Mwalimu Julius Nyerere, ambaye Mheshimiwa James Lembeli amewahi kujifananisha naye, aliwahi kusema kuwa ikitokea mtu wa kawaida akampiga mkewe hadharani, hii haiwezi kuwashughulisha watu na wala haiwezi kuwa habari. Lakini ikatokea yeye (Mwalimu) akafanya hivyo, basi hiyo itakuwa habari kubwa mno.

Mwalimu aliyasema hayo akiwaasa viongozi wa umma kuwa makini sana na vitendo wanavyofanya kwani maisha ya kiongozi, yakiwamo maisha binafsi, siku zote yatabaki kuwa na uzito na maslahi kwa umma. Kwa hiyo lazima lolote atakalofanya kiongozi litahojiwa.

Kwa muktadha huo, waziri au mbunge anayelewa na kutukana ovyo hawezi kuchukuliwa kama mwanakijiji wa kawaida kule Maganzo, Shinyanga. Vilevile mbunge au waziri mwongo, mzushi, tapeli, mwizi, mzinzi, mroho na kadhalika atahukumiwa tofauti na atakavyohukumiwa mwanakijiji wa Kisungule kule Namtumbo.

Mantiki ya nadharia hii ni kwamba madhara yanayosababishwa na kiongozi aliyekosa maadili ni makubwa zaidi kuliko yale ya mtu wa kawaida. Kiongozi ni kioo cha jamii na hivyo lolote analofanya linaweza kuchukuliwa kuwa sahihi. Kiongozi anaaminiwa na hivyo ni rahisi kwake kuipotosha jamii.

Zimeibuliwa tuhuma kadhaa dhidi ya Lembeli, Mbunge wa Kahama na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. Tuhuma hizi ni nzito na kwa kiasi kikubwa zinachafua Bunge letu, moja ya mihimili mitatu ya dola.

Lembeli anadaiwa kuuhadaa umma kiasi cha kuonekana kama msomi, mcha Mungu, mwadilifu, mkweli, mtetezi wa wanyonge, mzalendo na ‘mtambo’ wa kupambana na ufisadi! Ni kutokana na sifa hizi zinazotajwa na baadhi ya watu kwamba ni za kutunga, Lembeli amewahi kushika nyadhifa za juu katika taasisi kadhaa.

Nitajadili utata kuhusu elimu ya Lembeli kama unavyoonekana kwenye taarifa zake alizotoa mwenyewe kwa vyombo viwili anavyohusiana navyo. Vyombo hivyo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambako yeye ni Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira; na asasi ya Afrika Kusini inayoitwa African Parks Network (APN) ambako yeye ni Mjumbe wa Bodi.

Wasifu (CV) wa Lembeli kwenye tovuti ya Bunge unaonesha kuwa alisoma na kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Njombe. Aidha, alihitimu Diploma ya Uandishi wa Habari huko Kitwe, Zambia. Maelezo (profile) yake kwenye tovuti ya APN yanaonesha kuwa alisoma na kuhitimu Diploma ya Uandishi wa Habari hapa Tanzania; na sasa anachukua Shahada ya Uzamili ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Leicester, Uingereza.

Nataka kuamini kuwa maelezo haya yanayokinzana ameyatoa Lembeli mwenyewe kwa kuwa yamekuwa kwenye tovuti kwa muda mrefu sasa na hajajishughulisha kuyaweka sawa kama kweli yalikuwa na dosari.

Lembeli amekuwa akijinadi kuwa mkweli na itakumbukwa kuwa sababu yake kubwa ya kutaka Profesa Alexander Songorwa awajibishwe ni kitendo cha kukosea jina la mmoja wa walioumia wakati wa Operesheni Tokomeza. Ingawa kukosea jina la mtu ni bahati mbaya, Lembeli alikomalia hilo na hatimaye katika mazingira yenye utata alimghilibu rafiki yake, Lazaro Nyalandu, amng’oe Songorwa kwenye wadhifa wa ukurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.

Itakumbukwa kuwa siku za nyuma Bunge lilikumbwa na kashfa kutokana na baadhi ya wabunge kudanganya na hata kufikia kughushi vyeti vya taaluma. Wapo waliofikia kudai kuwa watunukiwe PhD za heshima kutokana na umuhimu wao katika jamii! Ni kipindi hiki ambapo tulishuhudia kila uchao tunatangaziwa kuwa fulani sasa kawa ‘dokta’! Waliona kuwa uheshimiwa pekee hautoshi bila kibwagizo cha udokta! Waliouliza kuwa madaktari hawa walisoma wapi na thesis zao ziko wapi, walionekana wachimvi.

Kutokana na maelezo yaliyo kwenye tovuti ya Bunge na ile ya APN, ni wazi kuwa historia ya elimu ya Lembeli inatia shaka. Mlolongo wa elimu yetu unaonesha kuwa stashahada (diploma) inapatikana baada ya kumaliza kidato cha sita au kusoma astashahada (certificate). CV ya Lembeli inaonesha kuwa kapata diploma yake moja kwa moja baada ya kuhitimu kidato cha nne. Hasemi kuwa alisoma wapi kidato cha sita au astashahada!

