*Profesa Muhongo, Maswi waanika wanachokiamini
*Wachukizwa wanasiasa kuupotosha umma wa Watanzania
Sakata la Sh bilioni 200 kutoka katika akaunti ya Escrow, inayomilikiwa kwa pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), limeendelea kutawala kwenye mijadala ndani na nje ya Bunge.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), Mei 8, mwaka huu alikoleza moto bungeni baada ya kuwahusisha viongozi kadhaa serikalini kuwa wameshiriki kuchukua fedha hizo.
Waliotuhumiwa na Kafulila ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema; Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo; Waziri wa Fedha, Saada Mkuya; na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.
Pia alisema wamo maofisa kadhaa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kafulila anasema fedha ‘zilizoibwa’ kutoka Akaunti ya Escrow ni nyingi kuliko Sh bilioni 120 zilizoibwa kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT) mwaka 2005.
Kutokana na sakata hili kuendelea kuwachanganya wananchi, JAMHURI imefanya juhudi za kuzungumza na Waziri Profesa Muhongo na Katibu Mkuu Maswi ili kujua ukweli wa jambo hili.
Historia ya Mradi wa IPTL
Makubaliano kati ya Serikali na IPTL kuanzisha mradi wa kufua umeme wenye uwezo wa kuzalisha MW 100 yalifikiwa ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa umeme katika miaka ya 1990. Serikali ilialika sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji umeme kwa vile haikuwa na fedha za kugharimia miradi ya umeme.
Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd ya Tanzania (VIP) iliweza kuishawishi Serikali kualika Kampuni ya Mechmar Corporation ya Malasyia (MECHMAR).
Baada ya MECHMAR kuonesha kuwa inaweza kuzalisha MW 100 katika Jiji la Dar es Salaam, ilisaini makubaliano (MoU) na Serikali. Mwaka 1994 Kampuni ya MECHMAR na Kampuni ya VIP kwa pamoja zilianzisha Kampuni ya IPTL, kama kampuni binafsi iliyokuwa inamilikiwa na MECHMAR kwa asilimia 70 na VIP kwa asilimia 30.
Kampuni ya IPTL ilipewa leseni ya kujenga-kumiliki na-kuendesha (Build-Own-Operate) mtambo wa kuzalisha MW 100 za umeme wa mafuta mazito katika eneo la Tegeta-Salasala.
Waziri Muhongo anasema; “Mkataba wa kununua umeme kati ya TANESCO na IPTL (Power Purchase Agreement-PPA) ulisainiwa Mei 26, 1995 kwa kipindi cha miaka 20, ingawa utekelezaji wake ulianza mwaka 2002. Katika mkataba wa PPA, TANESCO ndiye mnunuzi pekee wa umeme kutoka mtambo wa IPTL.
“Kulingana na IPTL kutakiwa kuiuzia TANESCO umeme usiopungua asilimia 85 ya umeme unaozalishwa kila siku, pamoja na mkataba huo, Serikali ilisaini mikataba miwili ambayo ni Mkataba wa Utekelezaji (Implementation Agreement) na Mkataba wa Dhamana (Guarantee Agreement), ambako ilikusudiwa kuwa endapo TANESCO itashindwa kulipa gharama za kununua umeme, Serikali ichukue dhamana ya kulipa gharama hizo kwa niaba ya TANESCO.
“Gharama za uwekezaji wa mradi huo zilikadiriwa kuwa dola milioni 150 za Marekani. IPTL walitakiwa kutoa asilimia 30 kama mtaji na asilimia 70 kama mkopo. Makubaliano kati ya wanahisa hao ni kwamba MECHMAR watoe fedha za mtaji na mchango wa VIP uwe huduma muhimu za kuwezesha kuanzishwa kwa IPTL na eneo la kiwanja kitakachojengwa mtambo wa kuzalisha umeme huko Tegeta Salasala.
“Kwa maelezo yote hayo, utaona kuwa Serikali na TANESCO siyo wabia, bali wateja wa kampuni ya IPTL. Hata hivyo, wanahisa wa IPTL (MECHMAR na VIP) hawakutoa asilimia 30 ya mtaji kama walivyotakiwa ila waligeuza fedha za mkopo kuwa mtaji. Kwa lugha nyingine wanahisa hao walidanganyana wenyewe.”
Kwa maelezo ya Profesa Muhongo, baada ya mkataba huo kutiwa saini Februari 4, 1997; IPTL iliingia mkataba wa ujenzi (EPC Contract) na Kampuni ya Wartsila ya Uholanzi. Juni 28, 1997 IPTL iliingia mkataba wa mkopo (Syndication Loan Agreement) na umoja wa mabenki ya Malaysia kwa ajili ya mkopo wa dola milioni 105 za Marekani ikiwa ni asilimia 70 ya mtaji wa IPTL.
