Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar
Wakati Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) ukiwatoa hofu wananchi kwa kusema kuwa upo imara na himilivu, magonjwa yasiyoambukizwa yanayosababishwa na ‘tabia-bwete’ yanatajwa kuwa chanzo cha ongezeko la gharama za matibabu nchini.
Akizungumza na wahariri jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Chama cha Ugonjwa wa Kisukari ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANDA), Profesa Andrew Swai, amesema magonjwa hayo yamekuwa yakiongezeka kutokana na mtindo wa maisha.
“Ni lazima kubadili mtindo wa maisha kwa kula vyakula vyenye lishe stahiki, kuacha tabia-bwete kwa kufanya mazoezi na kuepuka msongo wa mawazo,” amesema Profesa Swai akitoa takwimu za ongezeko la magonjwa ya kisukari, moyo, figo na mengine yanayoepukika tofauti na ilivyokuwa miaka ya 1980.
Profesa Swai amesema gharama kubwa za matibabu zinatishia kuingiza familia na jamii katika umaskini na kwamba sasa serikali imetoa mwongozo wa lishe na namna ya kukabiliana na magonjwa haya.
Ametoa mfano wa gharama zinazotumiwa na NHIF kuwalipia wateja wenye magonjwa yasiyoambukiza kiasi cha kutishia uhai wa mfuko.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, ameliambia JAMHURI kuwa mfuko ni imara na himilivu licha ya kuwapo kwa changamoto za hapa na pale.
Konga amesema hatua zinazochukuliwa na serikali kwa sasa hasa kwa kupeleka bungeni muswada wa ‘Bima kwa Wote’ zitaiimarisha zaidi NHIF.
“Tupo vizuri na serikali, ambaye ni mteja wetu mkubwa kwa kuwa wafanyakazi wake wote ni wanachama wetu, imekuwa ikilipa vizuri. Tangu mwaka 2016 hadi Juni mwaka huu, haidaiwi,” amesema.
Asilimia 66 ya wanachama wa NHIF ni watumishi wa umma; asilimia 16.9 wa sekta binafsi; asilimia 7.5 ni wanafunzi na waliobaki ni watoto.
NHIF imekuwa ikipata fedha kutoka vyanzo mbalimbali kama michango ya wanachama, uwekezaji na vinginevyo huku ikiwa imesaidia kuimarisha na kuboresha huduma katika hospitali kama KCMC, Moshi na Rufaa Mbeya kupitia mikopo yenye riba nafuu.
Konga amesema NHIF inaunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza kwamba:
“Mfuko huu ndio nguzo ya afya na kimbilio la Watanzania wengi kwa kuwa tupo kila kona ya nchi kupitia vituo zaidi ya 9,100 vinavyotoa huduma ya NHIF. Ni mtandao mpana sana.”
Katika wiki kadhaa zilizopita, kumekuwa na taarifa zinazodai kuwa NHIF inakaribia kufilisika, lakini kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, hali haipo hivyo.
Taarifa hiyo inasema kufilisika kwa mfuko kunaweza kutokea iwapo tu hatua madhubuti hazitachukuliwa.
“Hatua hizo zinaanzia kwa mtu mmoja mmoja kwa kubadili mtindo wa maisha, kwa kuzingatia aina za vyakula tunavyokula, kuepuka uvutaji wa sigara na kufanya mazoezi huku serikali ikibuni mikakati ya kukinga magonjwa yasiyoambukiza,” amesema Ummy.
Ummy anakemea vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma na wanachama wa NHIF vinavyolenga kujipatia manufaa kinyume cha utaratibu, akitoa mfano wa mwaka wa fedha 2021/22 ambapo wataaluma 65 wamefikishwa katika mabaraza yao kutokana na kukiuka taratibu na miongozo ya taaluma za afya.
Changamoto nyingine amesema ni uwepo wa kundi kubwa la wananchi wanaojiunga na NHIF kwa hiari ambao, takriban asilimia 99 tayari ni wagonjwa, kutokana na kutokuwapo kwa sheria ya ulazima kwa wananchi kujiunga na Bima ya Afya.
Ametaja hatua zinazochukuliwa kuhakikisha mfuko hauyumbi kuwa ni kuimarisha afua za kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza; kuongeza idadi ya wanachama; kudhibiti vitendo vya udanganyifu; kudhibiti matumizi ya huduma yasiyo na tija; kupunguza gharama za matibabu nchini na kuwa na mfumo endelevu wa kuhakikisha mfuko unakuwa na fedha wakati wote.
“Niwatoe wasiwasi wadau wa NHIF wakiwamo wanachama, watoa huduma pamoja na Watanzania wote kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha mfuko huu unakuwa imara, endelevu na stahimilivu.
“Mfuko huu ndio tegemeo la Watanzania wengi hususan wa kipato cha chini. Na Mfuko huu pia ndio umekuwa tegemeo la vituo vya kutoa huduma za afya nchini,” amesema Waziri Ummy.