Lakini pia, kwa nini Lembeli asiwe wazi juu ya nchi alikosoma diploma? Ni Zambia au Tanzania? Je, mtu akisema kuwa anadhani kuwa diploma ya Lembeli ni ya kuchonga atakuwa amekosea nini? Je, hakuna kila sababu Bunge na Takukuru kujiridhisha juu ya uhalali wa elimu ya watu hawa akiwamo Lembeli?

Kwa kutumia ujanja huo huo, Lembeli anatujuza kwamba sasa anafanya Shahada ya Uzamili ya Mawasiliano huko Uingereza! Hataki kusema aliposoma shahada ya kwanza. Je, shahada ya kwanza kwake haina ulazima na umuhimu? Inaeleweka kuwa siku hizi kuna shahada (degree) za kununua sokoni kama nyanya. Je, Lembeli anatutoaje wasiwasi kuwa si mmoja wa wanunuzi wa shahada hizi, hasa ikitiliwa maanani kwamba historia kuhusu taaluma yake tayari imeingia doa?

Lembeli amewahi kuwa Afisa Uhusiano kwenye vyama vya ushirika na ‘Chief Manager’ wa Uhusiano wa Umma Tanapa. Bila shaka nafasi hizi alizipata kutokana na diploma ambayo kwetu kama umma tunaona ina utata kutokana na kutowekwa wazi kuwa aliipata wapi na ilikuwaje akaipata kwa kuruka baadhi ya hatua kama elimu ya kidato cha sita au astashahada.

Nataka kuamini kwamba diploma hii ndiyo iliyofanya Lembeli akaajiriwa Tanapa. Hata hivyo, inasemekana kuwa baadaye Lembeli aliingia kwenye mgogoro na mwajiri wake na moja ya masuala yaliyojitokeza ni utata kuhusu elimu yake. Baada ya mambo kuwa mazito alitimkia kwenye siasa na hivyo mjadala kuhusu elimu yake ukafa kifo cha kawaida.

Ni ajira ya Tanapa iliyotokana na diploma yenye utata iliyomfanya Lembeli aaminike kama mtaalamu wa uhifadhi wa wanyamapori na hatimaye kupata uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. Ni uenyekiti huu uliomfanya awanyanyase na awajengee ‘fitna’ na ‘mizengwe’ watendaji waadilifu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, walioonekana kuwa kikwazo kwake katika kufikia malengo yake ya kiuchumi.

Ni uenyekiti huu wa Kamati uliozaliwa na diploma ‘isiyoeleweka’ ambao anautumia kulazimisha aogopwe na kupewa safari za nje ya nchi na wizara ili kumziba mdomo. Ni uenyekiti huu ambao amekuwa akiutumia kama fimbo kulazimisha apewe uenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori (TWPF) na kumnyanyasa yule anayeshauri kuwa kumpa uenyekiti wa Bodi kutazua mgongano wa maslahi kiutendaji.

Ni uenyekiti wa Kamati uliozaliwa na diploma ‘tata’ uliomsaidia Lembeli kupewa zawadi ya ujumbe wa Bodi ya APN ili afanikishe mchakato wa kukabidhi mbuga zetu kwa makaburu wa Afrika Kusini. Nasema ni zawadi yenye lengo maalum kwa kuwa Lembeli hana taaluma ya uhifadhi hata chembe. Na Tanzania haina ukame wa wataalamu waliobobea katika fani ya uhifadhi. Kuwa Afisa Uhusiano Tanapa hakumfanyi mtu kuwa mtaalamu wa uhifadhi kama ambavyo huwezi kujiita wakili kwa kuwa eti umewahi kuwa dereva wa jaji.

Diploma hii ya Lembeli ndiyo iliyompa imani kuwa anaweza kuwa waziri siku moja. Na hii ndiyo sababu ya kuwasimamia kooni kwa hila mbaya mawaziri kadhaa akiamini kuwa siku moja atapewa uwaziri ili anyamaze. Mbinu hii ilifanikiwa kwa baadhi ya wabunge, kama kina Njelu Kasaka na Philip Marmo, lakini kwa Lembeli imegonga mwamba. Na Nyalandu alilijua fika hili. Ndiyo maana mara tu alipojiuzulu Balozi Khamis Kagasheki, Nyalandu alihakikisha kuwa ‘anamwaga sumu’ kali akimtuhumu Lembeli na Kamati yake kwa kuongopa kuhusu Operesheni Tokomeza.

Nyalandu alijua kuwa pamoja na utata wa elimu yake, Lembeli anautaka uwaziri kwa udi na uvumba na hivyo alimuona kama mshindani wake. Baada ya kuukwaa uwaziri, Nyalandu akaamua kutafuta maridhiano na Lembeli ambaye hakukataa kwa kuwa bado alijua kuwa anamhitaji Nyalandu ili kufanikisha ‘dili’ zake nyingine kama ile ya kukabidhi hifadhi kwa wafadhili wake ambao ni APN. Kwa upande wa Nyalandu alijua uwaziri wake usingedumu bila kumnasa Lembeli.