Hata hivyo, anasema IPTL walitakiwa kuchukua dola 85,862,022.08 za Marekani kutoka dola milioni 105 za Marekani zilizotolewa kama mkopo.
“Si Serikali wala TANESCO waliokuwa sehemu ya mkataba huo. Mkopo huo ulitakiwa kurudishwa katika kipindi cha miaka minane na riba ilikuwa asilimia 2.5 kwa mwaka. Grace period ya mkopo huo ilikuwa miezi 18. Dhamana ya mkopo ilikuwa kiwanja cha Tegeta ambako mtambo wa kuzalisha umeme utawekwa pamoja na mtambo wa kuzalisha umeme. Mradi wa IPTL ulianza uzalishaji umeme Januari, 2002 na ndiyo utekelezaji wa mkataba ulipoanza,” anasema Profesa Muhongo.
Anasema kulingana na PPA, malipo ya gharama za umeme ambazo TANESCO inatakiwa kulipa ni ya aina mbili — energy na capacity charges. Capacity charge ni gharama za uendeshaji na matengenezo (O&M) pamoja na vilainishi, ambazo zinalipwa hata kama TANESCO haitumii umeme unaozalishwa na IPTL. Energy charges ni gharama za kuzalisha umeme ambazo TANESCO inalipa ikitumia umeme wa IPTL.
Ujenzi wa mtambo ulianza mwaka 1997 na kukamilika mwaka uliofuata, lakini uzalishaji ulianza Februari 15, 2002 (Commercial Operational Date). Mtambo ulichelewa kuanza uzalishaji kutokana na mgogoro kati ya TANESCO na IPTL katika Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID).
Akaunti ya Escrow
Katibu Mkuu Maswi anasema Akaunti ya Escrow ilifunguliwa katika BoT baada ya mkataba wa Escrow kusainiwa na Serikali (kwa niaba ya TANESCO), IPTL na BoT, Julai 5, 2006.
“Kufunguliwa kwa akaunti ya Escrow kulitokana na ushauri wa Mkono and & Co. Advocates in association with Denton Wilde Sapte wa Juni 30, 2004. Ushauri huo upo kwenye kifungu cha 10.1 na 10.2.
“Mkataba wa Escrow ulitokana na Mkataba wa Ununuzi wa Umeme kati ya TANESCO na IPTL uliosainiwa Mei 26, 1995. Kulingana na kifungu Na. 6.8 cha PPA, kinachoeleza kuwa iwapo pande mbili za mkataba hazikubaliani na gharama za umeme, fedha za gharama za umeme zilipwe kwenye akaunti ya Escrow hadi hapo mgogoro wa malipo utakapotatuliwa.
“Fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow zilikuwa zinalipwa na TANESCO kutokana na mgogoro wa gharama za malipo kati ya TANESCO na IPTL. TANESCO ilidai kuwa inalipa gharama za juu kutokana na IPTL kutumia fedha za mkopo kama mtaji, kukokotoa gharama za umeme wakati fedha halisi za mtaji wa IPTL si zaidi ya dola 1,000 za Marekani.
“IPTL walikuwa wakidai kuwa fedha za mkopo zihesabiwe kama mtaji kukokotoa gharama za umeme. Aidha, TANESCO walikuwa wakilipa fedha kwenye akaunti ya Escrow kuanzia Septemba 22, 2006 hadi Agosti 2009 walipoacha kuweka fedha kwenye akaunti hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo IPTL kuwa kwenye ufilisi na kuendelea kutoa dispute notice kwa ushauri wa wakili wao kulingana na kifungu cha XXII cha “Implementation Agreement” ya Julai 8, 1995 kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na IPTL, Serikali ilitoa dhamana (guarantee) kulipa fedha yoyote ambayo TANESCO itashindwa kulipa kama itatokea hivyo na siyo kama IPTL itakopa au mtu yeyote atakopa kwa niaba ya IPTL.
“Dhamana ya Serikali ilihusu ‘capacity charge’ na si vinginevyo. Mkopeshaji yeyote ambaye siyo sehemu ya PPA hawezi kujigeuza na kudai ni sehemu ya mkataba huu. Mawakili (Mkono & Company Advocates) wetu wanaelewa hivyo, lakini hawataki kusema kwa kuwa watapoteza au kuacha kulipwa na Serikali pamoja na TANESCO,” anasema Maswi na kuongeza:
“Kwa maelezo hayo, na kwa mtazamo wangu, kampuni pekee inayonufaika na dhamana ya Serikali ni IPTL au yeyote atakayekuwa anamiliki IPTL na Serikali pia ilikubali kulingana na sheria za nchi.”
