*Malipo yafanywa kwenye benki za ughaibuni

*Akaunti kadhaa zabainika kufunguliwa Mauritius

*Tanzania yaambulia ‘kiduchu’, nyingi zaishia huko

*TRA, Wizara Maliasili hawana taarifa za wizi huo

DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Baadhi ya kampuni za uwindaji wa kitalii zinatuhumiwa kukwepa kodi ya mabilioni ya shilingi kwa kufanya udanganyifu mkubwa kwenye mapato yao.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini pasi na shaka kuwa ukwepaji kodi huo unafanywa na kampuni zenye wamiliki wengi raia wa kigeni, kupitia akaunti za benki zilizofunguliwa ughaibuni.

Mbinu kadhaa zinatumika kwenye ‘mchezo’ huu ambao hata Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wameendelea kuwa kwenye mntanziko mkubwa.

Kwa kawaida kampuni hizi zinakuwa na akaunti kadhaa ughaibuni na nyingine za hapa nchini.

Wageni wanapopeleka maombi ya kuja kuwinda nchini hupewa maelekezo mbalimbali yakiwamo ya namna ya kulipa.

Miongoni mwa kampuni zinazotuhumiwa iko mkoani Arusha, lakini kwa kuwa hadi tunaandaa ripoti hii ilikuwa imesita kueleza ukweli wa mapato yake na kiasi inacholipa serikalini, kwa sasa tunahifadhi jina lake.

Kwenye taarifa zake inaonyesha kuwa mgeni anayekuja kuwinda analipa kama ifuatavyo: Siku 10 malipo yake ni wastani wa dola za Marekani 44,500 (Sh milioni 103.195); siku 14 ni dola 67,000 (Sh milioni 155.373); na siku 21 ni dola 88,000 (Sh milioni 204.072). Mwishoni mwa wiki dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa Sh 2,319.

Kiwango hicho cha malipo hupungua kulingana na idadi ya wageni, pia wawindaji bingwa (PH).

Kuwapo ukwepaji kodi kumeelezwa na wageni kadhaa raia wa Marekani ambao kwa maelezo yao hawafurahishwi na wizi unaofanywa na kampuni hizo.

Mgeni huyo ameonyesha nyaraka za mawasiliano kati yake na kampuni hiyo ya Tanzania inayomilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na raia wa kigeni – Wakenya na Waingereza.

Anasema: “Mimi nilitakiwa nilipe dola 44,500 (Sh milioni 103) sawa na mwenzangu pia. Wake zetu wawili walilipa ada kama watazamaji, kila mmoja dola 4,000 za Marekani (Sh milioni 9.276).

“Tukatakiwa tulipe usafiri wa ndege kutoka Arusha hadi (jina tunalihifadhi) dola 15,000 za Marekani (Sh milioni 34.785). Jumla kuu [bila kuhusisha tozo za uwindaji] tulitakiwa tulipe dola 112,000 (Sh milioni 259.728).”

Wageni hao wakatakiwa walipe nusu ya kiwango hicho kama malipo ya awali, na kiasi kinachobaki kingelipwa baadaye.

“Tukapewa akaunti za malipo – kitu cha awali tulichobaini ni kwamba tulitakiwa kulipa kwenye akaunti iliyoko Mauritius badala ya Tanzania ambako tunakwenda kuwinda. Tukahisi kuna ujanja ujanja wa kodi unaofanywa na ndipo hapo tulikuja kubaini mambo mengi,” amesema mgeni huyo.

JAMHURI limefanikiwa kupata taarifa za akaunti hizo, moja ikiwa inaonyesha kuwa imefunguliwa MauBank Ltd. Benki hiyo iko 25, Bank Street, Cybercity. Benki nyingine inayotumika kwenye uhamishaji huo wa fedha ni JP Morgan Chase.

Mchezo unavyofanywa

Chanzo cha habari ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii kinathibitisha kuwapo kwa ukwepaji kodi kupitia mbinu hiyo.

“Haya mambo tunayajua kitambo, TRA wanajua – japo si wote; lakini kumekuwa na ugumu wa kufuatilia jambo hili.

“Wanachofanya hawa jamaa, kwa mfano mgeni akiwa Marekani, anafanya booking [miadi] na malipo kwa benki zilizo offshore. Fedha zinalipwa huko halafu wanatoa kiasi kidogo na kuleta kwenye akaunti walizofungua kwenye benki zetu za hapa nchini au Kenya.

“Kwa mfano, kama mteja amelipa dola 40,000; zinapelekwa Mauritius, na kiasi kinachotolewa huko na kuingizwa nchini kinaweza kuwa hata dola 20,000 na hicho ndicho kinachotolewa taarifa TRA kwa ajili ya kodi.

“Wakiulizwa mbona malipo yametoka benki ya offshore, majibu yao yamekuwa kwamba malipo hayo yamefanywa na wakala wao; jambo ambalo si la kweli hata kidogo,” kimesema chanzo chetu.

Hoja hiyo inathibitishwa na mgeni aliyekuja nchini kuwinda: “Sisi hatukupitia kwa wakala, tuliwasiliana na kampuni [ya uwindaji] moja kwa moja, na malipo tulitakiwa tulipe katika benki iliyoko Mauritius.”

JAMHURI limewasiliana na mamlaka husika ndani ya TRA kupata maelezo kuhusu madai haya ya ukwepaji kodi.  

Mmoja wa viongozi waandamizi wa mamlaka hiyo amejibu: “Samahani nimechelewa kujibu ujumbe wako. Nikushukuru kwa kazi nzuri unayoifanya kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya taifa letu; sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Mapato, lakini na ile ya Tax Administration Act, inatuzuia kabisa kutoa taarifa za mlipakodi kwa third party! … nitapeleka investigation team kufanya ukaguzi maalumu.”

Kwa upande wa kampuni zinazotuhumiwa, kwa mwezi mmoja sasa zimesita kujibu maswali yanayohusu tuhuma za ukwepaji kodi.

Katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2022/2023, Waziri Dk. Pindi Chana, aliliambia Bunge kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye uwindaji wa kitalii ambako maeneo saba yametolewa kwa wawekezaji chini ya utaratibu wa uwekezaji mahiri katika mapori ya akiba na tengefu.

Maeneo hayo ni mapori ya akiba Ikorongo (1), Grumeti (1), Maswa (3) na Selous (1); na Pori Tengefu la Ziwa Natron (1).

“Uwekezaji huo umeiwezesha Mamlaka kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za uwindaji wa kitalii kutoka Sh 4,294,512,390.00 kwa mwaka 2021 hadi Sh 22,109,585,590.00 mwezi Aprili, 2022,” amesema Dk. Chana.

Amesema katika kupanua wigo wa masoko ya uwindaji wa kitalii, Mamlaka imeshiriki maonyesho mbalimbali ya biashara ya kimataifa ikiwamo Safari Club International Convention, Marekani.

“Kupitia maonyesho hayo, Mamlaka imetangaza fursa za uwekezaji na kuhamasisha wafanyabiashara kuwekeza katika shughuli za utalii na uwindaji. Mamlaka imeandaa mfumo wa kidijitali unaotoa taarifa kwa wageni kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA,” amesema Dk. Chana.