wajibu rufaa walipokea malalamiko ya kupingwa kwa uamuzi wa kamati ya zabuni.
Kati ya Desemba 8, mwaka jana na Januari 4, mwaka huu, wakata rufaa- Kampuni za Nagla General Services Limited, Portable Enterprises Limited na Carnival Investment Limited walikata rufaa PPAA ambayo ilifikia uamuzi Januari 19, mwaka huu.
Kuona hivyo, TPA ikawasilisha nia yake ya kukataa rufaa Februari 2, mwaka huu na kuanza kusikilizwa na Jaji Munisi kuanzia Februari 5, 8, mwaka huu na pia ilisikilizwa Jumatano iliyopita.
Mtazamo wa wadau
Wadau wa biashara hiyo wanahoji: “Kampuni hii inapata nguvu wapi?”
Kupitia barua ya Machi 6, mwaka huu yenye kichwa cha habari kinachohusu zabuni kusogezwa mbele, TPA inasema zabuni zimesogezwa mbele hadi Aprili 30, mwaka huu.
Wadau wanaoomba zabuni hiyo wameagizwa kuandika barua ya kuthibitisha kusubiri kwani imeshindwa kukamilika kutokana na sababu zilizo nje ya TPA.
Imeelezwa kuwa kitendo cha TPA kukata rufaa katika shauri hilo ni mbinu za kusogeza mbele daawa hilo ili Kampuni ya Hai Sub Suppliers iendelee kuhodhi kazi za Bandari kwa asilimia 90 hata ikafika mwakani.
Hivyo, Kampuni ya Hai Sub Suppliers kwa sasa inaendelea kupewa kazi katika gati saba kati ya gati nane za Bandari ya Dar es Salaam; imepewa kazi za maghala saba kati ya manane; imepewa kazi ya usafi wa ofisi, usafi wa jumla, kushusha na kupakia mizigo kwenye malori na mabehewa.
Kampuni ya Portable Enterprise Limited imepewa kazi moja kwenye gati Na. 8 na Kampuni ya Freight Meridian imepewa kazi moja tu katika ghala Na 8. Mkataba wa awali wa Hai Sub Suppliers ulikuwa wa kupakua na kupakia magari kwenye meli.
Katika hali inayotia shaka, Kampuni ya Hai ilipata mkataba mnono wa kufanya kazi na taasisi kubwa kama Bandari bila kuwa na sifa stahiki.
Tangu mwaka 2012 ilipopewa mkataba wa kwanza, Hai Sub Suppliers- kumbukumbu zinaonesha haikuwa na Namba ya Mlipa Kodi (TIN) badala yake ilikuwa inatumia Na 102-303-229, ambayo ni namba ya mtu binafsi anayejulikana kwa jina la Hidaya Amri.
Kwa miaka yote kampuni ya Hai imekuwa ikifanya kazi kinyume cha sheria, na hakuna rekodi za ulipaji kodi.
Baada ya kuwapo fununu za kushitukiwa ujanja wao, ndipo Mei 22, mwaka ikiwa ni baada ya miaka mitano ya kufanya kazi bandarini, ndipo iliposajiliwa kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela). Mei 25 ilipata TIN namba 127-110-069 na ndipo ikaomba ipewe zabuni kubwa zaidi.
Maombi hayo yalifanikiwa katika kile kilichokuja kubainika baadaye kuwa ni kubebwa na baadhi ya wakubwa ndani na nje ya Bandari.
JAMHURI lilizungumza na mfanyakazi wa Bandari, ambaye ni mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Hai Sub Supplier, Yusufu Ibrahim, ambaye anamiliki asilimia 50 ya hisa za kampuni hiyo.
Alisema: “Ni kweli nilikuwa namiliki kampuni hii, lakini nimefilisika.”
Licha ya Ibrahim kudai amefilisika, hisa nyingine zilikuwa ni za mke wake, Hidaya Amri; hivyo kufanya jina la Kampuni kuitwa Hai kwa maana ya Hidaya Amri na Ibrahim (Hai Sub Suppliers).
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Hidaya ni mpwa wa aliyekuwa Mkurugenzi wa TPA, Ephraim Mgawe ambaye kwa sasa anashitakiwa katika Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kusaini mkataba na Kampuni ya Ujenzi ya China Communication Limited bila zabuni.
Mgawe ndiye aliyempandisha daraja Mhanga kutoka Meneja Bandari ya Kigoma na kumpeleka Bandari ya Dar es Salaam kushika nafasi anayoishikilia hadi sasa.
Mhanga alipohojiwa na JAMHURI kuwa analinda mtandao huo wenye undugu na kampuni ya Hai Sub Suppliers kuendelea kunufaika, alisema: “Mimi sijui chochote. Kuna watu wanafanyia kazi hayo. Natoa ushirikiano kwenu, lakini nahisi mnanionea tu.”
Mhanga alianza kukaimu nafasi hiyo Desemba, 2013 na kunyang’anya kazi kampuni nyingine Mei, mwaka jana na kutoa zabuni kwa Kampuni ya Hai Sub Suppliers.
Hai Sub Suppliers inalipwa malipo makubwa kuanzia Mei, 2015 kwa sababu ya kile kinachoelezwa uhusiano wa moja kwa moja na baadhi ya viongozi huku Mhanga akitajwa mara nyingi.
Wakati kampuni ya Hai ikipewa uendeshaji wa gati saba, kampuni mbili za Portable Enterprises na Freight Meridian zimepewa gati moja tu, yaani namba nane. Kwenye vigezo, JAMHURI limeambiwa kampuni hizo ndizo zenye sifa.
Taarifa zatua kwa Waziri Mkuu
Malalamiko ya wazabuni hao yamefikishwa kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa; na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.
Machi 29, mwaka huu Profesa Mbarawa alizuru tena bandarini na kuagiza uongozi wa Bandari kuchunguza kampuni zote zinazotoa huduma bandarini kuboresha utendaji na kuepuka mgongano wa maslahi miongoni wa watumishi wa Bandari.
Profesa Mbarawa alifanya ziara nyingine ya kushtukiza akizuru eneo la kupakulia mafuta yanayoingia nchini (KOJ) Kurasini na kusema: “Haiwezekani mfanyakazi wa Bandari akawa na kampuni inatoa huduma bandarini, hapo ni lazima kutakuwa na mgongano wa kimaslahi.”