Profesa Muhongo anasema, “Ni vizuri ikaeleweka kuwa akaunti ya Escrow ilifunguliwa kutokana na ‘dispute’ iliyotolewa na TANESCO na sasa, ‘dispute’ haipo, na hivyo Serikali yoyote makini haina sababu ya kuzuia fedha ambazo zipo kwenye akaunti ya Escrow kwa sababu yoyote ile.
“IPTL ni kampuni binafsi na siyo kampuni ya Serikali, na TANESCO kama mnunuzi wa umeme, wajibu wake ni kununua umeme na siyo kuingilia masuala ya ndani ya kampuni. Kama ‘dispute’ imeisha, sasa fedha hizo zinazuiwa ili ziende wapi na zifanye nini?” Anahoji.
Hukumu ya Mahakama
Profesa Muhongo anasema, “Katika hukumu yake, ya Septemba 5, 2013 na pia ‘consent order’ iliyotolewa na Jaji Utamwa J, Januari 17, 2014, katika kesi yake Misc. Civil Case No.49/2002 na Misc. Civil Case No.254/2003 states ‘Among other prayers that, by this settlement order, parties have discharged all of their respective outstanding performance obligations required in completion of execution of the contract”.
“Hatuamini kama Bunge letu Tukufu lingependa kuhoji uamuzi wa Mahakama. Ninaamini Mahakama zetu zina uhuru wa kutoa uamuzi wowote na kulinda haki za wananchi.
“Vyama vya Upinzani wakifukuzana kwenye ubunge (kama ilivyo kwa Mheshimiwa Zitto Kabwe na Mheshimiwa David Kafulila) hukimbilia mahakamani na wanapopewa haki hawalalamiki – huona ni sawa, lakini katika kesi hii kati ya VIP na IPTL imeisha na Mahakama imeamua — hatutaki kukubali. Tumefikia mahali hatuiamini Mahakama kama chombo cha kutoa haki? Kwa nini hakuna aliyekata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama?”
Profesa Muhongo anasema, “Kwa mujibu wa Hati ya Makabidhiano (Handing Over Note) ya Septemba 5, 2013, IPTL inaonesha inaidai TANESCO Sh 370,738,773,651.09 sawa na dola milioni 227.45 za Marekani kufikia Septemba 5, mwaka huo.
“Kutokana na hukumu ya Mheshimiwa Jaji Utamwa ya Septemba 05, 2013 kuondoa IPTL kwenye ufilisi na kutambua PAP kama mmiliki kwa asilimia 100 wa IPTL, TANESCO ilifanya mazungumzo na IPTL kwa ajili usuluhisho wa hesabu ya fedha ambazo TANESCO ilikuwa haijaweka kwenye Akaunti ya Escrow na kukubaliana jinsi ya kulipa fedha hizo.
“Kwa mujibu wa Hati ya Makabidhiano ya Septemba 5, 2013, IPTL ilionesha inaidai TANESCO Sh 370,738,773,651.09 ambazo ni sawa na dola milioni 227.45 za Marekani kufikia Septemba 05, 2013.
“Aidha, kwa mujibu wa barua ya IPTL ya Septemba 20, 2013, IPTL wanaidai TANESCO dola milioni 239.6 za Marekani na Sh 33,370,147,675.88 kama ‘capacity charges’. Hata hivyo, baada ya TANESCO kukaa na kufanya hesabu upya na IPTL; walikubaliana kuwa madai halali ya IPTL ni dola milioni 79.05 za Marekani.”
Akaunti ya Escrow ilipofungwa Desemba, mwaka jana kulikuwa na dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh 161,359,686,585.34 (ambazo ni sawa na dola milioni 122 za Marekani).
“Baada ya makubaliano kati ya TANESCO na IPTL, Serikali ilisaini makubaliano na IPTL ya kuruhusu fedha za Escrow zilipwe kwa IPTL na kuagiza BoT kulipa fedha hizo kwa IPTL na kufunga akaunti hiyo,” anasema Profesa Muhongo.
Anahitimisha kwa kusema, “Napenda kusisitiza kuwa IPTL ni kampuni binafsi ya kuzalisha umeme kama ilivyo kampuni ya Symbion na Songas. Serikali haijihusishi na masuala binafsi ya kampuni hizo. Migogoro iliyopo ni kati ya Benki ya Standard Chartered Hong Kong na IPTL, Serikali si sehemu ya mgogoro huo.
“Viongozi na wananchi ni vizuri wakaheshimu Mahakama zetu na wasipende kuwa wasemaji tu bila uhakika. Hali hii ni hatari hasa habari zenyewe zinapokuwa zimepatikana mitaani. Kama wanaosema wangekuja kupata ufafanuzi wa aina hii jamii isingepotoshwa kama ilivyo sasa,” anasema Profesa Muhongo.