Uenyekiti wa Kamati uliotokana na diploma ndiyo umemfanya Lembeli aweze kujenga uswahiba na kampuni za uwindaji wa kitalii na hivyo kunufaika nazo kisiasa na kiuchumi. Ndiyo maana hawezi kusema hadharani kuwa anahusika vipi na mgogoro wa uwekezaji katika Eneo la Hifadhi ya Jamii Makao, Meatu. Ndiyo maana hakuona soni kuchomeka suala hili kwenye Ripoti yake ya Operesheni Tokomeza japo halikuwa na uhusiano wowote na ujangili! Ndiyo maana hasemi kuwa uswahiba wake na marehemu Nyaga Mawalla ulianzaje.

Si dhambi kuamini kuwa uenyekiti wa Kamati uliozaliwa na diploma hii tata ya Lembeli ndiyo umechangia kufanikisha kuundwa genge la “utatu” kati yake, Peter Msigwa na Nyalandu ili kujijengea mazingira ya kunufaika kiuchumi kutokana na urithi wetu na kwa gharama kubwa kwa Taifa letu.

Je, Lembeli anaweza kueleza kuwa utatu huu unatokana na nini hasa? Sasa hivi hatukosi kuwaona watu hawa watatu wakiwa pamoja katika hafla tofauti tofauti. Tuliwaona wakiwa pamoja Mwanza mara tu Nyalandu alipopata uwaziri; tumewaona wakimsindikiza rafiki yao kupokea helikopta Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA); na hazikupita siku wakaonekana wakiwa pamoja kwenye mahafali huko Pasiansi, Mwanza. Kuna nini hapa? Ni uzalendo wao kwa nchi hii? Wanakwenda huko bure? Nani anawalipa Lembeli na Msigwa katika shughuli hizi? Kama ni Nyalandu, tunatarajia waweze kuhoji lolote dhidi ya Nyalandu? Hawawezi.

Lembeli anatajwa kuwa mtu wa fitna, visasi, uzushi, majungu, ubabe, na mpenda pesa.

Huenda Lembeli anayo diploma au hana. Ninachosisitiza hapa ni yeye kututoa shaka juu ya uhalali wa diploma hiyo kwa kuwa mazingira ya upatikanaji wake na alipoipatia vinatia shaka. Ni wajibu wake kufanya hivyo kama kiongozi wa umma. Katuwekea taarifa hizi kwenye tovuti ili tujue, na sisi tuna haki ya kuhoji chochote tusichokielewa hasa kinapogongana.

Ukichunguza sana utaona kuwa baadhi ya waheshimiwa wanasiasa wetu hasa wabunge wenye upungufu kitaaluma ndiyo wanaoongoza kwa majungu na kupiga kelele. Wanajua kuwa kinachowaweka mjini/mjengoni ni kelele! Wengi wao ndiyo wanaotumiwa ili kupitisha au kukwamisha hoja. Kazi inakuwa kubwa zaidi pale sifa za elimu zinapokuwa za kughushi kwa kuwa wahusika hutaka kuonesha umma kuwa wamesoma na kuelimika!

Kwa jumla, kwa kutumia hila, Lembeli amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuuhadaa umma. Amethubutu hata kujifananisha na Mwalimu Nyerere, jambo ambalo limekera watu na hata baadhi ya waandishi wamelieleza kama kufuru na kutahadharisha kwamba kumfananisha Lembeli na Nyerere ni sawa na kufananisha giza na mwanga.

Binafsi nitamsamehe Lembeli kwa dhambi zote alizotutendea Watanzania. Dhambi ambayo siko tayari kumsamehe ni endapo atakuwa amedanganya kuhusu elimu yake. Kama ni kweli kadanganya ni wazi kuwa madhara yake ni haya tunayoyaona. Ni dhahiri kuwa atakuwa ametumia ‘diploma tata’ kupora madaraka na nyadhifa ambazo amezitumia vibaya kuumiza watu binafsi na Taifa zima. Ni juu ya Lembeli kututhibitishia kuwa diploma yake haina shaka hata chembe na kwamba tuhuma zinazoelekezwa kwake hazihusiani na elimu ya kughushi.

Katika makala kadhaa zilizopita waungwana walimshauri Lembeli kujipima kama bado anatosha kuendelea kukalia kiti cha Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. Naamini kuwa walifanya hivi kwa nia njema kabisa na hasa ikizingatiwa kuwa yeye mwenyewe amekuwa akitumia maneno hayo hayo dhidi ya viongozi asiowataka. Hufanya hivi akijua kuwa hasemi ukweli. Kwa bahati mbaya Lembeli amegeuka ‘kichwa ngumu’ ingawa anajua wazi kuwa nyingi ya tuhuma dhidi yake ni za kweli.